Waebrania 3
3
Yesu ni mkuu kuliko Mose
1Ndugu zangu, watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu Mtume na Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama. 2Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu. 3Lakini Yesu anastahili heshima kubwa kuliko Mose maana mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. 4Kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote. 5Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye. 6Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi wenyewe ni nyumba yake kama tukiendelea kuwa hodari na thabiti katika kile tunachotumainia.
Pumziko ambalo Mungu atawapa watu
7 # Taz Zab 95:7-11 Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu:
“Kama mkisikia sauti yake leo,
8msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasi
kama wakati ule wa majaribio kule jangwani.
9Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza,
ingawa walishuhudia matendo yangu kwa miaka arubaini!
10Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema,
‘Fikira za watu hawa zimepotoka,
hawajapata kamwe kuzijua njia zangu’.
11Basi, nilikasirika, nikaapa:
‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko.’
12Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai. 13Maadamu hiyo “Leo” inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi. 14Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni.
15 # Taz Zab 95:7-8 Maandiko yasema hivi:
“Kama mkisikia sauti yake leo,
msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasi.”
16Ni akina nani waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri. 17Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arubaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani. 18Mungu alipoapa: “Hawataingia mahali pangu pa pumziko,” alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi. 19Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini.
Currently Selected:
Waebrania 3: BHND
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Learn more about Biblia Habari Njema