1 Samweli 26:1-12
1 Samweli 26:1-12 NEN
Hao Wazifu wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kinachotazamana na Yeshimoni?” Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na watu wake 3,000 wa Israeli waliochaguliwa, kumsaka Daudi huko. Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko, Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka. Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?” Abishai akajibu, “Nitakwenda pamoja nawe.” Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli. Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome mpaka ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.” Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa BWANA na asiwe na hatia?” Daudi akasema, “Hakika kama vile BWANA aishivyo, BWANA mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au atakwenda vitani na kuangamia. Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa BWANA. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.” Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu BWANA alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito.