YouVersion Logo
Search Icon

Mithali 8

8
1 # Mit 1:20-21; 9:3; 1 Kor 1:24 Je! Hekima halii?
Ufahamu hatoi sauti yake?
2Juu ya mahali palipoinuka karibu na njia,
Penye njia panda, ndipo asimamapo.
3Karibu na malango, mahali pa kuingia mjini,
Mahali pa kuyaingilia malango anapiga kelele.
4Enyi watu, nawaita ninyi;
Na sauti yangu ni kwa wanadamu.
5Enyi wajinga, fahamuni werevu,
Nanyi wapumbavu, mpate moyo wa kufahamu.
6 # Zab 49:3; Mit 2:6,7; Kol 1:26 Sikilizeni, maana nitasema yaliyo mazuri,
Na kufumbua midomo yangu kutakuwa maadili.
7 # Yn 8:14; Rum 15:8 Maana kinywa changu kitasema kweli,
Na uovu ni chukizo kwa midomo yangu.
8Maneno yote ya kinywa changu yana haki;
Hapana hata neno lililopotoka au la ukaidi.
9Yote humwelea yule afahamuye,
Yote huelekea mbele yao waliopata maarifa.
10Pokea mafundisho yangu, wala si fedha,
Na maarifa kuliko dhahabu safi.
11 # Ayu 28:15; Zab 19:10 Maana hekima ni bora kuliko marijani;
Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.
12Mimi, hekima, nimefanya werevu kuwa makao yangu;
Natafuta maarifa na busara.
13 # Mit 16:6; 4:24; Zek 8:17; 1 Pet 5:5 Kumcha BWANA ni kuchukia uovu;
Kiburi na majivuno, na njia mbovu,
Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.
14 # Mhu 7:19 Ushauri ni wangu, na maarifa yaliyo sahihi;
Mimi ni ufahamu, mimi nina nguvu.
15 # Dan 2:21; Mt 28:18; Rum 13:1 Kwa msaada wangu wafalme humiliki,
Na wakuu wanahukumu haki.
16Kwa msaada wangu wakuu hutawala,
Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia.
17 # 1 Sam 2:30; Yak 1:5 Nawapenda wale wanipendao,
Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
18 # Mt 6:33 Utajiri na heshima ziko kwangu,
Naam, utajiri udumuo, na haki pia.
19 # Ayu 28:15; Mit 3:14 Matunda yangu ni bora kuliko dhahabu, naam, dhahabu safi,
Na faida yangu ni bora kuliko fedha iliyo safi.
20Natembea katika njia ya haki,
Katikati ya mapito ya hukumu.
21Niwarithishe mali wale wanipendao,
Tena nipate kuzijaza hazina zao.
Sehemu ya busara katika uumbaji
22 # Ufu 3:14; Mit 3:19; Yn 1:1 BWANA alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake,
Kabla ya matendo yake ya kale.
23 # Mwa 1:26; Zab 2:6; Mik 5:2; Yn 17:24 Nilitukuka tokea milele, tangu awali,
Kabla haijakuwako dunia.
24Wakati havijakuwapo vilindi nilizaliwa,
Wakati hazijakuwapo chemchemi zilizojaa maji.
25 # Ayu 15:7 Kabla milima haijawekwa imara,
Kabla ya vilima nilizaliwa.
26Alipokuwa hajaiumba dunia, wala mashamba
Wala chanzo cha udongo wa dunia;
27Alipozithibitisha mbingu nilikuwako;
Alipopiga duara katika uso wa bahari;
28Alipofanya imara mawingu yaliyo juu;
Chemchemi za bahari zilipopata nguvu;
29 # Ayu 38:4,10 Alipoipa bahari mpaka wake,
Kwamba maji yake yasiasi amri yake;
Alipoiagiza misingi ya nchi;
30 # Yn 1:1,2,18; Mt 3:17; Kol 1:13 Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi;
Nikawa furaha yake kila siku;
Nikifurahi daima mbele zake;
31 # Isa 4:2; Zab 16:3 Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu;
Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.
32 # Lk 11:28 Basi, wanangu, nisikilizeni sasa;
Maana heri hao wazishikao amri zangu.
33Sikieni mafundisho, mpate hekima,
Wala msiikatae.
34Ana heri mtu yule anisikilizaye,
Akisubiri sikuzote malangoni pangu,
Akingoja penye vizingiti vya milango yangu.
35 # Yn 3:16,36; Flp 3:8,9 Maana yeye anionaye mimi aona uzima,
Naye atapata kibali kwa BWANA.
36 # Ebr 2:3 Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe,
Na wao wanichukiao hupenda mauti.

Currently Selected:

Mithali 8: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy