Mathayo 16
16
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mk 8:11-13; Lk 12:54-56)
1Mafarisayo na Masadukayo walimjia Yesu. Walitaka kumjaribu, kwa hiyo wakamwomba awaoneshe muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu.
2Yesu akawajibu, “Ninyi watu mnapoona jua limezama, mnajua hali ya hewa itakavyokuwa. Anga ikiwa nyekundu, mnasema tutakuwa na hali ya hewa nzuri. 3Na asubuhi, ikiwa anga ni nyeusi na nyekundu, mnasema mvua itanyesha. Hizi ni ishara za hali ya hewa. Mnaziona ishara hizi angani na mnajua zinamaanisha nini. Kwa namna hiyo hiyo, mnaona mambo yanayotokea sasa. Hizi ni ishara pia, lakini hamwelewi maana yake. 4Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu na si waaminifu kwa Mungu. Ndiyo sababu kabla ya kuamini mnataka kuona muujiza. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia kitu cho chote. Yona#16:4 Yona Au “Nabii Yona”, nabii katika Agano la Kale. Baada ya kukaa katika tumbo la samaki mkubwa kwa siku tatu alitoka akiwa mzima, kisha akaenda kwenye mji uliojaa uovu wa Ninawi kuwaonya watu huko kama alivyotumwa na Mungu. Kwa njia hiyo hiyo, Yesu angetoka kaburini siku ya tatu, ishara ya kuthibitisha ukweli wa ujumbe wake kutoka kwa Mungu. ndiyo ishara pekee mtakayopewa.” Kisha Yesu akaondoka mahali pale.
Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu
(Mk 8:14-21)
5Yesu na wafuasi wake wakasafiri kwa kukatisha ziwa. Lakini wafuasi wakasahau kubeba mikate. 6Yesu akawaambia, “Muwe waangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
7Wafuasi wakajadiliana maana ya hili. Wakasema, “Amesema hivi kwa sababu tumesahau kubeba mikate?”
8Yesu alipotambua kuwa wanajadiliana hili, akawauliza, “Kwa nini mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Imani yenu ni ndogo. 9Bado hamwelewi? Mnakumbuka mikate mitano waliyokula watu 5,000 na vikapu vingi mlivyojaza mikate iliyosalia? 10Na mnakumbuka mikate saba waliyokula watu 4,000 na vikapu vingi mlivyojaza wakati ule? 11Hivyo inakuwaje mnadhani kuwa mimi ninajali sana kuhusu mikate? Ninawaambia muwe waangalifu na mjilinde dhidi ya chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
12Ndipo wafuasi wakaelewa Yesu alimaanisha nini. Hakuwa akiwaambia wajilinde na chachu inayotumika katika mikate bali wajilinde na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Petro Atambua Yesu ni Nani
(Mk 8:27-30; Lk 9:18-21)
13Yesu alikwenda eneo la Kaisaria Filipi na akawauliza wafuasi wake, “Watu wanasema mimi ni nani#16:13 mimi ni nani Kwa maana ya kawaida, “Mwana wa Adamu ni”.?”
14Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji. Wengine wanasema wewe ni Eliya. Na wengine wanasema wewe ni Yeremia au mmoja wa manabii.”
15Kisha Yesu akawauliza, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?”
16Simoni Petro akajibu, “Wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu aliye hai.”
17Yesu akajibu, “Umebarikiwa, Simoni mwana wa Yona. Hakuna aliyekufundisha hilo ila Baba yangu wa mbinguni ndiye amekuonesha mimi ni nani. 18Hivyo ninakwambia, Wewe ni Petro. Na nitalijenga kanisa langu kwenye mwamba#16:18 Petro … mwamba “Petro”, ni jina la Kiyunani (Kigiriki) ambalo kwa Kiaramu ni “Kefa” likimaanisha “mwamba”. Katika Maandiko (Isa 51:1,2), pamoja na desturi za Kiyahudi, Abrahamu alilinganishwa na mwamba ambao Mungu angeutumia “kujengea” watu wake. Hivyo Yesu anaweza kulinganisha kuwa Yesu ni kama Abrahamu. Mungu aliwapa majina mapya Abrahamu na Sara na aliwaheshimu kama mifano ya imani kwa wazaliwa wao. Katika namna hiyo hiyo, Yesu alimpa jina jingine Petro (tazama Mk 3:16) na akamheshimu hapa kwa ujasiri wake wa imani. huu. Nguvu ya mauti#16:18 Nguvu ya mauti Kwa maana ya kawaida, “malango ya Kuzimu”. haitaweza kulishinda kanisa langu. 19Nitawapa funguo za Ufalme wa Mungu. Mnapohukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Mnapotamka msamaha hapa duniani, msamaha huo utakuwa msamaha wa Mungu.”#16:19 Mnapotamka msamaha … msamaha wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “Kila mtakachofunga hapa duniani kitafungwa mbinguni, na mtakachokifungua hapa duniani kitafunguliwa mbinguni.”
20Kisha Yesu akawaonya wafuasi wake wasimwambie mtu yeyote kuwa yeye ndiye Masihi.
Yesu Asema ni Lazima Afe
(Mk 8:31–9:1; Lk 9:22-27)
21Kuanzia wakati huo Yesu alianza kuwaambia wafuasi wake kuwa ni lazima aende Yerusalemu. Alifafanua kuwa Viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria watamfanya apate mateso kwa mambo mengi. Na aliwaambia wafuasi wake kuwa lazima auawe. Na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu.
22Petro akamchukua Yesu na kwenda naye faragha mbali na wafuasi wengine. Akaanza kumkosoa Yesu kwa akasema, “Mungu akuepushe mbali na mateso hayo, Bwana! Hilo halitakutokea!”
23Ndipo Yesu akamwambia Petro, “Ondoka kwangu, Shetani!#16:23 Shetani Jina la Mwovu lenye maana “Adui”. Maana ya Yesu ni kuwa Petro alikuwa akiongea kama Shetani. Hunisaidii! Hujali mambo ya Mungu. Unajali mambo ambayo wanadamu wanadhani ni ya muhimu.”
24Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Ikiwa yeyote miongoni mwenu anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima aache kujiwazia yeye mwenyewe na mahitaji yake. Ni lazima awe radhi kuubeba msalaba aliopewa na kunifuata mimi. 25Yeyote kati yenu anayetaka kuokoa uhai wake, ataupoteza. Lakini ninyi mlioyaacha maisha yenu kwa ajili yangu mtaupata uzima wa kweli. 26Haina maana kwenu ninyi kuupata ulimwengu wote, ikiwa ninyi wenyewe mtapotea. Mtu atalipa nini ili kuyapata tena maisha yake baada ya kuyapoteza? 27Mimi, Mwana wa Adamu, nitarudi katika utukufu wa Baba yangu pamoja na Malaika. Na nitamlipa kila mtu kutokana na matendo yake. 28Niaminini ninaposema wapo watu waliopo hapa watakaoishi mpaka watakaponiona nikija kama Mwana wa Adamu kutawala kama mfalme.”
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International