Yohane 19
19
1Basi, Pilato akaamuru Yesu achukuliwe, apigwe viboko.#19:1 Apigwe viboko: Ilikuwa kawaida kwa Waroma kuwapiga mijeledi watumwa waliohukumiwa kifo. Lakini ilikuwa marufuku kuwapiga mijeledi raia wa Roma (taz Mate 22:25) 2Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika na joho la rangi ya zambarau.#19:2 Joho la rangi ya zambarau: Joho la namna hiyo walivikwa wafalme au viongozi wa nchi kuonesha kuwa ni wenye madaraka, na hapa madhumuni yake ni kumdhihaki Yesu. 3Wakawa wanakuja mbele yake na kusema: “Shikamoo, Mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga makofi. 4Pilato akatoka nje tena, akawaambia, “Tazameni, namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sikuona hatia yoyote kwake.” 5Basi, Yesu akatoka nje amevaa taji ya miiba na joho la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni! Mtu mwenyewe ni huyo.” 6Makuhani wakuu na walinzi#19:6 Makuhani wakuu na walinzi: Yaelekea ndio waliokuwa wachochezi sana ili Yesu asulubiwe. walipomwona wakapaza sauti: “Msulubishe! Msulubishe!” Pilato akawaambia, “Mchukueni basi, nyinyi wenyewe mkamsulubishe, kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake.”#19:6 Mimi sikuona hatia yoyote kwake: Kwa mara ya tatu Pilato anasisitiza kuwa Yesu hakutenda kosa lolote (taz aya 4; taz pia 18:38; ling Mat 27:19). 7Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria, na kufuatana na sheria hiyo, ni lazima afe,#19:7 Tunayo sheria …lazima afe: Sheria yenyewe inayotajwa hapa ni Lawi 24:16. kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.”
8Pilato aliposikia maneno hayo akazidi kuogopa. 9Basi, akaingia ndani ya ikulu tena, akamwuliza Yesu, “Umetoka wapi wewe?” Lakini Yesu hakumjibu neno. 10Hivyo Pilato akamwambia, “Husemi nami? Je, hujui kwamba ninayo mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukusulubisha?” 11Yesu akamjibu, “Hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa na Mungu. Kwa sababu hiyo, yule aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi.”#19:11 Yule aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi: Huyo au ni Yuda Iskarioti, au ni kuhani mkuu Kayafa. 12Tangu hapo, Pilato akawa anatafuta njia ya kumwachilia, lakini Wayahudi wakapiga kelele: “Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu anayejifanya kuwa mfalme humpinga Kaisari!” 13Basi, Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu,#19:13 Akaketi juu ya kiti cha hukumu: Wengine wanatafsiri “Akamketisha juu ya kiti cha hukumu”. mahali paitwapo “Sakafu ya Mawe” (kwa Kiebrania, Gabatha).
14Ilikuwa yapata saa sita mchana,#19:14 Ilikuwa yapata saa sita mchana: Hiyo ilikuwa saa au wakati ambapo Waisraeli kule hekaluni wakiwa pamoja na makuhani walikuwa wanachinja wale kondoo wa karamu ya Pasaka (rejea Yoh 18:19). siku ya maandalio ya Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, “Tazameni, Mfalme wenu!” 15Wao wakapaza sauti: “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe Mfalme wenu?” Makuhani wakuu wakajibu, “Sisi hatuna mfalme isipokuwa Kaisari!” 16Hapo, Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe.
Yesu anasulubiwa msalabani
(Mat 27:32-44; Marko 15:21-32; Luka 23:26-43)
Basi, wakamchukua Yesu. 17Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo “Fuvu la Kichwa” (kwa Kiebrania Golgotha).#19:17 Fuvu la kichwa …Golgotha: Labda mahali hapo paliitwa hivyo kwa kuwa kilima chenyewe kilifanana na fuvu la kichwa cha mtu. 18Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye Yesu katikati. 19Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: “Yesu Mnazareti, Mfalme wa Wayahudi.” 20Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji. Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki.#19:20 Ilani imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki: Pilato alitaka watu wote wasome ilani hiyo. Kiebrania kilikuwa lugha ya Wayahudi (lakini lugha ya watu wa kawaida ilikuwa Kiaramu, lugha ya Kisemiti inayofanana sana na Kiebrania); Kilatini kilikuwa lugha rasmi ya Waroma hata ingawa Waroma wengi waliongea pia Kigiriki ambacho wakati huo kilikuwa lugha ya biashara ambayo ilifahamika na watu wengi katika nchi za mwambao wa Bahari ya Mediteranea. 21Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, “Usiandike: ‘Mfalme wa Wayahudi,’ ila ‘Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’” 22Pilato akajibu, “Niliyoandika, nimeandika!”
23Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono. 24Basi, hao askari wakashauriana: “Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani.” Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo:
“Waligawana mavazi yangu,
na nguo yangu wakaipigia kura.”
Basi, ndivyo walivyofanya hao askari.
25Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. 26Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda,#19:26 Mwanafunzi aliyempenda: Yafikiriwa kuwa ni Yohane (taz pia 13:23; 21:20). akamwambia mama yake, “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” 27Halafu akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
Yesu anakufa
(Mat 27:45-56; Marko 15:33-41; Luka 23:44-49)
28Kisha, Yesu aliona kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, “Naona kiu.” 29Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki.#19:29 Siki: Yaani divai kali iliyokaa kwa siku nyingi ikiwa imepunguzwa nguvu kwa kutumia kinywaji kingine. Yasemekana maaskari walizoea kufanya hivyo kabla ya kuinywa. Kupewa siki ni tendo lililotokea kama ilivyotabiriwa katika Zab 69:21; taz pia Mat 27:34,38; Marko 15:36; Luka 23:36. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo,#19:29 Husopo: Mmea mdogo wenye matawi mafupi na ambao matawi yake yaliweza kutumiwa kwa urahisi kama ilivyotajwa hapa (taz pia 1Fal 4:33). wakamwekea mdomoni. 30Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, “Yametimia!”#19:30 Yametimia: Yesu aliposema “yametimia” alimaanisha sio tu kwamba maisha yake ya hapa duniani yalikuwa yamefikia mwisho ila kwamba ile kazi ambayo Mungu alikuwa amemtuma kuja kuifanya hapa duniani kwa kujitolea kwake na kufa msalabani kwa ajili ya dhambi za ulimwengu (1:29) ilikuwa imetimia. Kisha akainamisha kichwa, akatoa roho.
Yesu anachomwa mkuki ubavuni
31Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe#19:31 Miguu …ivunjwe: Kumvunja miguu mtu aliyesulubiwa ilikuwa njia ya kumwua upesi. na miili yao iondolewe. 32Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu. 33Lakini walipomfikia Yesu, waliona kwamba alikwisha kufa, kwa hivyo hawakumvunja miguu. 34Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji. ( 35Naye aliyeona tukio hilo ameshuhudia ili nanyi mpate kuamini. Na hayo aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli). 36Jambo hilo lilitendwa ili Maandiko Matakatifu yatimie: “Hapana hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.” 37Tena Maandiko mengine yanasema: “Watamtazama yule waliyemtoboa.”
Yesu anazikwa
(Mat 27:57-61; Marko 15:42-47; Luka 23:50-56)
38Baada ya hayo, Yosefu,#19:38 Yosefu: Yosefu huyu wa Arimathaya (kijiji yapata kilomita 30 kaskazini-magharibi mwa Yerusalemu) anatajwa katika Injili ya Marko na Luka kwamba alikuwa mmoja wa Baraza kuu la Wayahudi (taz Marko 15:43; Luka 23:50). Katika Injili ya Mathayo anatajwa tu kwamba alikuwa tajiri (taz Mat 27:57) na jambo hilo huenda lilikusudiwa kumpatia Yesu mazishi ya kufaa. mwenyeji wa Arimathaya, alimwomba Pilato ruhusa ya kuuchukua mwili wa Yesu. (Yosefu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini kwa siri, maana aliwaogopa viongozi wa Wayahudi). Basi, Pilato akamruhusu. Hivyo Yosefu alikwenda, akauondoa mwili wa Yesu. 39Naye Nikodemo#19:39 Nikodemo: Taz 3:1 maelezo. ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu usiku, akaja akiwa amechukua mchanganyiko wa manemane na ubani#19:39 Mchanganyiko wa manemane na ubani: Manemane na ubani vyote viliwili vilikuwa vitu vyenye harufu nzuri vilivyotolewa kutoka mimea fulani. kiasi cha kilo thelathini. 40Basi, waliutwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda pamoja na manukato kufuatana na desturi ya Wayahudi katika kuzika. 41Mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa na bustani, na katika bustani hiyo kulikuwa na kaburi#19:41 Bustani …kaburi: Mahali penyewe hapajulikani dhahiri. Lakini bila shaka palikuwa karibu na Golgotha (19:17). Mathayo (27:60) anasema kaburi hilo lilikuwa kaburi alilotengeneza Yosefu kwa ajili yake mwenyewe. jipya ambalo hakutiwa bado mtu yeyote ndani yake. 42Basi, kwa sababu ya shughuli za Wayahudi za maandalio ya Sabato, na kwa vile kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamweka Yesu humo.
Currently Selected:
Yohane 19: BHNTLK
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993
The Bible Society of Kenya 1993