Mwanzo 3
3
Kuanguka Kwa Mwanadamu
1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao bwana Mwenyezi Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”
2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”
4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5 Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
6 Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala. 7 Ndipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika.
8 Ndipo yule mwanaume na mkewe, waliposikia sauti ya bwana Mwenyezi Mungu alipokuwa akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka mbele za bwana Mwenyezi Mungu katikati ya miti ya bustani. 9 Lakini bwana Mwenyezi Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?”
10 Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.”
11 Mungu akamuuliza, “Ni nani aliyekuambia ya kuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?”
12 Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa sehemu ya tunda kutoka kwenye huo mti, nami nikala.”
13 Ndipo bwana Mwenyezi Mungu akamuuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”
14 Hivyo bwana Mwenyezi Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili,
“Umelaaniwa kuliko wanyama wote
wa kufugwa na wa porini!
Utatambaa kwa tumbo lako
na kula mavumbi
siku zote za maisha yako.
15 Nami nitaweka uadui
kati yako na huyo mwanamke,
na kati ya uzao wako na wake,
yeye atakuponda kichwa,
nawe utamuuma kisigino.”
16 Kwa mwanamke akasema,
“Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;
kwa utungu utazaa watoto.
Tamaa yako itakuwa kwa mumeo
naye atakutawala.”
17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’
“Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,
kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo
siku zote za maisha yako.
18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,
nawe utakula mimea ya shambani.
19 Kwa jasho la uso wako
utakula chakula chako
hadi utakaporudi ardhini,
kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,
kwa kuwa wewe u mavumbi
na mavumbini wewe utarudi.”
20 Adamu akamwita mkewe Hawa, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai.
21 bwana Mwenyezi Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. 22 Kisha bwana Mwenyezi Mungu akasema, “Sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya. Sharti asiruhusiwe kunyoosha mkono wake na kuchuma pia kutoka mti wa uzima akala, naye akaishi milele.” 23 Hivyo bwana Mwenyezi Mungu akamfukuzia mbali kutoka Bustani ya Edeni, akalime ardhi ambamo alitolewa. 24 Baada ya kumfukuzia mbali Adamu, Mungu akaweka makerubi mashariki ya Bustani ya Edeni, pamoja na upanga wa moto ukimulika huku na huko kulinda njia ya kuuendea mti wa uzima.
Okuqokiwe okwamanje:
Mwanzo 3: NMM
Qhakambisa
Dlulisela
Kopisha
Ufuna ukuthi okuvelele kwakho kugcinwe kuwo wonke amadivayisi akho? Bhalisa noma ngena ngemvume
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018 by Biblica, Inc.
Used with permission.
All rights reserved worldwide.