YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 49

49
Upumbavu wa kutegemea mali
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi)
1Sikieni jambo hili enyi watu wote!
Tegeni sikio enyi wakazi wote wa dunia;
2sikilizeni nyote, wakubwa kwa wadogo,
matajiri na maskini kwa pamoja.
3Maneno yangu yatakuwa mazitomazito;
mimi nitasema maneno ya hekima.
4Nitatega sikio nisikilize methali,
nitafafanua kitendawili kwa muziki wa zeze.
5Ya nini niogope siku mbaya,
wakati nizungukwapo na uovu wa adui?
6Watu waovu hutegemea mali zao,
hujisifia wingi wa utajiri wao.
7Lakini binadamu hawezi kamwe kujikomboa mwenyewe;
hawezi kumlipa Mungu bei ya maisha yake,
8maana fidia ya maisha ni kubwa mno.
Hawezi kutoa kitu chochote kinachotosha,
9kimwezeshe aendelee kuishi daima,
asipate kuonja kaburi.
10Yeye afahamu kuwa hata wenye hekima hufa,
wapumbavu hali kadhalika na watu wajinga.
Wote hao huwaachia wengine mali zao.
11Makaburi ni makao yao hata milele;
ni makao yao vizazi hata vizazi,
ingawa hapo awali walimiliki ardhi.
12Binadamu hatadumu katika fahari yake;
atakufa tu kama mnyama.
13Hayo ndiyo yawapatao wanaojiamini kipumbavu,
ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao.
14Wataongozwa kama kondoo hadi kuzimu,
kifo kitakuwa mchungaji wao.
Watashuka moja kwa moja kaburini.
Miili yao itaozea huko,
Kuzimu kutakuwa makao yao.#49:14 maana katika Kiebrania si dhahiri.
15Lakini Mungu ataniokoa na kuzimu.
Atanisalimisha kutoka huko.
16Usihangaike ukiona mtu anatajirika,
wala mali yake ikiongezeka zaidi na zaidi.
17Maana atakapokufa hatachukua chochote,
mali yake haitashuka huko chini pamoja naye.
18Ajapojikuza katika maisha haya,
na kusifiwa kwa sababu ya kufanikiwa,
19atajiunga na wazee waliomtangulia kufa,
ambao hawawezi kuona tena mwanga.
20Binadamu hatadumu milele katika fahari yake,
atakufa tu kama mnyama.

Currently Selected:

Zaburi 49: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in