Logo YouVersion
Icona Cerca

Mwanzo 3

3
Uasi wa binadamu
1Nyoka#3:1 Nyoka: Katika Mashariki ya Kati ya Kale, nyoka alifikiriwa kuwa alama au ishara ya hekima na nguvu za kichawi. Zaidi ya hayo, ujanja wake ulitajwa kama kitendawili au methali. Tabia hizo za nyoka zimekuwa kama kiwakilishi cha nguvu mbaya zinazopinga mpango wa Mungu na ambazo hufikia hata kumshawishi mtu asitii amri ya Mungu. Kutokana na hayo, baadaye nyoka amekuwa ni sawa na Ibilisi au Shetani. Rejea Yoh 8:44; Ufu 12:9; 20:2. alikuwa mwerevu#3:1 Mwerevu: Neno hili linajumuisha maana potovu. Yahusu werevu ambao unao ndani yake uongo na udanganyifu. kuliko wanyama wote wa porini walioumbwa na Mwenyezi-Mungu. Basi, nyoka akamwambia huyo mwanamke, “Ati Mungu alisema msile matunda ya mti wowote bustanini?” 2Mwanamke akamjibu huyo nyoka, “Twaweza kula matunda ya mti wowote bustanini; 3lakini Mungu alisema, ‘Msile matunda ya mti ulio katikati ya bustani, wala msiuguse, msije mkafa.’” 4Nyoka akamwambia mwanamke, “Hamtakufa! 5Mungu alisema hivyo kwa sababu anajua kwamba mkila matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
6Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe, naye pia akala. 7Mara macho yao yakafumbuliwa, wakatambua kwamba wako uchi;#3:7 Wakatambua kwamba wako uchi: Taz Mwa 2:25 maelezo. hivyo wakajishonea majani ya mtini, wakajifanyia mavazi ya kiunoni.
8Jioni, wakati wa kupunga upepo, huyo mwanamume na mkewe wakasikia hatua za Mwenyezi-Mungu akitembea bustanini, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona. 9Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, “Uko wapi?”#3:9 Uko wapi?: Taz Mwa 4:9 maelezo. 10Naye akamjibu, “Nimesikia hatua zako bustanini, nikaogopa na kujificha, maana nilikuwa uchi.” 11Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?” 12Huyo mwanamume akajibu, “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala.”
13Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza huyo mwanamke, “Umefanya nini wewe?” Mwanamke akamjibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”
Adhabu
14Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia nyoka,
“Kwa kuwa umefanya hivyo,
umelaaniwa kuliko wanyama wote wa kufugwa,
na kuliko wanyama wote wa porini.
Kwa tumbo lako utatambaa,
na kula vumbi siku zote za maisha yako.
15Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke,
kati ya uzawa wako na uzawa wake;
yeye atakiponda kichwa chako,
nawe utamwuma kisigino chake.”#3:15 Rejea Rom 16:20; Ufu 12:17. Kwa Wakristo, neno “mzawa” linachukuliwa kuwa linamhusu Masiha ambaye alishinda nguvu za Shetani na uovu.
16Kisha akamwambia mwanamke,
“Nitakuzidishia uchungu wa kuzaa,
kwa uchungu utazaa watoto.
Hata hivyo utakuwa na hamu na mumeo,
naye atakutawala.”
17Kisha akamwambia huyo mwanamume,
“Kwa kuwa wewe umemsikiliza mkeo,
ukala matunda ya mti ambayo nilikuamuru usile;
kwa hiyo, kwa kosa lako ardhi imelaaniwa.#3:17 Kwa kosa lako ardhi imelaaniwa: Dhambi ya binadamu inaathiri ardhi ambayo ni makazi yao na ambamo wanapata chakula chao. Taz Mwa 12:2-3 maelezo.
Kwa jasho utajipatia humo riziki yako,#3:17 Kwa jasho utajipatia humo riziki yako: Taz Mwa 2:15 maelezo.
siku zote za maisha yako.
18Ardhi itakuzalia michongoma na magugu,
nawe itakubidi kula majani ya shambani.
19Kwa jasho lako utajipatia chakula
mpaka utakaporudi udongoni ulimotwaliwa;
maana wewe ni mavumbi, na mavumbini utarudi.”
20Adamu akampa mkewe jina “Hawa”,#3:20 Hawa: Katika Kiebrania, jina hilo lina maana ya “uhai” au “enye uhai”. kwani alikuwa mama wa binadamu wote. 21Mwenyezi-Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi#3:21 Mwenyezi-Mungu akawatengenezea …mavazi: Kitendo cha Mungu hapa bila shaka kinaonesha huruma yake; namna ya kutenda ya Mungu inajumuisha pia msamaha na ahadi ya kuokolewa wakati fulani. Taz pia namna ya kutenda inayofanana katika Mwa 4:15 maelezo. ya ngozi, akawavika.
Adamu na Hawa wanafukuzwa bustanini
22Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Sasa, binadamu amekuwa kama mmoja wetu, anajua mema na mabaya. Lazima kumzuia kula lile tunda la mti wa uhai, kwani akilila ataishi milele!” 23Basi, Mwenyezi-Mungu akamfukuza Adamu nje ya bustani ya Edeni, ili akailime ardhi ambamo alitwaliwa. 24Alimfukuza nje, na kuweka mlinzi#3:24 Mlinzi: Kiebrania “Kerubi” (wingi “Kerubimu”). Hao walifikiriwa kuwa viumbe wenye mabawa, na huko Mashariki ya Kati ya Kale walifikiriwa kuwa walinzi wa mahekalu na mahali patakatifu. Taz Kut 25:18 maelezo. upande wa mashariki wa bustani ya Edeni na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia iendayo kwenye mti wa uhai.#3:24 Hali ya kutoweza kuufikia mti wa uhai ndiyo adhabu yenyewe ambayo ilikuwa imetangazwa katika Mwa 2:17. Majaliwa ya awali ya binadamu ilikuwa kuwa hai lakini, kwa kuacha kumtii Mungu, binadamu alijitenga na Mungu aliye chanzo cha uhai wote; na kama dhambi ilivyoingia ulimwenguni ndivyo na kifo nacho (Rom 5:12).

Attualmente Selezionati:

Mwanzo 3: BHNTLK

Evidenziazioni

Condividi

Copia

None

Vuoi avere le tue evidenziazioni salvate su tutti i tuoi dispositivi?Iscriviti o accedi