YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 33

33
Utenzi wa kumsifu Mungu
1Shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu!
Kumsifu Mungu ni wajibu wa watu wanyofu.
2Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa zeze;
mwimbieni kwa kinubi cha nyuzi kumi.
3Mwimbieni wimbo mpya;
pigeni kinubi vizuri na kushangilia.
4Neno la Mwenyezi-Mungu ni la kweli;
na matendo yake yote ni ya kuaminika.
5Mungu apenda uadilifu na haki,
dunia imejaa fadhili za Mwenyezi-Mungu.
6Mbingu ziliumbwa kwa neno la Mwenyezi-Mungu,
na vyote vilivyomo kwa pumzi ya mdomo wake.
7Alikusanya maji ya bahari kama katika chupa,
vilindi vya bahari akavifunga ghalani.
8Dunia yote na imwogope Mwenyezi-Mungu!
Wakazi wote duniani, wamche!
9Maana alisema na ulimwengu ukawako;
alitoa amri nao ukajitokeza.
10Mwenyezi-Mungu hupangua mipango ya mataifa,
na kuyatangua mawazo yao.
11Mpango wa Mwenyezi-Mungu hudumu milele;
maazimio yake yadumu vizazi vyote.
12Heri taifa ambalo Mungu wake ni Mwenyezi-Mungu;
heri wale aliowachagua kuwa watu wake mwenyewe!
13Mwenyezi-Mungu huangalia chini kutoka mbinguni,
na kuwaona wanadamu wote.
14Kutoka kwenye kiti chake cha enzi,
huwaangalia wakazi wote wa dunia.
15Yeye huunda mioyo ya watu wote,
yeye ajua kila kitu wanachofanya.
16Mfalme hawezi kuokolewa kwa kuwa na jeshi kubwa;
wala shujaa hapati ushindi kwa nguvu zake kubwa.
17Farasi wa vita hafai kitu kwa kupata ushindi;
nguvu zake nyingi haziwezi kumwokoa mtu.
18Mwenyezi-Mungu huwaangalia wale wamchao,
watu ambao wanatumainia fadhili zake.
19Yeye huwaokoa katika kifo,
huwaweka hai wakati wa njaa.
20Mioyo yetu yamtumainia Mwenyezi-Mungu.
Yeye ni msaada wetu na ngao yetu.
21Naam twafurahi kwa sababu yake;
tuna matumaini katika jina lake takatifu.
22Fadhili zako zikae nasi, ee Mwenyezi-Mungu,
kwani sisi tumekuwekea tumaini letu.

Currently Selected:

Zaburi 33: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in