Yohane 20
20
Kaburi tupu
(Mat 28:1-8; Marko 16:1-8; Luka 24:1-12)
1Alfajiri na mapema Jumapili,#20:1 Alfajiri na mapema Jumapili: Yaani baada ya kumalizika siku ya Sabato. kukiwa bado na giza, Maria Magdalene#20:1 Maria Magdalene: Jina lake linadokezea kwamba alitoka Magdala, mji uliokuwa katika mwambao wa magharibi mwa Ziwa Galilaya. Injili nyingine zinataja jinsi Yesu alivyomponya (Marko 16:9; Luka 8:2). alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa kaburi. 2Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda,#20:2 Simoni Petro na …mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda: Taz 1:42 na 13:23. akawaambia, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na wala hatujui walikomweka.” 3Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda kaburini. 4Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbio kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 5Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini hakuingia ndani. 6Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini; humo akaona sanda, 7na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani. Hicho kitambaa hakikuwekwa pamoja na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa mahali peke yake. 8Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyetangulia kufika kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaamini. ( 9Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema kwamba ilikuwa lazima afufuke kutoka kwa wafu). 10Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani.
Yesu anamtokea Maria Magdalene
(Mat 28:9-10; Marko 16:9-11)
11Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia. Huku akiwa bado analia, aliinama na kuchungulia kaburini, 12akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni. 13Hao malaika wakamwuliza, “Mama, kwa nini unalia?” Naye akawaambia, “Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!”
14Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu amesimama hapo, lakini asitambue ya kuwa ni Yesu. 15Yesu akamwuliza, “Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?” Maria, akidhani kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia, “Mheshimiwa, kama ni wewe umemwondoa, niambie ulikomweka, nami nitamchukua.” 16Yesu akamwambia, “Maria!” Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, “Raboni”#20:16 Raboni: Hapa mwandishi wa Injili hii ya Yohane ametumia namna nyingine ya kuandika jina Rabi (taz 1:38). Jina hilo la sifa lilitumika aghalabu kwa waalimu walioheshimika sana. (yaani “Mwalimu”). 17Yesu akamwambia, “Usinishike; sijaenda bado juu kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu uwaambie: naenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu.” 18Hivyo Maria Magdalene akaenda akawapasha habari wale wanafunzi kuwa amemwona Bwana, na kwamba alikuwa amemwambia hivyo.
Yesu anawatokea wanafunzi wake
(Mat 28:16-20; Marko 16:14-18; Luka 24:36-49)
19Ilikuwa jioni ya siku hiyo ya Jumapili. Wanafunzi walikuwa wamekutana pamoja ndani ya nyumba, na milango ilikuwa imefungwa kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi.#20:19 Kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi: Hofu yao ni kwamba wangetambuliwa na kusumbuliwa kwa sababu ya imani yao; kwa hiyo wakawa wamejificha katika nyumba, mlango ukiwa umebanwa. Basi, Yesu akaja, akasimama kati yao, akawaambia, “Amani kwenu!” 20Alipokwisha sema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake.#20:20 Akawaonesha mikono yake na ubavu wake: Aliwaonesha alama alizozipata kutokana na kusulubiwa msalabani kwa misumari na baadaye maaskari kumtoboa ubavuni mwake. Basi, hao wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana. 21Yesu akawaambia tena, “Amani kwenu! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma nyinyi.” 22Alipokwisha sema hayo, akawapulizia#20:22 Akawapulizia: Kama Mungu alivyompulizia mtu uhai wakati wa kuumbwa ulimwengu (taz Mwa 2:7). na kuwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu.#20:22 Pokeeni Roho Mtakatifu: Yesu anawapa wafuasi wake Roho Mtakatifu kama alivyoahidi hapo kabla (14:16,26; 16:7). Kwa namna nyingine kitendo hicho kinamaanisha kwamba tangu sasa watakuwa na uhai unaotokana na Roho Mtakatifu. 23Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa;#20:23 Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa …: Baada ya kuwapa Roho Mtakatifu Yesu anawapa kipaji cha kusamehe dhambi. Iliaminika kwamba uwezo huo ulikuwa ni uwezo wa Mungu lakini sasa Yesu anasema wanafunzi wake wataushiriki. Uwezo wa kanisa wa kusamehe dhambi una msingi wake katika kutumwa na Yesu (20:21). msipowasamehe, hawasamehewi.”
Yesu na Thoma
24Thoma, mmoja wa wale kumi na wawili (aitwaye Pacha), hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja. 25Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.” Thoma akawaambia, “Nisipoona mikononi mwake alama za misumari na kutia kidole changu katika kovu hizo, na kutia mkono wangu ubavuni mwake, sitasadiki.”
26Basi, baada ya siku nane hao wanafunzi walikuwa tena pamoja mle ndani, na Thoma alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja, akasimama kati yao, akasema, “Amani kwenu!” 27Kisha akamwambia Thoma, “Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini!” 28Thoma akamjibu, “Bwana wangu na Mungu wangu!”#20:28 Bwana wangu na Mungu wangu: Maneno haya ya Tomaso ni kilele cha Kitabu hiki, maneno makamilifu ya imani ya Kikristo katika Yesu Kristo kama Bwana na Mungu wa wote wanaomwamini. 29Yesu akamwambia, “Je, unaamini kwa kuwa umeniona? Heri yao wale ambao hawajaona, lakini wameamini.”
Shabaha ya kitabu#20:30-31 Sababu ya kuandikwa kwa kitabu hiki 2:11; 6:7; 7:31. Yohane anadokezea hapa kwamba watu ambao hawakupata kumwona Yesu kwa macho yao wenyewe (20:29) wanapata fursa, kwa ishara zilizoandikwa katika kitabu hiki, ya kumwamini Yesu.
30Yesu alifanya mbele ya wanafunzi wake ishara nyingine nyingi ambazo hazikuandikwa katika kitabu hiki. 31Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mpate kuwa na uhai kwa nguvu ya jina lake.
Currently Selected:
Yohane 20: BHNTLK
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993
The Bible Society of Kenya 1993