1 Samweli 20
20
Daudi na Yonathani
1Kisha Daudi akakimbia kutoka Nayothi huko Rama akamwendea Yonathani na kumuuliza, “Kwani nimefanya nini? Kosa langu ni nini? Nimemkosea baba yako kwa jinsi gani, hata kwamba anajaribu kuniua?”
2Yonathani akajibu, “La hasha! Hutakufa! Tazama, baba yangu hafanyi kitu chochote, kikubwa au kidogo, bila kuniambia mimi. Kwa nini anifiche hili? Sivyo ilivyo!”
3Lakini Daudi akaapa na kusema, “Baba yako anajua kabisa kwamba nimepata kibali mbele yako, naye amesema moyoni mwake, ‘Yonathani sharti asilijue hili, la sivyo atahuzunika.’ Lakini hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na kama uishivyo, kuna hatua moja tu kati yangu na mauti.”
4Yonathani akamwambia Daudi, “Chochote unachotaka nifanye, nitakufanyia.”
5Basi Daudi akamwambia Yonathani, “Angalia, kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo, nami inanipasa kula chakula pamoja na mfalme; lakini niache niende kujificha shambani hadi kesho kutwa. 6Kama baba yako akiona ya kuwa sipo, mwambie, ‘Daudi aliniomba sana ruhusa kuwahi Bethlehemu, mji wake wa nyumbani, kwa sababu dhabihu ya mwaka inafanywa huko kwa ajili ya ukoo wake wote.’ 7Akisema, ‘Ni vyema sana,’ basi mtumishi wako yu salama. Lakini akikasirika, unaweza kuwa na hakika kwamba anakusudia kunidhuru. 8Kwako wewe, mtende wema mtumishi wako, kwa sababu mmeingia kwenye agano naye mbele za Mwenyezi Mungu. Nikiwa na hatia, basi niue wewe mwenyewe! Kwa nini unikabidhi kwa baba yako?”
9Yonathani akasema, “La hasha! Kama ningekuwa na kidokezo kidogo kwamba baba yangu amekusudia kukudhuru wewe, je, nisingekuambia?”
10Daudi akamuuliza Yonathani, “Je, nani atakayeniambia kama baba yako atakujibu kwa ukali?”
11Yonathani akamwambia, “Njoo, twende shambani.” Basi wakaenda huko pamoja.
12Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Ninakuahidi kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hakika nitamchunguza baba yangu wakati kama huu kesho kutwa! Kama ameweka utaratibu wa kufaa kukuhusu wewe, je, sitakutumia ujumbe na kukufahamisha? 13Lakini ikiwa baba yangu amenuia kukudhuru, Mwenyezi Mungu na aniadhibu vikali zaidi iwapo sitakufahamisha na kukuaga uende salama. Mwenyezi Mungu na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu. 14Lakini nitendee wema usiokoma kama ule wa Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yangu, ili nisije nikauawa, 15wala usiuondoe wema wako kwa jamaa yangu, hata kama ni wakati ule Mwenyezi Mungu atakapokuwa amekatilia mbali kila adui wa Daudi kutoka uso wa dunia.”
16Basi Yonathani akafanya agano na nyumba ya Daudi, akisema: “Mwenyezi Mungu na awaangamize adui za Daudi.” 17Naye Yonathani akamtaka Daudi athibitishe tena kiapo chake cha kumpenda, kwa sababu Yonathani alimpenda Daudi kama nafsi yake mwenyewe.
18Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo. Itajulikana kwamba haupo kwa kuwa kiti chako kitakuwa wazi. 19Kesho kutwa, inapokaribia jioni, nenda mahali pale ulipojificha wakati tatizo hili lilipoanza na usubiri karibu na jiwe la Ezeli. 20Nitapiga mishale mitatu kando yake, kana kwamba nilienda kulenga shabaha. 21Kisha nitamtuma mvulana na kumwambia, ‘Nenda ukaitafute mishale.’ Nikimwambia, ‘Tazama mishale iko upande huu wako! Uilete hapa,’ basi uje, kwa sababu hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, wewe ni salama, hakuna hatari. 22Lakini nikimwambia huyo mvulana, ‘Angalia, mishale iko mbele yako,’ basi inakupasa uondoke, kwa sababu Mwenyezi Mungu amekuruhusu uende zako. 23Kuhusu yale tuliyozungumza wewe na mimi: kumbuka, Mwenyezi Mungu ndiye shahidi kati yako wewe na mimi milele.”
24Basi Daudi akajificha shambani, na sikukuu ya Mwezi Mwandamo ilipowadia, mfalme akaketi ili ale. 25Akaketi mahali pake pa kawaida karibu na ukuta, kuelekeana na Yonathani, naye Abneri akaketi karibu na Mfalme Sauli, lakini kiti cha Daudi kilikuwa wazi. 26Sauli hakusema chochote siku ile kwa kuwa alifikiri, “Kuna kitu cha lazima kimetokea kwa Daudi ambacho kimemfanya najisi asihudhurie karamu; hakika yeye yu najisi.” 27Lakini siku iliyofuata, siku ya pili ya mwezi, kiti cha Daudi kilikuwa wazi tena. Kisha Sauli akamwambia mwanawe Yonathani, “Kwa nini mwana wa Yese hajaja chakulani jana wala leo?”
28Yonathani akamjibu, “Daudi alinisihi sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu. 29Alisema, ‘Niruhusu niende, kwa sababu jamaa yetu wana dhabihu mjini, na ndugu yangu ameniagiza niwepo huko. Kama nimepata kibali mbele yako, niruhusu niende kuona ndugu zangu.’ Hii ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme.”
30Hasira ya Sauli ikawaka dhidi ya Yonathani na kumwambia, “Wewe mwana wa mwanamke mkaidi na mwasi! Je, sijui kuwa umekuwa upande wa mwana wa Yese kwa aibu yako mwenyewe na kwa aibu ya mama yako aliyekuzaa? 31Maadamu mwana wa Yese angali anaishi katika dunia hii wewe wala ufalme wako hautasimama. Sasa tuma aitwe umlete kwangu, kwa kuwa ni lazima afe!”
32Yonathani akamuuliza baba yake, “Kwa nini auawe? Kwani amefanya nini?” 33Lakini Sauli akamtupia Yonathani mkuki wake kwa nguvu ili amuue. Hapo ndipo Yonathani alipotambua kwamba baba yake alikusudia kumuua Daudi.
34Yonathani akainuka kutoka mezani kwa hasira kali. Siku ile ya pili ya mwezi hakula chakula, kwa kuwa alikuwa amehuzunishwa na vitendo vya aibu ambavyo baba yake alikuwa anamtendea Daudi.
35Kesho yake asubuhi Yonathani alienda shambani kukutana na Daudi. Alikuwa amefuatana na mvulana mdogo, 36naye Yonathani akamwambia yule mvulana, “Kimbia ukatafute mishale nitakayorusha.” Mvulana alipokuwa akikimbia, akarusha mishale mbele yake. 37Yule mvulana alipofika mahali pale mshale wa Yonathani ulikuwa umeanguka, Yonathani akamwita, “Je, mshale hauko mbele yako?” 38Yonathani akampigia kelele, “Harakisha, nenda haraka! Usisimame!” Mvulana akaokota mshale na kurudi kwa bwana wake. 39(Mvulana hakujua chochote kuhusu hayo yote; Yonathani na Daudi tu ndio waliojua.) 40Basi Yonathani akampa yule mvulana silaha zake na kumwambia, “Nenda, zirudishe mjini.”
41Baada ya mvulana kwenda, Daudi akainuka kutoka upande wa kusini wa lile jiwe, naye akasujudu mara tatu mbele ya Yonathani. Kisha kila mmoja akambusu mwenzake, wakalia pamoja. Lakini Daudi akalia zaidi.
42Yonathani akamwambia Daudi, “Nenda kwa amani, kwa kuwa tumeapiana kiapo cha urafiki kati yetu kwa jina la Mwenyezi Mungu, tukisema, ‘Mwenyezi Mungu ndiye shahidi kati yako na mimi, na kati ya wazao wako na wazao wangu milele.’ ” Kisha Daudi akaondoka, naye Yonathani akarudi mjini.
Iliyochaguliwa sasa
1 Samweli 20: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.