Luka MT. 22
22
1IKAKARIBIA siku kuu ya mikate isiyochachwa, iitwayo Pasaka. 2Makuhani wakuu na waandishi wakatafuta njia ya kumwua, kwa maana walikuwa wakiwaogopa watu. 3Shetani akamwingia Yuda, aitwae Iskariote, nae alikuwa katika hesabu ya wale thenashara.
4Akaenda zake akasema na makuhani wakuu na majemadari jinsi ya kumtia katika mikono yao. 5Wakafurahi, wakapatana kumpa fedha. 6Akaahidi, akatafuta nafasi kumsaliti kwao pasipo kuwapo makutano. 7Ikawadia siku ya mikate isiyochachwa, ilipopasa kuchinja pasaka. 8Akapeleka Petro na Yohana, akisema, Enendeni, mkatuandikie pasaka, illi tuile. 9Wakamwambia, Wapi utakapo tuiandalie? 10Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini, atakutana nanyi mtu mume achukuae mtungi wa maji: mfuateni mpaka nyumba atakayoingia. 11Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula Pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? 12Na mtu yule atawaonyesha orofa kubwa iliyopambwa; huko andalieni. 13Wakaenda wakaona kama alivyowaambia, wakaiandalia Pasaka. 14Bassi saa ilipowadia, akaketi, na mitume pamoja nae. 15Akawaambia, Nimetamani sana kula pasaka hii pamoja nanyi, kabla va kuteswa: 16kwa maana nawaambieni, Sitaila kabisa hatta itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu. 17Akakipokea kikombe, akashukuru, akasema: Twaeni hiki mkagawanye ninyi kwa ninyi; 18Maana nawaambieni, Sitakunywa tangu sasa mazao ya mzabibu hatta ufalme wa Mungu utakapokuja. 19Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. 20Nacho kikombe vivyo hivyo baada ya kula, akinena, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu. 21Illa angalieni, mkono wake anisalitiye u pamoja nami mezani. 22Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyoamriwa; lakini ole wake mtu yule ambae anasalitiwa nae! 23Nao wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni nani katika wao atakaetenda neno hili. 24Kulikuwa na mashindano kwao, ni nani anaehesabiwa kuwa mkubwa. 25Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa wafadhili. 26Lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa wenu awe kama aliye mdogo; nafe atanguliae kama akhudumuye. 27Maana nani mkubwa, aketiye chakulani, ama akhudumuye? 28Siye aketiye chakulani? Lakini mimi kati mwenu kama akhudumuye. 29Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama alivyoniwekea Baba yangu; 30mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, na kuketi katika viti vya enzi, mkiwahukumu kabila thenashara za Israeli. 31Bwana akasema, Simon, Simon, tazama, Shetani amewataka ninyi awapepete kama nganu: 32lakini nimekuombea, illi imani yako isipunguke; nawe uongokapo, wathubutishe ndugu zako. 33Akamwambia, Bwana, pamoja nawe mimi ni tayari kwenda gerezani na kufa. 34Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla hujanikana marra tatu kwamba hunijui. 35Akawaambia, Nilipowatuma bila mifuko na mkoba na viatu, mlipunguka kitu? Wakasema, Hapana. 36Akawaambia, Bali sasa mwenye kifuko akitwae, na mkoba vivyo hivyo; nae asiye na upanga, auze joho yake, akanunue mmoja. 37Kwa maana nawaambieni, Hili lililoandikwa halina buddi kutimizwa kwangu, Alihesabiwa pamoja na maasi; kwa maana linipasalo lina mwisho. 38Wakasema, Bwana, tazama, panga mbili hizi. Akawaambia, Zatosha. 39Akatoka, akaenda zake hatta mlima wa mizeituni, kama ilivyo kawaida yake: wanafunzi wake wakamfuata. 40Alipofika pahali pale, akawaambia, Ombeni, msiingie majaribuni. 41Akiisha akajitenga nao kadiri ya mtupo wa jiwe, akapiga magoti, akaomba, akisema, 42Baba, ukipenda, uniondolee kikombe hiki: lakini si kama nitakavyo mimi, illa utakavyo wewe vifanyike. 43Akamtokea malaika toka mbinguni akimtia nguvu. 44Nae kwa kuwa alikuwa na huzuni sana, akazidi kuomba kwa bidii. Hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka hatta inchi. 45Alipoondoka katika kuomba, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala kwa huzuni, akawaambia, 46Mbona mnielala? Ondokeni, mkaombe, msipate kuingia majaribuni. 47Nae alipokuwa akisema, tazama, makutano, nae aitwae Yuda, mmoja wa wathenashara, akitangulia mbele yao, akamkaribia Yesu kumbusu. 48Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu? 49Nao waliokuwa pamoja nae walipoona yatakayokuwa, wakasema, Bwana, na tupige kwa upanga? 50Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio la kuume. 51Yesu akajibu, akasema, Acheni kadiri hii. Akamgusa sikio, akamponya. 52Yesu akawaambia waliomjia, makuhani wakuu, na majemadari wa hekalu, na wazee, Kama juu ya mnyanyangʼanyi mmetoka kwa panga na marungu? 53Killa siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono; lakini saa yenu hii, na mamlaka ya giza. 54Wakamkamata, wakamchukua, wakamleta nyumbani kwa kuhani mkuu; na Petro akafuata mbali. 55Hatta walipowasha moto kati yasebule wakaketi pamoja, akaketi Petro kati yao. 56Bassi, mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akisema, Huyu nae alikuwa pamoja nae. 57Akakana, akisema, Mwanamke, simjui. 58Na punde baadae mwingine akamwona, akasema, Na wewe u mmoja wao. Petro akasema, Ewe mtu, sio mimi. 59Hatta khalafu, kaciiri ya saa moja, mtu mwingine akahakikisha, akisema, Hakika na huyu alikuwa pamoja nae: kwa maana ni Mgalilaya. 60Petro akasema, Ewe mtu, sijui unenalo. Papo hapo alipokuwa akisema yeye, jogoo akawika. 61Bwana akageuka, akamtazamisha Petro: Petro akalikumbuka neno la Bwana, jinsi alivyomwambia, Kabla hajawika jogoo leo, utanikana marra tatu. 62Akatoka nje, akalia kwa uchungu. 63Na wale watu waliomshika Yesu, wakamdhihaki, wakampiga. 64Wakamfunika macho, wakamwuliza, wakisema, Fanya unabii, ni nani aliyekupiga? 65Wakamnena na mengine mengi kwa kufuru. 66Hatta ulipokuwa mchana wakakusanyika jamii ya wazee wa watu, na makuhani wakuu, na waandishi, wakamleta kwa haraza yao, wakisema, 67Kama wewe u Kristo, tuambie. Akawaambia, Nijapowaambieni, hamtaamini kabisa: 68nami nikiwaulizeni, hamtanijibu wala kuniachilia. 69Lakini tangu sasa Mwana wa Adamu atakuwa ameketi mkono wa kuume wa ukuu wa Mungu. 70Wakasema wote, Bassi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu? Akawaambia, Ninyi mnasema kama mimi ndiye. 71Wakasema, Bassi, mbona tunahitaji ushuhuda? Kwa maana sisi wenyewe tumesikia kwa kinywa chake.
Actualmente seleccionado:
Luka MT. 22: SWZZB1921
Destacar
Compartir
Copiar
¿Quieres guardar tus resaltados en todos tus dispositivos? Regístrate o Inicia sesión
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.