1 Mose 1
1
Kuuumba ulimwengu.
(Taz. Sh. 104.)
1Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.#Yoh. 1:1-3; Tume. 17:24; Ebr. 11:3; Ufu. 4:11. 2Nayo nchi ilikuwa peke yake pasipo kitu, nalo giza lilivifunika vilindi, nayo Roho Ya Mungu ilikuwa imejitanda juu ya maji. 3Mungu akasema: Na uwe mwanga! Ndipo, mwanga ulipokuwa.#Sh. 33:9; 2 Kor. 4:6. 4Mungu akauona mwanga kuwa mwema, kisha Mungu akatenganisha mwanga na giza; 5mwanga Mungu akauita mchana, nalo giza akaliita usiku. Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya kwanza.
6Mungu akasema: Na uwe utando katikati ya maji, uyatenganishe maji na maji! 7Mungu akaufanya utando, akayatenga maji yaliyoko chini ya utando nayo maji yaliyoko juu ya utando; yakawa hivyo.#Sh. 19:2. 8Utando Mungu akauita mbingu. Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya pili.
9Mungu akasema: Maji yaliyoko chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, pakavu paonekane! Yakawa hivyo.#2 Petr. 3:5; Iy. 38:8-11. 10Mungu akapaita pakavu nchi, nalo kusanyiko la maji akaliita bahari. Mungu akayaona kuwa mema. 11Kisha Mungu akasema: Nchi na ichipuze machipuko: mboga ziletazo mbegu na miti ya matunda iletayo matunda, kila mmmoja kwa namna yake, nayo yawe yenye mbegu zao ndani yao za kupandwa katika nchi. Yakawa hivyo. 12Ndipo, nchi ilipotoa machipuko: mboga ziletazo mbegu kwa namna zao na miti iletayo matunda, kila mmoja kwa namna yake, nayo yalikuwa yenye mbegu zao ndani yao, Mungu akayaona kuwa mema. 13Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya tatu.
14Mungu akasema: Na iwe mianga penye utando wa mbingu ya kuutenga mchana na usiku, iwe vielekezo vya kujulisha sikukuu na siku nyingine na miaka;#Sh. 74:16. 15nayo iwe mianga utandoni kwa mbingu ya kuiangaza nchi! Yakawa hivyo. 16Mungu akaifanya mianga miwili iliyo mikubwa: mwanga mkubwa wa kuutawala mchana nao mwanga mdogo wa kuutawala usiku pamoja na nyota.#Sh. 136:7-9. 17Mungu akaiweka utandoni kwa mbingu, ipate kingaza nchi 18na kuutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akayaona kuwa mema. 19Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya nne.
20Mungu akasema: Maji na yajae viumbe vya kuwa humo vyenye uzima, hata ndege na waruke juu ya nchi chini ya utando wa mbingu! 21Mungu akawaumba nyangumi wakubwa na viumbe vyote wanaokaa majini na kutembea humo, kila mmoja kwa namna yake, nao ndege wote warukao kwa mabawa, kila mmoja kwa namna yake. 22Mungu akawabariki kwamba: Zaeni, mwe wengi, mjae majini baharini, nao ndege na mawe wengi katika nchi! 23Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya tano.
24Mungu akasema: Nchi na itoe viumbe vyenye uzima vya kila namna, nyama wa nyumbani na wadudu na nyama wa porini wa kila namna! Yakawa hivyo. 25Mungu akawafanya nyama wa porini kila mmoja kwa namna yake na wadudu wote wa nchi kila mmoja kwa namna yake. Mungu akayaona kuwa mema. 26Kisha Mungu akasema: na tufanye mtu kwa mfano wetu, afanane na sisi, awatawale samaki wa baharini na ndege wa angani na nyama na nchi yote nzima na wadudu wote watambaao katika nchi!#Sh. 8:6-9. 27Mungu akamwumba mtu kwa mfano wake, mfano wake Mungu ndio, aliomwumbia, akamwumba kuwa mume na mke.#Mat. 19:4; Ef. 4:24; 1 Mose 2:7,22. 28Mungu akawabariki, Mungu akawaambia: Zaeni wana, mwe wengi, mwijaze nchi, kisha mwitiishe! Watawaleni samaki wa baharini na ndege wa angani na nyama wote pia watambaao katika nchi!#Tume. 17:2,6. 29Kisha Mungu akasema: Tazameni, nimewapa ninyi mboga zote zenye mbegu zilizoota katika nchi na miti yote izaayo matunda yenye mbegu ndani yao kuwa chakula chenu ninyi! 30Nao nyama wote wa nchi na ndege wote wa angani nao wote watambaao katika nchi walio viumbe vyenye uzima, nao chakula chao ni majani yote yanayolika. Yakawa hivyo. 31Mungu alipoyatazama yote, aliyoyafanya, akayaona kuwa mema sana. Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya sita.
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.