Mwanzo 31
31
Yakobo anamutoroka Labani
1Basi, Yakobo akasikia kwamba wana wa Labani walinungunika na kusema: “Yakobo amepeleka kila kitu cha baba yetu; ndivyo alivyopata kuwa tajiri.” 2Yakobo alijua vilevile kwamba Labani hakumujali yeye kama pale mbele. 3Kisha Yawe akamwambia Yakobo: “Rudia katika inchi ya wazee wako na kwa jamaa yako, nami nitakuwa pamoja nawe.”
4Basi Yakobo akatuma watu kuita Rakeli na Lea kumukutana katika shamba alimokuwa anachunga nyama wake. 5Yakobo akawaambia: “Unaona kwamba baba yenu hanijali tena kama vile mbele. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. 6Munajua kwamba nimemutumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote. 7Hata hivyo yeye amenidanganya na kubadilisha mushahara wangu mara kumi. Lakini Mungu hakumuruhusu kunizuru. 8Kila mara baba yenu aliposema: ‘Nyama wenye madoadoa ndio watakaokuwa mushahara wako’, basi kundi lote lilizaa nyama wenye madoadoa. Na kila mara aliposema: ‘Nyama wenye mistari ndio watakaokuwa mushahara wako’, basi, kundi lote lilizaa nyama wenye mistari. 9Ndivyo Mungu alivyotwaa nyama wa baba yenu, akanipa mimi.
10“Wakati wa nyama kupata mimba niliota ndoto, na katika ndoto hiyo niliona mabeberu wote waliopanda madike walikuwa wenye mistari, madoadoa na matakamataka. 11Malaika wa Mungu akaongea nami katika ndoto hiyo, akaniita: ‘Yakobo’, nami nikaitika, ‘Niko hapa!’ 12Naye akaniambia: ‘Angalia mabeberu wote wanaowapanda madike wana mistari, madoadoa na matakamataka. Jambo hili limekuwa hivyo kwa sababu nimeona jinsi Labani alivyokutendea. 13Mimi ndimi yule Mungu aliyekutokea kule Beteli, pahali pale ulipotakasa lile jiwe kwa kulimiminia mafuta na ambapo ulifanyia kiapo. Sasa ondoka katika inchi hii urudi katika inchi yako.’ ”
14Rakeli na Lea wakamujibu Yakobo: “Sisi hatuna tena sehemu au urizi wowote katika nyumba ya baba yetu! 15Tena yeye anatuona sisi kama wageni, kwa maana ametuuzisha. Naye amekula mali yetu. 16Mali yote ambayo Mungu ametwaa kutoka kwa baba yetu ni yetu, sisi na watoto wetu. Kwa hiyo, fanya yale Mungu aliyokuagiza!”
17Basi, Yakobo akajitayarisha kusafiri, akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia. 18Alitwaa nyama wake wote pamoja na mali yote aliyopata kule Padani-Aramu, akaanza safari ya kurudi katika inchi ya Kanana kwa baba yake Isaka. 19Wakati ule Labani alikuwa amekwenda kukata manyoya ya nyama wake. Hivyo Rakeli akapata nafasi ya kuiba sanamu za miungu ya baba yake. 20Yakobo akamudanganya Labani wa Aramu kwa kuondoka bila kumujulisha. 21Basi, Yakobo akatwaa mali yake yote, akatoroka. Kisha kuvuka muto Furati, akaelekea Gileadi, inchi ya milima.
Labani anamufuata Yakobo
22Nyuma ya siku tatu, Labani akajulishwa kwamba Yakobo amemutoroka. 23Basi, Labani akawatwaa wandugu zake, akamufuata Yakobo kwa muda wa siku saba, akamukuta katika milima, katika inchi ya Gileadi. 24Lakini usiku, Mungu akamutokea Labani wa Aramu katika ndoto, akamwambia: “Ujichunge! Usimwambie Yakobo neno lolote, jema au baya.”
25Basi, Labani akamufikia Yakobo. Wakati ule Yakobo alikuwa amepiga kambi yake kwenye milima. Labani naye, pamoja na wandugu zake, akapiga kambi yake kwenye milima ya Gileadi.
26Halafu Labani akamwambia Yakobo: “Umefanya nini? Mbona umenidanganya, ukatwaa wabinti zangu kama vile wafungwa wa vita? 27Kwa nini ulitoroka kwa siri, ukanidanganya, wala haukuniarifu kusudi nipate kukuaga kwa shangwe, nyimbo, matari na vinubi? 28Mbona haukunipa wakati wa kubusu wabinti na wajukuu wangu? Kweli umetenda kipumbafu! 29Nina uwezo wa kukuzuru; lakini Mungu wa baba yako alinitokea usiku wa kuamukia leo, akaniambia nifanye angalisho, akisema: ‘Ujichunge! Usimwambie Yakobo neno lolote, zuri au baya’. 30Ninajua ulitoroka kwa sababu ya hamu kubwa ya kurudi katika nyumba ya baba yako. Lakini kwa nini uliiba sanamu za miungu yangu?”
31Yakobo akamujibu: “Niliogopa kwa sababu nilizani ungeninyanganya wabinti zako. 32Lakini ukipata mumoja kati yetu na sanamu za miungu yako, atakufa! Mbele ya hawa wandugu zetu, onyesha chochote kinachokuwa chako, ukitwae.” Yakobo hakujua kwamba Rakeli alikuwa ameiba sanamu za miungu ya Labani.
33Basi, Labani akatafuta sanamu hizo za miungu yake katika hema la Yakobo, la Lea na la wale wajakazi wawili; lakini hakuzipata. Akatoka katika hema la Lea na kuingia katika hema la Rakeli. 34Rakeli alikuwa ametwaa zile sanamu, akazificha chini ya matandiko ya ngamia na kuketi juu yake. Labani akazitafuta katika hema lote; lakini hakuzipata.
35Halafu Rakeli akamwambia baba yake: “Tafazali baba, usiuzike, maana siwezi kusimama mbele yako kwa sababu niko katika siku zangu.” Basi, Labani akatafuta sanamu za miungu yake, lakini hakuzipata.
36Kwa hiyo Yakobo akakasirika, akagombana na Labani akisema: “Kosa langu ni nini hata ukanifuatilia namna hii? 37Umepata kitu gani kinachokuwa chako hata kupekua mizigo yangu yote? Ukiweke mbele ya wandugu zangu na wandugu zako, kusudi wao waamue kati yetu sisi wawili! 38Nimekaa nawe kwa muda wa miaka makumi mbili. Muda ule wote kondoo wako, wala mbuzi wako hawajapata kuharibu mimba, wala sikukula kondoo dume wa kundi lako. 39Mimi sikukuletea nyama wako aliyeuawa na nyama wa pori, lakini nilibeba hasara hiyo mimi mwenyewe. Wewe ulinidai nyama aliyeibwa muchana au usiku! 40Hivyo, muchana nilivumilia jua kali na usiku baridi ilinipiga. Sikuweza kupata usingizi hata kidogo. 41Kwa miaka makumi mbili hii yote nimeishi katika nyumba yako. Nilikutumikia miaka kumi na mine kwa ajili ya wabinti zako wawili, na miaka sita nikachunga nyama wako. Lakini wewe, ukabadilisha mushahara wangu mara kumi. 42Kama Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu ambaye ni kitisho cha Isaka, asingelikuwa upande wangu, hakika ungeliniacha niondoke mikono mitupu. Lakini Mungu aliona mateso yangu na kazi niliyofanya kwa mikono yangu, akakukaripia usiku wa kuamukia leo.”
43Halafu Labani akamujibu Yakobo: “Wabinti hawa ni wabinti zangu, watoto hawa ni watoto wangu, nyama hawa ni nyama wangu, na yote unayoona hapa ni yangu. Lakini mimi ninaweza kufanya nini leo juu ya hawa wabinti zangu na watoto wao waliowazaa? 44Basi, tufanye agano mimi nawe, likuwe ushuhuda kati yako nami.”
45Basi, Yakobo akatwaa jiwe, akalisimika kama nguzo ya ukumbusho. 46Tena Yakobo akawaambia wandugu zake: “Mukusanye mawe.” Nao wakakusanya mawe na kufanya lundo. Kisha wakakula chakula karibu na lundo lile la mawe. 47-48Wakaita lundo lile “Lundo la ushuhuda”. Labani akaliita katika kiaramea Yegari-Sahaduta; Yakobo akaliita katika kiebrania Galedi. Labani akasema: “Lundo hili ni ushuhuda kati yako na mimi leo.” 49Ile nguzo akaiita Misipa, ni kusema “Nafasi ya Ulinzi”, maana alisema: “Yawe akuwe mulinzi kati yako na mimi tunapokuwa mbali bila kuonana. 50Kama ukitesa wabinti zangu, au ukioa wanawake wengine zaidi ya hawa, basi ujue kwamba hakuna anayekuwa mushuhuda kati yetu ila Mungu mwenyewe.” 51Halafu Labani akamwambia Yakobo: “Angalia lundo hili la mawe na nguzo ambayo nimeisimika kati yako nami. 52Lundo hili na nguzo hii ni ushuhuda kwamba mimi sitaruka lundo hili kuja kwako kukuzuru, wala wewe hautavuka lundo hili na nguzo hii kuja kwangu kunizuru. 53Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Nahori, ataamua kati yetu.”
Basi, Yakobo akaapa kwa Mungu ambaye ni kitisho cha baba yake Isaka. 54Kisha akatoa sadaka kule kwenye mulima na kuwaalika wandugu zake wakule chakula. Kisha kula, wakabaki kule usiku kucha.
Currently Selected:
Mwanzo 31: SWC02
Highlight
Share
Copy
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fen.png&w=128&q=75)
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.