Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nyakati 18

18
Ushindi wa Daudi
(2 Samweli 8:1-18)
1Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akatwaa Gathi pamoja na vijiji vinavyouzunguka kutoka utawala wa Wafilisti.
2Pia Daudi akawashinda Wamoabu, wakawa watumishi wake, nao wakawa wanamletea ushuru.
3Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mfalme wa Soba, hadi Hamathi, wakati alienda kuimarisha utawala wake katika Mto Frati. 4Daudi akateka magari ya vita elfu moja miongoni mwa magari yake, waendesha hayo magari ya vita elfu saba, na askari wa miguu elfu ishirini. Daudi akakata mishipa ya miguu ya farasi wa magari ya vita, akabakiza farasi mia moja.
5Waaramu wa Dameski, walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua watu elfu ishirini na mbili miongoni mwao. 6Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski. Basi Waaramu wakawa watumwa wa Daudi, na kumlipa ushuru. Mwenyezi Mungu akampa Daudi ushindi kote alipoenda.
7Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu. 8Kutoka miji ya Tibathi na Kuni, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi sana, ambayo Sulemani aliitumia kutengenezea ile Bahari ya shaba, zile nguzo na vifaa mbalimbali vya shaba.
9Tou mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba, 10akamtuma mwanawe Hadoramu kwa Mfalme Daudi, ili kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Mfalme Hadadezeri, kwa maana alikuwa amepigana vita mara nyingi na Tou. Hadoramu akamletea Daudi vifaa mbalimbali vya dhahabu, fedha na shaba.
11Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu aliyokuwa ameitwaa katika mataifa haya yote: Edomu na Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki.
12Abishai mwana wa Seruya akawaua Waedomu elfu kumi na nane katika Bonde la Chumvi. 13Akaweka kambi za askari walinzi huko Edomu, nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Daudi. Mwenyezi Mungu akampa Daudi ushindi kila alipoenda.
Maafisa wa Daudi
14Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote.
15Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi;
Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu;
16Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani;
Shausha alikuwa mwandishi;
17naye Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi;
nao wana wa Daudi walikuwa maafisa wakuu katika utumishi wa mfalme.

Iliyochaguliwa sasa

1 Nyakati 18: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia