Yohana 13

13
Yesu Aiosha Miguu ya Wafuasi wake
1Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Yesu alijua kwamba wakati wake wa kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ulikuwa umefika. Daima Yesu aliwapenda watu wa ulimwengu huu waliokuwa wake. Huu ulikuwa wakati alipowaonesha upendo wake mkuu.
2Yesu na wafuasi wake walikuwa wakila chakula cha jioni. Ibilisi alikuwa tayari amekwisha kumshawishi Yuda Iskariote kumsaliti Yesu kwa maadui zake. (Yuda alikuwa Mwana wa Simoni.) 3Baba alikuwa amempa Yesu uwezo juu ya kila kitu. Naye Yesu alilifahamu hili. Alijua pia kuwa yeye alitoka kwa Mungu. Tena alijua kuwa alikuwa anarudi kwa Mungu. 4Kwa hiyo walipokuwa wakila,#13:4 wakila Wafuasi walikuwa kwenye makochi, wakiwa wameegemea kushoto kwao, na wakitumia mikono ya kulia kufikia vyombo vilivyokuwa mezani, vilivyowekwa mbele ya makochi. Yesu akamimina maji kwenye “jagi” (Wayunani huelezea kuwa hiki kilikuwa chombo kilichotumika maalumu kwa kusudi hilo) na kisha akaenda akimpitia mmoja mmoja nyuma ya kochi, ambako miguu ya wafuasi ilikuwa imenyooshwa. Yesu alisimama na kulivua vazi lake. Akachukua taulo na kuifunga kiunoni mwake. 5Kisha akamimina maji katika bakuli na kuanza kuwaosha miguu#13:5 kuwaosha miguu Utaratibu wa kijamii wa karne ya kwanza, kwa sababu watu walivaa viatu vya wazi katika barabara za vumbi jingi. Ulikuwa ni wajibu wa unyenyekevu, kawaida uliofanywa na mtumishi. Pia katika mstari wa 6-14. wafuasi wake. Kisha akaifuta miguu yao kwa taulo aliolifunga kiunoni mwake.
6Akamfikia Simoni Petro, naye Simoni Petro akamwambia, “Bwana, huwezi kuiosha miguu yangu.”
7Yesu akamjibu, “Huyaelewi ninayofanya hivi sasa. Lakini utayaelewa baadaye.”
8Petro akasema, “Hapana! Huwezi kamwe kuniosha miguu yangu kamwe.”
Yesu akamjibu, “Kama sitakuosha miguu yako, basi hutakuwa miongoni mwa watu wangu.”
9Simoni Petro akasema, “Bwana, utakapomaliza miguu, unioshe mikono na kichwa pia!”
10Yesu akamwambia, “Baada ya mtu kuoga, mwili wake wote huwa safi. Anahitaji tu kunawa miguu. Nanyi mko safi, lakini sio nyote.” 11Yesu alimjua yule atakayemsaliti mbele ya adui zake. Ndiyo maana alisema, “Sio wote mlio safi.”
12Yesu alipomaliza kuwaosha miguu wafuasi, alivaa nguo zake na kurudi pale mezani. Akawauliza, “Je! mmelielewa nililowafanyia? 13Mnaniita mimi ‘Mwalimu’. Tena mnaniita mimi ‘Bwana’. Hayo ni sahihi, kwa sababu hivyo ndivyo nilivyo. 14Mimi ni Bwana na Mwalimu wenu. Lakini niliwaosha miguu yenu kama mtumishi. Hivyo nanyi mnapaswa kuoshana miguu yenu. 15Nilifanya hivyo kama mfano. Hivyo nanyi mnapaswa kuhudumiana ninyi kwa ninyi kama nilivyowahudumia. 16Mniamini mimi, watumishi huwa sio wakubwa kuzidi bwana zao. Wale waliotumwa kufanya jambo fulani sio wakubwa kumzidi yule aliyewatuma. 17Sasa, mkielewa maana ya yale niliyotenda, Mungu atawabariki mkiyatendea kazi.
18Nami sizungumzii habari zenu nyote. Nawafahamu watu wale niliowachagua. Lakini Maandiko yanapaswa kutimia kama yanavyosema: ‘Mtu aliyekula chakula pamoja nami amenigeuka.’#13:18 amenigeuka Amenigeuka kwa hali halisi ina maana ya kuwa “Ameinua kisigino chake dhidi yangu.” Imenukuliwa kutoka Zab 41:9. 19Ninawaambia hili sasa kabla halijatokea. Hivyo litakapotokea, mtaweza kuamini kuwa MIMI NDIYE.#13:19 MIMI NDIYE Hili ni kama Jina la Mungu lililotumiwa katika Agano la Kale. Tazama Isa 41:4; 43:10; Kut 3:14. Hata hivyo, Inaweza kuwa na maana ya “Mimi Ndiye”, maana yake “Mimi Ndiye Masihi”. Pia katika mstari wa 28,58. 20Hakika nawaambieni, yeyote anayempokea mtu yule niliyemtuma ananipokea mimi pia. Na yeyote anayenipokea mimi humpokea pia yeye aliyenituma.”
Yesu Amtaja Atakayemgeuka
(Mt 26:20-25; Mk 14:17-21; Lk 22:21-23)
21Baada ya Yesu kuyasema mambo haya, alisumbuka sana moyoni. Akasema kwa uwazi, “Mniamini ninaposema kwamba mmoja wenu atanisaliti kwa maadui zangu.”
22Wafuasi wake wote wakatazamana wao kwa wao. Hawakuelewa kuwa Yesu alikuwa anamzungumzia nani. 23Mmoja wa wafuasi wake alikaa karibu na Yesu na alikuwa amemwegemea. Huyu alikuwa yule aliyependwa sana na Yesu. 24Simoni Petro akaonyesha ishara kwa mfuasi huyo amwulize Yesu alikuwa anamzungumzia nani.
25Yule mfuasi alisogea karibu sana na Yesu na kumwuliza, “Bwana, ni nani huyo?”
26Yesu akamjibu, “Nitachovya mkate huu kwenye bakuli. Mtu yule nitakayempa mkate huo ndiye mwenyewe.” Kwa hiyo Yesu akachukua kipande cha mkate, akakichovya, na akampa Yuda Iskariote, Mwana wa Simoni. 27Yuda alipoupokea mkate ule, Shetani akamwingia. Yesu akamwambia Yuda, “Yale unayotaka kuyafanya, yafanye haraka!” 28Hakuna hata mmoja pale mezani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia Yuda hayo. 29Kwa vile Yuda ndiye aliyekuwa msimamizi wa fedha#13:29 msimamizi wa fedha Mtunzaji wa fedha. Wafuasi walikuwa kama kundi moja walipokea michango na kuitunza pamoja kwa ajili ya mahitaji yao na kwa kuwasaidia maskini ila mmoja wao alisimamia sanduku la fedha. zao,#13:29 zao Kiongozi wa mambo ya fedha ni sawa na kusema kwamba yeye alikuwa anatunza mfuko wa fedha za wafuasi walizopata hata kwa kuchangiwa na watu wengine. baadhi yao walidhani kuwa Yesu alikuwa na maana kuwa Yuda aende kununua vitu ambavyo wangehitaji kwa ajili ya sherehe. Au walidhani kuwa Yesu alitaka Yuda aende na kuwapa maskini cho chote.
30Yuda akaula mkate aliopewa na Yesu. Kisha akatoka nje mara hiyo hiyo. Wakati huo ulikuwa ni usiku.
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
31Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa ni wakati wa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu. Na Mungu ataupokea utukufu kupitia kwake. 32Kama Mungu hupokea utukufu kupitia kwake, atampa Mwana Utukufu kupitia kwake yeye mwenyewe. Na hilo litatimia haraka sana.”
33Yesu akasema, “Watoto wangu, nitakuwa nanyi kwa kipindi kifupi tu kijacho. Nanyi mtanitafuta, lakini nawaambia sasa yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: Kule niendako ninyi hamwezi kuja.”
34“Nawapa amri mpya: Pendaneni ninyi kwa ninyi. Mnapaswa kupendana kama mimi nilivyowapenda ninyi. 35Endapo mtapendana ninyi kwa ninyi watu wote watatambua kuwa ninyi ni wafuasi wangu.”
Yesu Asema Petro Atamkana
(Mt 26:31-35; Mk 14:27-31; Lk 22:31-34)
36Simoni Petro akamwuliza Yesu, “Bwana, unaenda wapi?”
Yesu akajibu, “Kule niendako hamwezi kunifuata sasa. Lakini mtanifuata baadaye.”
37Petro akauliza, “Bwana, kwa nini nisikufuate sasa? Mimi niko radhi kufa kwa ajili yako!”
38Yesu akajibu, “Je! ni kweli utayatoa maisha yako kwa ajili yangu? Hakika nakwambia, kabla jogoo hajawika, utasema mara tatu kwamba hunijui mimi.”

ទើបបានជ្រើសរើសហើយ៖

Yohana 13: TKU

គំនូស​ចំណាំ

ចែក​រំលែក

ចម្លង

None

ចង់ឱ្យគំនូសពណ៌ដែលបានរក្សាទុករបស់អ្នក មាននៅលើគ្រប់ឧបករណ៍ទាំងអស់មែនទេ? ចុះឈ្មោះប្រើ ឬចុះឈ្មោះចូល