1 Samweli 19
19
Sauli ajaribu kumuua Daudi
1Sauli akamwambia mwanawe Yonathani na watumishi wake wote wamuue Daudi. Lakini Yonathani mwana wa Sauli alimpenda sana Daudi. 2Yonathani akamwonya Daudi, akisema, “Baba yangu Sauli anatafuta nafasi ya kukuua. Ujilinde kesho asubuhi, nenda mahali pa siri na ukae huko. 3Nitatoka na kukaa na baba yangu shambani mahali uliko. Nitazungumza naye juu yako, nami nitakueleza nitakachogundua.”
4Yonathani akanena mema kuhusu Daudi kwa Sauli baba yake na kumwambia, “Mfalme asitende mabaya kwa mtumishi wake Daudi; hajakukosea, aliyoyafanya yamekuwa ya faida sana kwako. 5Alihatarisha maisha yake alipomuua yule Mfilisti. Mwenyezi Mungu akajipatia ushindi mkubwa kwa ajili ya Israeli wote, nawe uliuona na ukafurahi. Kwa nini basi utende mabaya kwa mtu asiye na hatia kama Daudi kwa kumuua bila sababu?”
6Sauli akamsikiliza Yonathani na kuapa hivi: “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, Daudi hatauawa.”
7Basi Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mazungumzo yote. Akamleta kwa Sauli, naye Daudi akawa pamoja na Sauli kama kwanza.
8Vita vilitokea tena, naye Daudi akatoka na kupigana na Wafilisti. Akawapiga kwa nguvu nyingi hata wakakimbia mbele yake.
9Lakini roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu ikaja juu ya Sauli alipokuwa ameketi katika nyumba yake akiwa na mkuki mkononi mwake. Daudi alipokuwa anampigia kinubi, 10Sauli akajaribu kumchomea Daudi ukutani kwa huo mkuki wake, lakini Daudi akauhepa huo mkuki wa Sauli ukakita ukutani. Usiku ule ule Daudi akakimbia na kuokoka.
11Sauli akatuma watu nyumbani mwa Daudi wailinde hiyo nyumba na kumuua asubuhi. Lakini Mikali, mkewe Daudi, akamwonya akisema, “Usipokimbia kuokoa maisha yako usiku huu, kesho utauawa.” 12Basi Mikali akamteremsha Daudi kupitia dirishani, naye akakimbia na kuokoka. 13Kisha Mikali akachukua kinyago, akakilaza kitandani, akakifunika kwa vazi na kukiwekea singa za mbuzi kichwani.
14Sauli alipotuma watu kumkamata Daudi, Mikali akasema, “Yeye ni mgonjwa.”
15Kisha Sauli akatuma watu tena kumwona Daudi naye akawaambia, “Mleteni kwangu juu ya kitanda chake ili nipate kumuua.” 16Lakini wale watu walipoingia, kumbe ni kinyago tu kilichokuwa kitandani, na kwenye kichwa kulikuwa na singa za mbuzi.
17Sauli akamwambia Mikali, “Kwa nini umenidanganya mimi hivi na kumwacha adui yangu aende zake ili apate kuokoka?”
Mikali akamwambia, “Yeye aliniambia, ‘Niache niende zangu. Kwa nini nikuue?’ ”
18Daudi alipokuwa amekimbia na kuokoka, alimwendea Samweli huko Rama na kumwambia yale yote Sauli alimfanyia. Ndipo Daudi na Samweli wakaenda Nayothi kukaa huko. 19Habari zikamfikia Sauli kusema: “Daudi yuko Nayothi huko Rama.” 20Basi Sauli akatuma watu kumkamata Daudi, lakini walipoona kundi la manabii wakitoa unabii, wakiwa pamoja na Samweli akiwa amesimama hapo kama kiongozi wao, Roho wa Mungu akaja juu ya watu wa Sauli, nao pia wakatoa unabii. 21Sauli akaelezwa hilo, naye akapeleka watu wengine zaidi, nao wakatoa unabii pia. Sauli akatuma watu mara ya tatu, nao pia wakatoa unabii. 22Mwishowe, yeye mwenyewe akaondoka kwenda Rama na kwenda hadi kwenye kile kisima kikubwa kilichoko huko Seku. Naye akauliza, “Wako wapi Samweli na Daudi?”
Wakasema, “Wako Nayothi huko Rama.”
23Hivyo Sauli akaenda Nayothi huko Rama. Lakini Roho wa Mungu akaja juu yake hata yeye, akawa anatembea huku anatoa unabii hadi akafika Nayothi. 24Akavua majoho yake na pia akatoa unabii mbele ya Samweli. Akalala hali hiyo ule mchana kutwa na usiku kucha. Hii ndiyo sababu watu husema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?”
Iliyochaguliwa sasa
1 Samweli 19: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.