1 Wakorintho 1:9-30
1 Wakorintho 1:9-30 NENO
Mungu ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Isa Al-Masihi, Bwana wetu ni mwaminifu. Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano kati yenu, na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi. Ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi kati yenu. Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa”; na mwingine, “Mimi ni wa Al-Masihi.” Je, Al-Masihi amegawanyika? Je, Paulo ndiye alisulubishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? Nashukuru kwamba sikumbatiza mtu yeyote isipokuwa Krispo na Gayo. Kwa hiyo hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kwamba alibatizwa kwa jina langu. (Naam, niliwabatiza pia watu wa nyumbani mwa Stefana; lakini zaidi ya hao sijui kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote.) Kwa maana Al-Masihi hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili; sio kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili msalaba wa Al-Masihi usije ukakosa nguvu yake. Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa maana imeandikwa: “Nitaiharibu hekima ya wenye hekima, na kubatilisha akili ya wenye akili.” Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? Kwa kuwa katika hekima ya Mungu ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. Lakini sisi tunamhubiri Al-Masihi aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Al-Masihi ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu. Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika vyeo. Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima; Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Al-Masihi Isa, aliyefanyika kwetu hekima inayotoka kwa Mungu, yaani haki yetu, na utakatifu na ukombozi.