1 Wafalme 4:21-28
1 Wafalme 4:21-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Solomoni alitawala falme zote kuanzia mto Eufrate mpaka nchi ya Wafilisti, hadi mpakani na Misri. Mataifa yote yalimtumikia na kulipa kodi kwake wakati wote wa maisha yake. Chakula alichohitaji Solomoni kwa siku moja, kilikuwa unga laini madebe 360, na unga wa kawaida madebe 720, ng'ombe wanono kumi, na ng'ombe wa kundini ishirini, kondoo 100 pamoja na kulungu, paa, swala na kuku wanono. Naam, nchi yote magharibi ya mto Eufrate: Kutoka Tifsa mpaka mji wa Gaza, ilikuwa chini ya utawala wake. Wafalme wote magharibi ya mto Eufrate walikuwa chini yake, na alikuwa na amani na nchi zote jirani. Siku zote za utawala wake Solomoni, watu wa Yuda na watu wa Israeli, toka Dani mpaka Beer-sheba, walikaa salama, kila mtu kwenye miti yake ya mizabibu na mitini. Solomoni alikuwa na vibanda 40,000 kwa ajili ya farasi wa magari yake ya kukokotwa, na askari wapandafarasi 12,000. Wale maofisa wake kumi na wawili, kila mmoja kwa mwezi aliopangiwa, walipeleka chakula cha kutosha kwa ajili ya mfalme na wale wote waliokula nyumbani mwake. Mahitaji yao yote yalitoshelezwa. Zamu ya kila mmoja ilipofika, alipeleka pia shayiri na majani ya kulisha farasi na wanyama waendao kasi.
1 Wafalme 4:21-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Sulemani akatawala juu ya falme zote, toka Mto mpaka nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri; walimletea tunu, na kumtumikia Sulemani siku zote za maisha yake. Na vyakula vya Sulemani vya siku moja vilikuwa kori thelathini za unga mzuri, na kori sitini za ngano, na ng'ombe kumi walionona, na ng'ombe ishirini za malisho, na kondoo mia moja, pamoja na ayala, na paa, na kulungu, na kuku walionona. Kwani alikuwa akitawala nchi yote upande huu wa Mto, toka Tifsa mpaka Gaza, juu ya wafalme wote wa upande huu wa Mto; naye alikuwa na amani pande zake zote. Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, tokea Dani mpaka Beer-sheba, siku zote za Sulemani. Tena Sulemani alikuwa na mabanda ya farasi elfu arubaini kwa magari yake, na wapandao farasi elfu kumi na mbili. Na maofisa wale wakaleta chakula kwa mfalme Sulemani na kwa wote walioijia meza ya mfalme Sulemani, kila mtu katika mwezi wake, kisipunguke kitu. Shayiri pia na majani kwa farasi, na kwa wanyama wenye mbio, wakaleta mahali walipokuwapo, kila mtu kwa kadiri ya kazi yake.
1 Wafalme 4:21-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Sulemani akatawala juu ya falme zote, toka Mto mpaka nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri; walimletea tunu, na kumtumikia Sulemani siku zote za maisha yake. Na vyakula vya Sulemani vya siku moja vilikuwa kori thelathini za unga mzuri, na kori sitini za ngano, na ng’ombe kumi walionona, na ng’ombe ishirini za malisho, na kondoo mia, pamoja na ayala, na paa, na kulungu, na kuku walionona. Kwani alikuwa akitawala nchi yote upande huu wa Mto, toka Tifsa mpaka Gaza, juu ya wafalme wote wa upande huu wa Mto; naye alikuwa na amani pande zake zote. Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, tokea Dani mpaka Beer-sheba, siku zote za Sulemani. Tena Sulemani alikuwa na mabanda ya farasi arobaini elfu kwa magari yake, na wapandao farasi kumi na mbili elfu. Na maakida wale wakaleta chakula kwa mfalme Sulemani na kwa wote walioijia meza ya mfalme Sulemani, kila mtu katika mwezi wake, kisipunguke kitu. Shayiri pia na majani kwa farasi, na kwa wanyama wenye mbio, wakaleta mahali walipokuwapo, kila mtu kwa kadiri ya kazi yake.
1 Wafalme 4:21-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mfalme Solomoni akatawala katika falme zote kuanzia Mto Frati hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Solomoni, siku zote za maisha yake. Mahitaji ya Solomoni ya kila siku yalikuwa kori thelathini za unga laini, kori sitini za unga wa kawaida. Ngʼombe kumi wa zizini, ngʼombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana. Kwa kuwa Solomoni alitawala falme zote magharibi ya mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote. Wakati wa maisha ya Solomoni Yuda na Israeli, kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba, wakaishi salama kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake. Solomoni alikuwa na mabanda 4,000 ya magari ya vita, na farasi 12,000. Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Solomoni na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna chochote kilichopungua. Pia walileta sehemu walizopangiwa za shayiri na majani kwa ajili ya farasi wavutao magari na farasi wengine mahali palipostahili.