Mwanzo 12
12
Wito wa Abramu
1Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonesha.
2“Nitakufanya taifa kubwa
na nitakubariki,
Nitalikuza jina lako,
nawe utakuwa baraka.
3Nitawabariki wale wanaokubariki,
na yeyote akulaaniye nitamlaani;
na kupitia kwako mataifa yote duniani
yatabarikiwa.”
4Hivyo Abramu akaondoka kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwambia; naye Lutu akaondoka pamoja naye. Abramu alipoitwa aondoke Harani, alikuwa na umri wa miaka sabini na tano. 5Abramu akamchukua Sarai mkewe pamoja na Lutu mwana wa ndugu yake, mali yote waliyokuwa nayo, pamoja na watu aliokuwa amewapata huko Harani, wakasafiri kwenda nchi ya Kanaani, na wakafika huko.
6Abramu akasafiri katika nchi hiyo hadi huko Shekemu, mahali penye mwaloni wa More. Wakati huo Wakanaani walikuwa wanaishi katika nchi hiyo. 7Mwenyezi Mungu akamtokea Abramu, akamwambia, “Nitawapa uzao wako nchi hii.” Hivyo hapo akamjengea madhabahu Mwenyezi Mungu aliyekuwa amemtokea.
8Kutoka huko Abramu akasafiri kuelekea kwenye vilima mashariki mwa Betheli, naye akapiga hema huko, Betheli ikiwa upande wa magharibi na Ai upande wa mashariki. Huko alimjengea Mwenyezi Mungu madhabahu na akaliitia jina la Mwenyezi Mungu.
9Kisha Abramu akasafiri kuelekea upande wa Negebu.
Abramu akiwa Misri
10Basi kulikuwa na njaa katika nchi hiyo, naye Abramu akashuka kwenda Misri kukaa huko kwa muda, kwa maana njaa ilikuwa kali. 11Alipokaribia kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, “Ninajua kwamba wewe ni mwanamke mzuri wa sura. 12Wamisri watakapokuona, watasema, ‘Huyu ni mke wake.’ Kisha wataniua, lakini wewe watakuacha hai. 13Sema wewe ni dada yangu, ili nitendewe mema kwa ajili yako, na maisha yangu yahifadhiwe kwa sababu yako.”
14Abramu alipoingia Misri, Wamisri wakamwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana wa sura. 15Maafisa wa Farao walipomwona, wakamsifia kwa Farao; ndipo Sarai akapelekwa kwa nyumba ya mfalme. 16Kwa ajili ya Sarai, Farao akamtendea Abramu mema, naye Abramu akapata kondoo, ng’ombe, punda, ngamia, na watumishi wa kiume na wa kike.
17Lakini Mwenyezi Mungu akamwadhibu Farao na nyumba yake kwa maradhi ya kufisha kwa sababu ya kumchukua Sarai, mke wa Abramu. 18Ndipo Farao akamwita Abramu, akamuuliza, “Umenifanyia nini? Kwa nini hukuniambia yeye ni mke wako? 19Kwa nini ulisema, ‘Yeye ni dada yangu,’ hata nikamchukua kuwa mke wangu? Sasa basi, mke wako huyu hapa. Mchukue uende zako!” 20Kisha Farao akawapa watu wake amri kuhusu Abramu, wakamsindikiza pamoja na mke wake na kila alichokuwa nacho.
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.