1 Wafalme 4:21-28
1 Wafalme 4:21-28 NENO
Mfalme Sulemani akatawala katika falme zote kuanzia Mto hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Sulemani, siku zote za maisha yake. Mahitaji ya Sulemani ya kila siku yalikuwa kori thelathini za unga laini, kori sitini za unga wa kawaida. Ngʼombe kumi wa zizini, ngʼombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana. Kwa kuwa Sulemani alitawala falme zote magharibi ya Mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote. Wakati wa maisha ya Sulemani, watu wa Yuda na Israeli, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, waliishi salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake. Sulemani alikuwa na mabanda elfu nne ya magari ya vita, na farasi elfu kumi na mbili. Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Sulemani na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna chochote kilichopungua. Pia walileta kiasi walichopangiwa cha shayiri na majani kwa ajili ya farasi wa magari ya vita na farasi wengine mahali palipostahili.