1 Nyakati 16:4-22
1 Nyakati 16:4-22 NENO
Akawaweka pia baadhi ya Walawi ili wahudumu mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu kufanya maombi, kumshukuru na kumsifu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Asafu ndiye alikuwa mkuu wao, akisaidiwa na Zekaria, Yeieli, Shemiramothi, Yehieli, Matithia, Eliabu, Benaya, Obed-Edomu na Yeieli. Hawa ndio wangepiga zeze na vinubi, Asafu angepiga matoazi, nao Benaya na Yahazieli makuhani, ndio wangepiga tarumbeta mara kwa mara mbele ya Sanduku la Agano la Mungu. Siku ile, kitu cha kwanza Daudi alichofanya ni kumkabidhi Asafu na wenzake zaburi hii ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu: Mshukuruni Mwenyezi Mungu, liitieni jina lake; wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda. Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa; waambieni matendo yake yote ya ajabu. Lishangilieni jina lake takatifu; mioyo ya wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu na ifurahi. Mtafuteni Mwenyezi Mungu na nguvu zake; utafuteni uso wake siku zote. Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka, enyi wazao wa Israeli mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mungu wetu; hukumu zake ziko duniani kote. Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu, agano alilolifanya na Ibrahimu, kiapo alichomwapia Isaka. Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele: “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.” Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake, walitangatanga kutoka taifa moja hadi lingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine. Hakuruhusu mtu yeyote awadhulumu; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema: “Msiwaguse niliowapaka mafuta; msiwadhuru manabii wangu.”