1 Samweli 28
28
1Siku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.”
2Daudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.”
Akishi akamjibu Daudi, “Vyema sana, mimi nitakufanya uwe mlinzi wangu daima.”
Sauli na mchawi wa Endori
3Wakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Waisraeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi.
4Wafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa. 5Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu. 6Ndipo Sauli akauliza ushauri kwa Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu#28:6 Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha., wala kupitia manabii. 7Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.”
Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.”
8Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.”
9Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?”
10Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina la Mwenyezi Mungu, akasema, “Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.”
11Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?”
Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.”
12Yule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.”
13Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?”
Yule mwanamke akasema, “Naona mungu unapanda kutoka ardhini.”
14Sauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?”
Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.”
Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu, uso wake ukagusa chini.
15Samweli akamuuliza Sauli, “Kwa nini unanitaabisha kwa kunipandisha juu?”
Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena kupitia manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe la kufanya.”
16Samweli akamuuliza, “Kwa nini uniulize mimi, kuona Mwenyezi Mungu amekuacha na kuwa adui yako? 17Mwenyezi Mungu ametenda lile alilotangulia kusema kupitia kwangu. Mwenyezi Mungu ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa majirani zako, yaani Daudi. 18Kwa sababu wewe hukumtii Mwenyezi Mungu, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, Mwenyezi Mungu amekutendea mambo haya leo. 19Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu atawatia Israeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti, na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Mwenyezi Mungu pia atalitia jeshi la Israeli mikononi mwa Wafilisti.”
20Papo hapo Sauli akaanguka chini, akajinyoosha, akiwa amejawa na hofu kwa ajili ya maneno ya Samweli. Nguvu zake zikamwishia kwa maana alikuwa hajala chochote mchana ule wote na usiku.
21Yule mwanamke alipomwendea Sauli na kumwona amepatwa na hofu, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako mwanamke nimekutii. Nimeweka maisha yangu hatarini kwa kufanya kile ulichoniagiza nifanye. 22Sasa tafadhali isikilize sauti ya mtumishi wako, uniruhusu nikupatie chakula kidogo ule ili uwe na nguvu za kurejea ulikotoka.”
23Akakataa, akisema, “Mimi sitaki kula.”
Lakini watumishi wake wakaungana na yule mwanamke wakamsihi ale, naye akakubali. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.
24Yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona hapo nyumbani, akamchinja mara moja. Akachukua unga, akaukanda, akatengeneza mkate usio chachu. 25Ndipo akamwandalia meza Sauli pamoja na watu wake, nao wakala. Usiku ule ule wakainuka na kwenda zao.
Iliyochaguliwa sasa
1 Samweli 28: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.