Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nyakati 19

19
Vita dhidi ya Waamoni
(2 Samweli 10:1-19)
1Baada ya muda, Nahashi mfalme wa Waamoni akafa, na mwanawe akawa mfalme baada yake. 2Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kwa sababu baba yake alinitendea wema.”
Hivyo Daudi akatuma wajumbe ili kumfariji Hanuni kwa ajili ya kifo cha baba yake. Watu wa Daudi walipofika kwa Hanuni katika nchi ya Waamoni ili kumfariji, 3wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni, “Hivi unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kuwatuma wajumbe kukufariji? Je, hawa watu hawakuja kuipeleleza na kuidadisi nchi ili waishinde?” 4Kwa hiyo Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa ndevu, akakata nguo zao katikati kwenye matako, akawaachia waende zao.
5Mtu mmoja alipofika na kumpasha Daudi habari za watu hawa, akawatuma wajumbe wengine kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko hadi ndevu zenu ziote, ndipo mje.”
6Waamoni walipotambua kwamba wamekuwa machukizo kwa Daudi, basi Hanuni na Waamoni wakatuma talanta elfu moja#19:6 Talanta 1,000 ni sawa na tani 34. za fedha ili kukodisha magari ya vita, pamoja na waendeshaji wa hayo magari ya kukokotwa na farasi, kutoka Mesopotamia, Aram-Maaka na Soba. 7Wakakodisha magari ya vita elfu thelathini na mbili na waendeshaji wake, pamoja na mfalme wa Maaka na vikosi vyake. Wakapiga kambi karibu na Medeba. Waamoni nao wakakusanyika toka miji yao, wakatoka ili kupigana vita.
8Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji. 9Waamoni wakatoka, wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati wale wafalme wengine waliokuja nao walijipanga kwa vita uwanjani.
10Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli, akavipanga dhidi ya Waaramu. 11Akawaweka wale wanajeshi wengine waliobaki chini ya amri ya Abishai ndugu yake, nao wakapangwa ili wakabiliane na Waamoni. 12Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itakupasa wewe uniokoe; lakini kama Waamoni watakuzidi nguvu, basi mimi nitakuokoa. 13Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Mwenyezi Mungu atafanya lile lililo jema machoni pake.”
14Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake. 15Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao pia wakakimbia mbele ya nduguye Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi Yerusalemu.
16Baada ya Waaramu kuona kwamba wameshindwa na Israeli, wakapeleka wajumbe na kuwataka Waaramu wengine kutoka ng’ambo ya Mto#19:16 yaani Mto Frati, wakiongozwa na Shofaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri.
17Daudi alipoambiwa haya, akawakusanya Israeli wote na kuvuka Yordani. Akasonga mbele dhidi yao na akajipanga kuwakabili. Daudi akapanga vita ili kupigana na Waaramu, nao wakapigana dhidi yake. 18Lakini Waaramu wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akawaua waendesha magari ya vita elfu saba, na askari wa miguu elfu arobaini. Pia akamuua Shofaki, jemadari wa jeshi lao.
19Raia wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya mapatano ya amani na Daudi, wakawa watumishi wake.
Hivyo Waaramu hawakukubali kuwasaidia Waamoni tena.

Iliyochaguliwa sasa

1 Nyakati 19: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia