YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 33

33
Maafa kwa mwangamizi
1Ole wako ewe mwangamizi,
unayeangamiza bila wewe kuangamizwa!
Ole wako wewe mtenda hila,
ambaye hakuna aliyekutendea hila!
Utakapokwisha kuangamiza
wewe utaangamizwa!
Utakapomaliza kuwatendea watu hila
wewe utatendewa hila.
2Ee Mwenyezi-Mungu, utuonee huruma,
kwako tumeliweka tumaini letu.
Uwe kinga yetu kila siku,
wokovu wetu wakati wa taabu.
3Kwa kishindo cha sauti yako watu hukimbia;
unapoinuka tu, mataifa hutawanyika.
4Maadui zao wanakusanya mateka,
wanayarukia kama panzi.
5Mwenyezi-Mungu ametukuka,
yeye anaishi juu mbinguni.
Ameujaza Siyoni haki na uadilifu.
6Enyi watu wa Yerusalemu,
Mwenyezi-Mungu atawajalieni usalama,
atawaokoa na kuwapa hekima na maarifa.
Hazina yenu kuu ni kumcha Mwenyezi-Mungu.
7Haya, mashujaa wao wanalia,
wajumbe wa amani wanaomboleza.
8Barabara kuu zimebaki tupu;
hamna anayesafiri kupitia humo.
Mikataba inavunjwa ovyo,
mashahidi wanadharauliwa.
Hamna anayejali tena maisha ya binadamu.
9Nchi inaomboleza na kunyauka;
misitu ya Lebanoni imekauka,
bonde zuri la Sharoni limekuwa jangwa,
huko Bashani na mlimani Karmeli
miti imepukutika majani yake.
Mwenyezi-Mungu awaonya maadui zake
10Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Sasa mimi nitainuka;
sasa nitajiweka tayari;
sasa mimi nitatukuzwa.
11Mipango yenu yote ni kama makapi,
na matokeo yake ni takataka tupu.
Pumzi yangu#33:11 Pumzi yangu: Kadiri ya hati kadhaa za kale; makala ya Kiebrania ina pumzi yenu. itawaangamiza kama moto.
12Watu watakuwa kama wamechomwa kuwa majivu,
kama miiba iliyokatwa na kuteketezwa motoni.
13Sikilizeni mambo mliyofanya enyi mlio mbali,
nanyi mlio karibu kirini uwezo wangu.”
14Wenye dhambi katika Siyoni wanaogopa,
wasiomcha Mungu wanatetemeka na kusema:
“Nani awezaye kuukaribia moto huu mkali?
Nani awezaye kustahimili miali ya moto wa milele?”
15Ni mtu aishiye kwa uadilifu na asemaye ukweli;
mtu anayedharau kabisa utajiri wa dhuluma,
anayekataa hongo kata kata,
asiyekubali kamwe kusikia mipango ya mauaji,
wala hakubali macho yake yaone maovu.
16Mtu wa namna hiyo anaishi juu,
mahali salama penye ngome na miamba;
chakula chake atapewa daima,
na maji yake ya kunywa hayatakosekana.
Wakati mzuri ujao
17Mtaweza kumwona mfalme katika fahari yake,
mtaiona nchi anayotawala, kubwa na pana.
18Mtafikiria tisho lililopita na kujiuliza,
“Wako wapi wale waliokadiria na kukisia kodi?
Wako wapi wale waliopeleleza ulinzi wetu?”
19Hamtawaona tena watu wale wenye kiburi,
wanaozungumza lugha isiyoeleweka.
20Tazameni Siyoni tunamofanya sikukuu zetu;
tazameni mji Yerusalemu, makao matulivu, hema imara;
vigingi vyake havitangolewa kamwe,
kamba zake hazitakatwa hata moja.
21Humo Mwenyezi-Mungu atatuonesha ukuu wake.
Kutakuwa na mito mikubwa na vijito,
ambamo meli za vita hazitapita,
wala meli kubwa kuingia.
22Maana Mwenyezi-Mungu ni hakimu wetu,
yeye ni mtawala wetu;
Mwenyezi-Mungu ni mfalme wetu,
yeye ndiye anayetuokoa.
23Ewe Siyoni, kamba zako zimelegea,
haziwezi kushikilia matanga yake,
wala kuyatandaza.
Lakini nyara nyingi zitagawanywa;
hata vilema wataweza kuchukua sehemu yao.
24Hakuna atakayesema tena ni mgonjwa;
watu watasamehewa uovu wao wote.

Currently Selected:

Isaya 33: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in