Mwanzo 8
8
Mwisho wa gharika
1Mungu akamkumbuka Nuhu na wanyama pori na mifugo wote waliokuwa naye ndani ya safina; akatuma upepo ukavuma katika dunia, nayo maji yakapungua. 2Chemchemi za vilindi zikawa zimefungwa, na malango ya mafuriko ya mbinguni pia yakawa yamefungwa; nayo mvua ikawa imekoma kunyesha. 3Maji yakaendelea kupungua taratibu katika dunia. Mwishoni mwa siku ya mia moja na hamsini, maji yakawa yamepungua. 4Na katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua katika milima ya Ararati. 5Maji yakaendelea kupungua hadi mwezi wa kumi. Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana.
6Baada ya siku arobaini, Nuhu akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina, 7akamtoa kunguru, naye akawa akiruka kwenda na kurudi hadi maji yalipokwisha kukauka juu ya dunia. 8Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya ardhi. 9Lakini hua hakupata mahali pa kutua, kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Nuhu ndani ya safina. Nuhu akanyoosha mkono akamchukua yule hua, akamrudisha ndani ya safina. 10Nuhu akangojea siku saba zaidi, kisha akamtoa tena hua kutoka safina. 11Jioni hua aliporudi kwa Nuhu alikuwa amebeba jani bichi la mzeituni lililochumwa wakati ule ule katika mdomo wake! Ndipo Nuhu akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya dunia. 12Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Nuhu.
13Kufikia siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa mia sita na moja (601) wa maisha ya Nuhu, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Nuhu akatoa kifuniko juu ya safina, akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka. 14Kufikia siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili, dunia ilikuwa imekauka kabisa.
15Ndipo Mungu akamwambia Nuhu, 16“Toka katika safina, wewe na mkeo, na wanao na wake zao. 17Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe, wakiwamo ndege, wanyama na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.”
18Kwa hiyo Nuhu akatoka nje pamoja na mkewe, na wanawe na wake zao. 19Wanyama wote na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini, na ndege wote, kila kitu kinachoenda juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina.
Nuhu atoa dhabihu
20Kisha Nuhu akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu, akachukua baadhi ya wale wanyama na ndege wote walio safi, akatoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. 21Mwenyezi Mungu akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya.
22“Kwa muda dunia idumupo,
majira ya kupanda na ya kuvuna,
wakati wa baridi na wa joto,
wakati wa kiangazi na wa masika,
usiku na mchana
kamwe havitakoma.”
अहिले सेलेक्ट गरिएको:
Mwanzo 8: NENO
हाइलाइट
शेयर गर्नुहोस्
कपी गर्नुहोस्
तपाईंका हाइलाइटहरू तपाईंका सबै यन्त्रहरूमा सुरक्षित गर्न चाहनुहुन्छ? साइन अप वा साइन इन गर्नुहोस्
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.