1 Nyakati 10
10
Sauli ajiua
(1 Samweli 31:1-13)
1Basi Wafilisti wakapigana na Israeli. Waisraeli wakawakimbia, na wengi wakauawa katika mlima Gilboa. 2Wafilisti wakawafuatilia Sauli na wanawe kwa karibu, na wakawaua Yonathani, Abinadabu, na Malki-Shua. 3Mapigano yakawa makali kumzunguka Sauli na wakati wapiga mishale walipompata, wakamjeruhi.
4Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa watu wasiotahiriwa watakuja na kunidhalilisha.”
Lakini mbeba silaha wake akaogopa sana wala hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo Sauli akachukua upanga wake mwenyewe na kuuangukia. 5Mbeba silaha wake alipoona kwamba Sauli amekufa, naye pia akauangukia upanga wake akafa. 6Kwa hiyo Sauli na wanawe watatu wakafa, pamoja na nyumba yake yote.
7Waisraeli wote waliokuwa bondeni walipoona kwamba jeshi limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, waliacha miji yao wakakimbia. Nao Wafilisti wakaenda na kuyamiliki.
8Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, walimkuta Sauli na wanawe wameanguka katika Mlima Gilboa. 9Wakamvua mavazi, wakachukua kichwa chake pamoja na silaha zake, wakawatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari hizi miongoni mwa sanamu zao na watu wao. 10Waliweka silaha zake katika hekalu la miungu yao, na wakatundika kichwa chake katika hekalu la Dagoni.
11Wakazi wote wa Yabesh-Gileadi waliposikia yale Wafilisti waliyomtendea Sauli, 12mashujaa wao wote wakaondoka, wakautwaa mwili wa Sauli na miili ya wanawe, wakaileta Yabeshi. Wakaizika mifupa yao chini ya mwaloni ulio Yabeshi, nao wakafunga kwa siku saba.
13Sauli alikufa kwa sababu hakuwa mwaminifu kwa Mwenyezi Mungu. Hakulishika neno la Mwenyezi Mungu, hata akataka shauri kwa mwaguzi kwa ajili ya uongozi, 14hakumuuliza Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu alimuua, na ufalme akampa Daudi mwana wa Yese.
Iliyochaguliwa sasa
1 Nyakati 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.