Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 26:1-12

1 Samueli 26:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Baadhi ya wanaume kutoka mji wa Zifu walimwendea Shauli huko Gibea wakamwambia kwamba Daudi alikuwa anajificha kwenye mlima Hakila, upande wa mashariki wa Yeshimoni. Mara moja, Shauli alikwenda kwenye nyika za Zifu kumtafuta Daudi akiwa na askari waliochaguliwa 3,000 wa Israeli. Shauli akapiga kambi juu ya mlima Hakila, karibu na barabara, mashariki ya Yeshimoni. Lakini Daudi alikuwa bado huko nyikani. Daudi alipojua kwamba Shauli alikuwa amekuja nyikani kumtafuta, alituma wapelelezi, akafahamishwa kwamba ni kweli. Daudi akatoka, akaenda mahali Shauli alipopiga kambi. Akapaona mahali ambapo Shauli alikuwa amelala na Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli, alikuwa amelala karibu na Shauli. Shauli alikuwa amelala katikati ya kambi huku akizungukwa na jeshi lake. Daudi akamwambia Ahimeleki ambaye alikuwa, Mhiti, na Abishai ndugu yake Yoabu (mama yao aliitwa Seruya), “Nani atakwenda pamoja nami kwenye kambi ya Shauli?” Abishai akamwambia; “Mimi nitakwenda pamoja nawe.” Hivyo usiku, Daudi na Abishai wakaingia kwenye kambi ya Shauli, wakamkuta Shauli amelala katikati ya kambi hiyo, na mkuki wake umechomekwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri pamoja na askari walikuwa wamelala kumzunguka Shauli. Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Basi, niache nimbane udongoni kwa pigo moja tu la mkuki; sitampiga mara mbili.” Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; maana hakika Mwenyezi-Mungu atamwadhibu mtu yeyote atakayeunyosha mkono wake dhidi ya mteule wake aliyepakwa mafuta. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba Mwenyezi-Mungu mwenyewe atamuua Sauli; ama siku yake ya kufa itafika, au atakwenda vitani na kufia huko. Lakini Mwenyezi-Mungu anakataza nisinyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye amemteua kwa kumpaka mafuta. Lakini chukua mkuki wake ulio karibu na kichwa chake pamoja na gudulia lake la maji, halafu tujiendee zetu.” Hivyo, Daudi alichukua ule mkuki na gudulia la maji karibu na kichwa cha Shauli nao wakajiendea zao. Lakini hakuna mtu aliyeona au kujua tukio hilo, wala hakuna aliyeamka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu aliwaletea usingizi mzito.

1 Samueli 26:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi hao Wazifi wakamwendea Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kuelekea Yeshimoni? Basi Sauli akaondoka, akashuka nyikani kwa Zifu, naye alikuwa na watu elfu tatu, wateule wa Israeli, pamoja naye, ili kumtafuta Daudi katika nyika ya Zifu. Naye Sauli akapiga hema katika kilima cha Hakila, kilichoelekea Yeshimoni, barabarani; lakini Daudi alikuwa akikaa nyikani, akaona ya kwamba Sauli amemfuata mpaka nyikani. Basi Daudi akatuma wapelelezi, akapata habari ya hakika ya kwamba Sauli amefika. Daudi akainuka, akafika mahali pale alipotua Sauli; Daudi akapaangalia mahali alipolala Sauli, na Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi lake; naye Sauli alikuwa amelala kati ya magari, na hao watu wamepiga hema zao wakimzunguka. Ndipo Daudi akajibu, akamwambia Ahimeleki, Mhiti, na Abishai, mwana wa Seruya, ndugu yake Yoabu, akisema, Ni nani atakayeshuka pamoja nami kwa Sauli kambini? Abishai akasema, Mimi nitashuka pamoja nawe. Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama, Sauli alikuwapo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake; naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka. Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hadi chini kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili. Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa BWANA, naye akawa hana hatia? Daudi akasema, Aishivyo BWANA, BWANA atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea. Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa BWANA; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu. Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa BWANA umewaangukia.

1 Samueli 26:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi hao Wazifi wakamwendea Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kuelekea Yeshimoni? Basi Sauli akaondoka, akashuka nyikani kwa Zifu, naye alikuwa na watu elfu tatu, wateule wa Israeli, pamoja naye, ili kumtafuta Daudi katika nyika ya Zifu. Naye Sauli akapiga hema katika kilima cha Hakila, kilichoelekea Yeshimoni, barabarani; lakini Daudi alikuwa akikaa nyikani, akaona ya kwamba Sauli amemfuata mpaka nyikani. Basi Daudi akatuma wapelelezi, akapata habari ya hakika ya kwamba Sauli amefika. Daudi akainuka, akafika mahali pale alipotua Sauli; Daudi akapaangalia mahali alipolala Sauli, na Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi lake; naye Sauli alikuwa amelala kati ya magari, na hao watu wamepiga hema zao wakimzunguka. Ndipo Daudi akajibu, akamwambia Ahimeleki, Mhiti, na Abishai, mwana wa Seruya, ndugu yake Yoabu, akisema, Ni nani atakayeshuka pamoja nami kwa Sauli kambini? Abishai akasema, Mimi nitashuka pamoja nawe. Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama, Sauli alikuwapo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake; naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka. Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili. Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa BWANA, naye akawa hana hatia? Daudi akasema, Aishivyo BWANA, BWANA atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea. Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa BWANA; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu. Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa BWANA umewaangukia.

1 Samueli 26:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hao Wazifu wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kinachotazamana na Yeshimoni?” Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na watu wake 3,000 wa Israeli waliochaguliwa, kumsaka Daudi huko. Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko, Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka. Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?” Abishai akajibu, “Nitakwenda pamoja nawe.” Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli. Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome mpaka ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.” Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa BWANA na asiwe na hatia?” Daudi akasema, “Hakika kama vile BWANA aishivyo, BWANA mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au atakwenda vitani na kuangamia. Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa BWANA. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.” Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu BWANA alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito.