YouVersion Logo
Search Icon

2 Wamakabayo 11

11
Yuda Makabayo amshinda Lisia
(1Mak 4:26-35)
1Mara baada ya hayo, si muda mrefu baada ya Timotheo kushindwa, Lisia, mlinzi na ndugu ya mfalme na mkuu wa serikali, alipata habari hizo. Alikasirika sana, 2akaongoza askari wa miguu 80,000 na wapandafarasi wake wote dhidi ya Wayahudi. Alikuwa na shabaha ya kuufanya mji wa Yerusalemu makao ya Wagiriki, 3na kulitoza kodi hekalu, kama mahali pengine pote pa ibada ya watu wa mataifa mengine. Na ukuhani mkuu ungenadiwa kila mwaka. 4Lisia hakujali chochote juu ya uwezo wa Mungu, bali alijivunia makumi elfu ya askari wake wa miguu, maelfu ya wapandafarasi wake, na tembo wake themanini. 5Hivi akaivamia Yudea na kuishambulia ngome ya Beth-zuri, yapata kilomita thelathini kusini ya Yerusalemu.
6Yuda Makabayo na watu wake waliposikia kwamba Lisia alikuwa anazizingira ngome zao, wakalia na kuomboleza pamoja na watu wote, wakimsihi Bwana amtume malaika mwema awaokoe. 7Yuda Makabayo alikuwa wa kwanza kuchukua silaha, akawahimiza wengine wajiunge naye katika kutoa mhanga maisha yao ili kuwasaidia Wayahudi wenzao. Hivi, wakatoka pamoja naye kwa ari na motomoto kabisa. 8Lakini, kabla hawajaenda mbali na Yerusalemu, kwa ghafla wakagundua kwamba walikuwa wanaongozwa na mpandafarasi mwenye mavazi meupe, amechukua silaha za dhahabu. 9Mara, wote kwa pamoja, wakamshukuru Mungu kwa huruma yake; alikuwa amewatia ujasiri wa kutosha kwa kushambulia si binadamu tu, bali pia wanyama wakali na hata kuta za chuma. 10Basi, wakaenda mbele wamejipanga kivita, wakiwa pamoja na yule msaidizi kutoka mbinguni, maana Bwana alikuwa amewaonea huruma. 11Kama simba, waliwarukia maadui zao na kuwaangusha askari wa miguu 11,000, na wapandafarasi 1,600, na kuwafanya wengine wakimbie. 12Wengi wa hao waliokimbia walikuwa wamejeruhiwa na kupoteza silaha zao. Hata Lisia mwenyewe alikimbia kwa aibu.
Lisia apatana na Wayahudi
(1Mak 6:56-61)
13Lisia, kwa vile hakuwa mjinga, alitafakari juu ya kushindwa kwake vitani, akatambua kwamba Wayahudi walikuwa hawashindiki kwa sababu Mungu Mwenye Nguvu alikuwa amewapigania. Kwa hiyo akapeleka ujumbe, 14akawashawishi wakubali kupatana kwa masharti ya haki, na akaahidi kumshawishi mfalme awe rafiki wao. 15Kwa manufaa ya watu wake, Yuda Makabayo akayakubali mapendekezo yote ya Lisia, kwa vile mfalme alikuwa ameyapokea na kuyakubalia maombi yote ambayo Yuda alikuwa amempa Lisia kwa maandishi.
Barua ya Lisia kwa Wayahudi
16Ifuatayo ni barua ambayo Lisia aliwaandikia Wayahudi:
“Mimi Lisia kwa taifa la Wayahudi, salamu. 17Wajumbe wenu, Yohane na Absalomu, wamenikabidhi hati maalumu ambayo mliwatuma waniletee, na wameniomba nikubaliane na yaliyoandikwa katika hati hiyo. 18Nimemwarifu mfalme kuhusu masuala yote ambayo mlitaka kuweka mbele yake, naye amekubali kufanya lolote linalowezekana. 19Kama mtaendelea kuwa waaminifu kwa serikali, nitafanya kila niwezalo siku za mbele, kwa manufaa ya taifa lenu. 20Nimewaagiza wajumbe wenu na wawakilishi wangu kukutana nanyi na kujadiliana mambo hayo katika vipengele vyake vyote. 21Nawatakieni kila la fanaka. Imeandikwa siku ya ishirini na nne ya mwezi Dioskorinthio, mwaka 148.”#11:21 Mwaka 148: Ni sawa na 164 K.K.
Barua ya mfalme kwa Lisia
22Na barua ya mfalme ilikuwa kama ifuatavyo:
“Mimi mfalme Antioko kwa ndugu yangu Lisia, salamu. 23Kwa kuwa baba yangu amekwenda kujiunga na miungu, nataka raia wa ufalme wangu kuendesha mambo yao wenyewe bila kuingiliwa. 24Naelewa kwamba Wayahudi hawataki kuishi kadiri ya utamaduni wa Kigiriki - kama baba yangu alivyokuwa amenuia - ila wanapendelea kuishi kadiri ya utamaduni wao, na wameomba waruhusiwe kuishi hivyo. 25Kwa vile natamani waishi bila wasiwasi kama mataifa mengine katika milki yangu, sasa natoa amri kwamba warudishiwe hekalu lao, na kuruhusiwa kuishi kadiri ya mila za wazee wao. 26Basi, itakuwa vema kuwajulisha juu ya uamuzi huu, na kuwahakikishia kwamba nitakuwa rafiki kwao, ili waweze kuendesha mambo yao wenyewe kwa amani, bila wasiwasi wowote.”
27Ifuatayo ni barua ya mfalme kwa taifa la Wayahudi:
“Mimi mfalme Antioko kwa Baraza Kuu la Wayahudi na Wayahudi wengine wote, salamu. 28Natumaini mambo yenu yote yanawaendea vizuri kama ninavyotamani. Mimi ni mzima wa afya. 29Menelao ameniarifu kwamba mnataka kurudi nyumbani na kushughulika na mambo yenu wenyewe. 30Kwa hiyo, basi, baadhi yenu watakaorudi nyumbani ifikapo tarehe kumi na tatu ya mwezi Ksanthiko, ninawaapia, wasiogope chochote. 31Mnaweza kuendelea kushika sheria zenu kuhusu vyakula, na nyinginezo, kama mlivyokuwa mmezoea. Na hapana Myahudi atakayenyanyaswa kwa mambo yaliyofanyika bila kujua. 32Ninamtuma Menelao kuwatieni moyo. 33Tunawatakieni fanaka. Imeandikwa siku ya kumi na tano ya mwezi Ksanthiko, mwaka 148.”#11:33 Mwaka 148: Ni sawa na 164 K.K.
Barua ya Waroma kwa Wayahudi
34Waroma nao waliwaandikia Wayahudi barua ifuatayo:
“Kwinto Memio na Tito Manio, wawakilishi wa Waroma, kwa Wayahudi, salamu. 35Sisi tunakubaliana kabisa masharti yote mliyopewa na Lisia, nduguye mfalme. 36Sasa tumo njiani kwenda Antiokia; kwa hiyo, yachunguzeni kwa makini masuala yale ambayo Lisia alimwuliza mfalme. Halafu tuleteeni majibu haraka kusudi tuweze kuwawakilisheni kwa mfalme, kwa manufaa yenu. Fanyeni hilo mapema iwezekanavyo, 37bila kukawia, ili tuweze kujua mmeamua nini. 38Tunawatakieni fanaka. Imeandikwa siku ya kumi na tano ya mwezi Ksanthiko, mwaka 148.”#11:38 Mwaka 148: Ni sawa na 164 K.K.

Currently Selected:

2 Wamakabayo 11: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in