2 Wamakabayo 12
12
Wayahudi wa Yopa wauawa
1Makubaliano ya amani kati ya Wayahudi na Wasiria yalipokamilika, Lisia alirejea kwa mfalme na Wayahudi wakarudia kazi zao za shambani. 2Lakini baadhi ya wakuu wa sehemu hizo, yaani, Timotheo na Apolonio mwana wa Genaeo, hali kadhalika, Hieronimo na Demofoni, na pia Nikanori kamanda wa askari wa kukodiwa kutoka Kupro, hawakuwaacha Wayahudi watulie na kuishi kwa amani. 3Nao watu wa Yopa walitenda jambo baya sana kwa Wayahudi wa mji wao. Walijifanya kuwa marafiki wa Wayahudi, wakawaalika pamoja na jamaa zao kwenda nao kwenye meli zao ili wasafiri. 4Kwa kuwa watu wote wa mji huo walikuwa wameamua kufanya hivyo, Wayahudi hawakutia shaka, wakakubali mwaliko huo kwa moyo ulio radhi. Lakini walipokuwa baharini, watu wa Yopa wakawazamisha majini Wayahudi wasiopungua 200, wote wakafa maji.
5Mara alipopata habari ya kitendo hicho kikatili walichokuwa wametendwa Wayahudi wenzake, Yuda aliwaarifu watu wake. 6Baada ya kumwomba Mungu, hakimu mwenye haki, wakawashambulia wauaji hao. Usiku wakaichoma moto bandari na kuunguza meli zote, na kuwaulia mbali wote waliowafuma wamejificha melini. 7Kisha, kwa kuwa milango ya mji ilikuwa imefungwa kabisa, Yuda akaenda zake, akikusudia kurudi Yopa wakati mwingine na kuwafutilia mbali wakazi wake wote.
8Yuda aliposikia kwamba watu wa Yamnia walikuwa na mpango wa kuwaua Wayahudi wa mji wao pia, 9akawashambulia watu wa Yamnia usiku, akachoma moto bandari yake na meli zilizokuwa bandarini, hata miali ya moto huo ikaonekana kutoka Yerusalemu, umbali wa kilomita hamsini.
Ushindi wa Yuda katika eneo la Gileadi
(1Mak 5:9-54)
10Yuda na watu wake walipokuwa wanaondoka kutoka hapo kwenda kupambana na Timotheo, wakiwa yapata kilomita mbili tu kutoka Yamnia, walishambuliwa ghafla na Waarabu zaidi ya 5,000, wakisaidiwa na askari wapandafarasi 500. 11Baada ya mapigano makali sana, kwa msaada wa Mungu, Yuda na wenzake walishinda. Ndipo mabedui hao walioshindwa wakaomba wawe marafiki wa Wayahudi, wakiahidi kuwapa wanyama na kuwasaidia kwa njia nyinginezo. 12Yuda akaona urafiki huo ungeweza kuwafaa Wayahudi kwa namna nyingi, akakubali kufanya nao amani. Baada ya hayo, Waarabu wakarudi kwenye mahema yao.
13Yuda pia aliushambulia mji wa Kaspini, uliokuwa umezungushiwa maboma na kuta. Wenyeji waliokaa humo mjini walikuwa mchanganyiko wa watu wa mataifa mengine. 14Wakazi wa huko walitegemea uimara wa kuta zao, na walikuwa na imani kwamba chakula walichokuwa wameweka akiba kingewatosha kwa muda wote wa kuzingirwa. Kwa hiyo wakaifanyia Yuda na watu wake dhihaka na hata kumkufuru Mungu na kutoa matusi. 15Lakini Wayahudi wakasali kwa Mwenyezi-Mungu, Bwana wa ulimwengu, ambaye alikuwa ameziporomosha kuta za Yeriko wakati wa Yoshua bila ya kutumia mitambo ya kubomolea au silaha nyinginezo. Kisha wakaushambulia kwa nguvu huo ukuta, 16na kwa sababu Mungu alitaka, wakauteka mji. Wayahudi waliwaua watu wengi hivi hata ziwa la karibu, ambalo lilikuwa na upana upatao robo kilomita, likaonekana linafurika damu.
Yuda ashinda jeshi la Timotheo
(1Mak 5:37-44)
17Kutoka mji wa Kaspini, Yuda na watu wake walisafiri umbali wa kilomita 150 hivi, wakawasili kwenye makazi ya Wayahudi ya Karaksi, karibu na mji wa Tobu. 18Lakini hawakumkuta Timotheo hapo, kwa vile alikuwa amekwisha ondoka sehemu hizo. Hakuwa amefanya lolote hapo, isipokuwa kuacha kikosi hodari katika ngome fulani. 19Makapteni wawili wa Yuda Makabayo, Dositheo na Sosipateri, wakaishambulia ngome hiyo na kuwaua wote walioachwa humo na Timotheo, watu 10,000. 20Halafu Yuda Makabayo akaligawa jeshi lake katika vikosi kadha, akawaweka Dositheo na Sosipateri waongoze kila mmoja kikosi chake, akaondoka mbio kumwandama Timotheo, aliyekuwa na askari wa miguu 120,000, na wapandafarasi 2,500. 21Timotheo alipogundua kwamba Yuda alikuwa anamwandama, aliwatanguliza wanawake na watoto pamoja na mizigo, waende Karnaimu, mji ambao ulikuwa karibu hauwezekani kuuzingira au hata kuufikia, kwa sababu vinjia vya kuendea huko vilikuwa vyembamba. 22Lakini kikosi cha kwanza cha Yuda kilipotokeza tu, askari maadui wakashikwa na woga mkubwa kutokana na maono yaliyoletwa na Mungu, aonaye kila kitu. Katika hofu hiyo, walianza kukimbia ovyo huko na huko, na wengi wao wakajeruhiwa kwa mapanga ya wenzao. 23Hapo Yuda na watu wake wakawafukuza maadui kwa kasi, wakawaua askari wapatao 30,000. 24Timotheo mwenyewe alikamatwa na askari wa Dositheo na Sosipateri. Lakini alikuwa mwerevu sana. Alifaulu kuwasadikisha kwamba jamaa zao wengi walikuwa wafungwa wake, na kwamba wangeuawa kama yeye asingeachiliwa aende zake. 25Hatimaye, baada ya kuahidi kuwarudisha makwao hao jamaa za askari, Timotheo aliachiwa huru.
Ushindi mwingine wa Yuda
(1Mak 5:45-54)
26Kisha Yuda alishambulia mji wa Karnaimu na hekalu la Atargati mungu wa kike, akawaua watu 25,000. 27Halafu, baada ya maangamizi hayo, akaushambulia pia mji wa Efroni wenye boma, makao ya Lisia na#12:27 Lisia na: Hati kadha hazina maneno haya. watu kutoka mataifa yote. Vijana wenye nguvu wakajipanga mbele ya kuta, wakapiga vita kwa ujasiri. Na ndani ya mji mlikuwa na akiba kubwa ya zana za vita na silaha. 28Lakini Wayahudi wakasali kuomba msaada kwa Bwana, avunjaye nguvu za adui. Hivyo wakauteka mji huo na kuwaua watu wapatao 25,000. 29Kutoka hapo wakaenda kwa haraka Skithopoli, mji uliopo kilomita 120 kaskazini ya Yerusalemu. 30Wayahudi waliokuwa huko walimweleza Yuda jinsi wakazi wa mji huo walivyowafanyia hisani, hasa wakati wa shida. 31Basi, Yuda na watu wake wakawashukuru wenyeji hao na kuwahimiza waendelee kuwaonesha nia njema Wayahudi siku za mbele. Kisha wakaondoka na kwenda zao Yerusalemu, ambako waliwasili muda mfupi tu kabla ya sikukuu ya mavuno.
Yuda amshinda Gorgia
32Baada ya sikukuu iitwayo Pentekoste Yuda na watu wake wakaondoka haraka kumkabili Gorgia, gavana wa Idumea, 33ambaye alipambana nao akiwa na askari wa miguu 3,000, na wapandafarasi 400. 34Katika mapigano hayo Wayahudi wachache waliuawa. 35Lakini Myahudi mmoja kutoka mji wa Tobu, mpandafarasi mwenye nguvu, aliyeitwa Dositheo, alimshika Gorgia kwa kulikamata vazi lake, akaanza kumkokota kwa nguvu, akiwa na lengo la kumteka nyara huyo mlaanifu. Lakini, ghafla, mmoja wa wapandafarasi wa Thrakia akamwendea mbio Dositheo na kumkata mkono wake; kwa hiyo Gorgia akafaulu kutoroka na kwenda zake mjini Marisa.
36Wakati huo Wayahudi waliokuwa chini ya kamanda Esdri walikuwa wamepiga vita kwa muda mrefu, wakawa wamechoka. Basi, Yuda akasali ili Bwana aoneshe kwamba alikuwa upande wao, na kwamba anaongoza vikosi vyao. 37Ndipo, Yuda alipokuwa anapiga mbiu ya vita na kuimba utenzi kwa lugha yake ya wazee wake, Wayahudi wakawashambulia ghafla Gorgia na watu wake; maadui wakakimbia.
Sala za kuwaombea waliouawa vitani
38Kisha Yuda aliwaongoza watu wake kwenda mjini Adulamu. Hiyo ilikuwa siku kabla ya Sabato, kwa hiyo wakajitakasa kadiri ya desturi ya Kiyahudi, kisha wakaadhimisha Sabato hapo. 39Siku iliyofuata waliona ni haraka na muhimu kukusanya miili ya wenzao waliokuwa wameuawa vitani, na kuizika katika makaburi ya wazee wao. 40Lakini katika kila maiti, walikuta zimefichwa nguoni sanamu ndogondogo za miungu iliyoabudiwa Yamnia, jambo ambalo sheria inawakataza Wayahudi kuzivaa. Hapo kila mtu alijua kwa nini hao walikuwa wameuawa. 41Hivyo wakazisifu njia za Bwana, hakimu mwenye haki, afichuaye vilivyofichika, 42na wakamwomba Bwana afutilie mbali dhambi hiyo. Kisha, Yuda, yule mtu mwadilifu, akawataka watu waepuke dhambi, kwa sababu walikuwa wamejionea wenyewe yaliyokuwa yamewapata wale waliokuwa wametenda dhambi. 43Pia alichangisha kutoka kwa watu wake fedha ipatayo drakma 2,000 akaipeleka Yerusalemu kwa ajili ya tambiko ya kuondoa dhambi. Yuda alifanya tendo hilo jema kwa sababu aliamini juu ya ufufuo wa wafu. 44Kama asingekuwa na imani kwamba wafu watafufuliwa, ingekuwa ni upumbavu na kazi bure kuwaombea marehemu. 45Lakini akiwa anatazamia tuzo nzuri waliowekewa waliokufa wakiwa waaminifu kwa Mungu, hilo lilikuwa wazo jema na takatifu. Kwa hiyo Yuda alitolea tambiko ya upatanisho ili watu wapate kuondolewa dhambi zao.
Currently Selected:
2 Wamakabayo 12: BHND
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Learn More About Biblia Habari Njema