Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 1:9-30

1 Wakorintho 1:9-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita nyinyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu. Ndugu, nawasihini kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo: Pataneni nyote katika kila jambo msemalo; yasiweko mafarakano kati yenu; muwe na fikira moja na nia moja. Ndugu zangu, habari nilizopata kutoka kwa watu kadhaa wa jamaa ya Kloe, zaonesha wazi kwamba kuna kutoelewana kati yenu. Nataka kusema hivi: Kila mmoja anasema chake: Mmoja husema, “Mimi ni wa Paulo”, mwingine: “Mimi ni wa Apolo”, mwingine: “Mimi ni wa Kefa,” na mwingine: “Mimi ni wa Kristo.” Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? Namshukuru Mungu kwamba sikumbatiza mtu yeyote miongoni mwenu isipokuwa tu Krispo na Gayo. Kwa hiyo hakuna awezaye kusema amebatizwa kwa jina langu. ( Samahani, nilibatiza pia jamaa ya Stefana; lakini zaidi ya hawa, sidhani kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote). Kristo hakunituma kubatiza, bali kuhubiri Habari Njema; tena, niihubiri bila kutegemea maarifa ya hotuba za watu, kusudi nguvu ya kifo cha Kristo msalabani isibatilishwe. Maana ujumbe kuhusu kifo cha Kristo msalabani ni jambo la kipumbavu kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea, lakini kwetu sisi tulio katika njia ya wokovu, ujumbe huo ni nguvu ya Mungu. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, na elimu ya wataalamu nitaitupilia mbali.” Yu wapi basi, mwenye hekima? Yu wapi basi, mwalimu wa sheria? Naye bingwa wa mabishano wa nyakati hizi yuko wapi? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upumbavu. Maana, kadiri ya hekima ya Mungu, watu hawawezi kumjua Mungu kwa njia ya hekima yao wenyewe. Badala yake, Mungu amependa kuwaokoa wale wanaoamini kwa njia ya kile ambacho wenye hekima wanakiona kuwa ni upumbavu, yaani ujumbe tunaohubiri. Wayahudi wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima; lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa. Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa watu wa mataifa ni upumbavu; lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu. Ndugu, kumbukeni wakati mlipoitwa: Wengi wenu hawakuwa wenye hekima hata kwa fikira za binadamu; wengi hawakuwa wenye nguvu au watu wa tabaka la juu. Ndiyo kusema, Mungu aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni upumbavu, ili awaaibishe wenye hekima; na aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni dhaifu, ili awaaibishe wenye nguvu. Mungu ameyachagua yale ambayo kwa fikira za dunia ni mambo yaliyo duni na yanayodharauliwa, mambo ambayo hata hayakuwako, ili kwa hayo ayafutilie mbali yale ambayo kwa fikira za binadamu ni mambo ya maana. Basi, hakuna mtu awezaye kujivunia chochote mbele ya Mungu. Mungu mwenyewe ndiye aliyewaunganisha nyinyi na Kristo Yesu. Mungu amemfanya Kristo awe hekima yetu; kwa njia yake sisi tunapatanishwa na Mungu, tunakuwa watu wake Mungu na kukombolewa.

1 Wakorintho 1:9-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu. Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu migawanyiko, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba uko ugomvi kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulubiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo? Nashukuru, kwa sababu sikumbatiza mtu kwenu, ila Krispo na Gayo; mtu asije akasema kwamba mlibatizwa kwa jina langu. Tena niliwabatiza watu wa nyumbani mwa Stefana; zaidi ya hao, sijui kama nilimbatiza mtu yeyote mwingine. Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa. Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi mwandishi? Yuko wapi mleta hoja wa nyakati hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu? Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa. Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulubiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wagiriki ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wagiriki, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu. Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi

1 Wakorintho 1:9-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu. Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo? Nashukuru, kwa sababu sikumbatiza mtu kwenu, ila Krispo na Gayo; mtu asije akasema kwamba mlibatizwa kwa jina langu. Tena naliwabatiza watu wa nyumbani mwa Stefana; zaidi ya hao, sijui kama nalimbatiza mtu ye yote mwingine. Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa. Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu? Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa. Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu. Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi

1 Wakorintho 1:9-30 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Mungu ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Isa Al-Masihi, Bwana wetu ni mwaminifu. Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano kati yenu, na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi. Ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi kati yenu. Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa”; na mwingine, “Mimi ni wa Al-Masihi.” Je, Al-Masihi amegawanyika? Je, Paulo ndiye alisulubishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? Nashukuru kwamba sikumbatiza mtu yeyote isipokuwa Krispo na Gayo. Kwa hiyo hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kwamba alibatizwa kwa jina langu. (Naam, niliwabatiza pia watu wa nyumbani mwa Stefana; lakini zaidi ya hao sijui kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote.) Kwa maana Al-Masihi hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili; sio kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili msalaba wa Al-Masihi usije ukakosa nguvu yake. Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa maana imeandikwa: “Nitaiharibu hekima ya wenye hekima, na kubatilisha akili ya wenye akili.” Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? Kwa kuwa katika hekima ya Mungu ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. Lakini sisi tunamhubiri Al-Masihi aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Al-Masihi ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu. Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika vyeo. Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima; Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Al-Masihi Isa, aliyefanyika kwetu hekima inayotoka kwa Mungu, yaani haki yetu, na utakatifu na ukombozi.

1 Wakorintho 1:9-30

1 Wakorintho 1:9-30 BHN1 Wakorintho 1:9-30 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima