Yohana 6

6
Isa alisha wanaume 5,000
(Mathayo 14:13-21; Marko 6:30-44; Luka 9:10-17)
1Baada ya haya, Isa alienda ng’ambo ya Bahari ya Galilaya (ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia). 2Umati mkubwa wa watu waliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa. 3Kisha Isa akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. 4Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
5Isa alipotazama na kuona umati ule mkubwa wa watu wakimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” 6Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya.
7Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili#6:7 Dinari 200 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 200. hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.”
8Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, 9“Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa watu hawa wote?”
10Isa akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi (palikuwa na wanaume wapatao elfu tano). 11Ndipo Isa akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka.
12Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.” 13Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula.
14Baada ya watu kuona muujiza ule Isa aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!” 15Isa akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake.
Isa atembea juu ya maji
(Mathayo 14:22-33; Marko 6:45-52)
16Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini. 17Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Isa alikuwa hajajumuika nao. 18Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. 19Wanafunzi walipokuwa wameenda mwendo wa maili tatu au nne#6:19 kama kilomita 5 au 6, walimwona Isa akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana. 20Lakini Isa akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.” 21Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda.
Watu wanamtafuta Isa
22Siku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ng’ambo waliona kwamba palikuwa na mashua moja tu, na kwamba Isa hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao. 23Lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Bwana Isa kumshukuru Mungu. 24Mara wale watu wakatambua kwamba Isa hakuwa hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Isa.
Isa ni mkate wa uzima
25Walipomkuta Isa ng’ambo ya bahari wakamuuliza, “Mwalimu, umefika lini huku?”
26Isa akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba#6:27 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi amemtia muhuri.”
28Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”
29Isa akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”
30Hivyo wakamuuliza, “Utafanya ishara gani ya muujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani? 31Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ”
32Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Musa aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
34Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”
35Isa akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe. 36Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini. 37Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuza nje kamwe. 38Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. 39Haya ndio mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. 40Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”
41Wayahudi wakaanza kunung’unika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” 42Wakasema, “Huyu si Isa, mwana wa Yusufu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?”
43Hivyo Isa akawaambia, “Acheni kunung’unikiana ninyi kwa ninyi. 44Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. 45Imeandikwa katika Manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Yeyote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu. 46Hakuna mtu yeyote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba. 47Amin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. 48Mimi ni mkate wa uzima. 49Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. 50Lakini hapa kuna mkate kutoka mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa. 51Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”
52Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?”
53Hivyo Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 54Mtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. 55Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56Yeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. 57Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. 58Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” 59Isa alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi#6:59 Nyumba ya ibada na mafunzo. huko Kapernaumu.
Wafuasi wengi wamwacha Isa
60Wengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?”
61Isa alipojua kwamba wafuasi wake wananung’unika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi? 62Ingekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza? 63Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima. 64Lakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Isa alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti. 65Akaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”
66Tangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata.
67Hivyo Isa akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?”
68Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. 69Tunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu.”
70Ndipo Isa akajibu, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Lakini mmoja wenu ni ibilisi.” 71(Hapa alikuwa anasema kuhusu Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili, ndiye ambaye baadaye angemsaliti Isa.)

Արդեն Ընտրված.

Yohana 6: ONMM

Ընդգծել

Կիսվել

Պատճենել

None

Ցանկանու՞մ եք պահպանել ձեր նշումները ձեր բոլոր սարքերում: Գրանցվեք կամ մուտք գործեք