Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 28:15-25

1 Samweli 28:15-25 NENO

Samweli akamuuliza Sauli, “Kwa nini unanitaabisha kwa kunipandisha juu?” Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena kupitia manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe la kufanya.” Samweli akamuuliza, “Kwa nini uniulize mimi, kuona Mwenyezi Mungu amekuacha na kuwa adui yako? Mwenyezi Mungu ametenda lile alilotangulia kusema kupitia kwangu. Mwenyezi Mungu ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa majirani zako, yaani Daudi. Kwa sababu wewe hukumtii Mwenyezi Mungu, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, Mwenyezi Mungu amekutendea mambo haya leo. Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu atawatia Israeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti, na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Mwenyezi Mungu pia atalitia jeshi la Israeli mikononi mwa Wafilisti.” Papo hapo Sauli akaanguka chini, akajinyoosha, akiwa amejawa na hofu kwa ajili ya maneno ya Samweli. Nguvu zake zikamwishia kwa maana alikuwa hajala chochote mchana ule wote na usiku. Yule mwanamke alipomwendea Sauli na kumwona amepatwa na hofu, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako mwanamke nimekutii. Nimeweka maisha yangu hatarini kwa kufanya kile ulichoniagiza nifanye. Sasa tafadhali isikilize sauti ya mtumishi wako, uniruhusu nikupatie chakula kidogo ule ili uwe na nguvu za kurejea ulikotoka.” Akakataa, akisema, “Mimi sitaki kula.” Lakini watumishi wake wakaungana na yule mwanamke wakamsihi ale, naye akakubali. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda. Yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona hapo nyumbani, akamchinja mara moja. Akachukua unga, akaukanda, akatengeneza mkate usio chachu. Ndipo akamwandalia meza Sauli pamoja na watu wake, nao wakala. Usiku ule ule wakainuka na kwenda zao.