1 Wafalme 4:21-28
1 Wafalme 4:21-28 NEN
Mfalme Solomoni akatawala katika falme zote kuanzia Mto Frati hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Solomoni, siku zote za maisha yake. Mahitaji ya Solomoni ya kila siku yalikuwa kori thelathini za unga laini, kori sitini za unga wa kawaida. Ngʼombe kumi wa zizini, ngʼombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana. Kwa kuwa Solomoni alitawala falme zote magharibi ya mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote. Wakati wa maisha ya Solomoni Yuda na Israeli, kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba, wakaishi salama kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake. Solomoni alikuwa na mabanda 4,000 ya magari ya vita, na farasi 12,000. Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Solomoni na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna chochote kilichopungua. Pia walileta sehemu walizopangiwa za shayiri na majani kwa ajili ya farasi wavutao magari na farasi wengine mahali palipostahili.