1 Mose 32
32
Yakobo anakutana na malaika.
1Yakobo alipokwenda safari yake akakutana na malaika wa Mungu.#1 Mose 28:12; Sh. 34:8. 2Yakobo alipowaona akasema: Hapa ndipo kambi la Mungu, akapaita mahali pale Mahanaimu (Makambi Mawili).
Yakobo anamwogopa Esau.
3Yakobo akatuma wajumbe kwenda katika nchi ya Seiri kwenye bara ya Edomu, wamtangulie kufika kwake mkubwa wake Esau.#1 Mose 36:8. 4Akawaagiza kwamba: Hivi ndivyo, mmwambie bwana wangu Esau: Hivi ndivyo, mtumishi wako Yakobo anavyosema: Nimekaa ugenini kwake Labani, nikakawilia huko mpaka sasa, 5nikapata ng'ombe na punda, mbuzi na kondoo, watumwa wa kiume na wa kike, nikatuma kumpasha bwana wangu habari hizi, nijipatie upendeleo machoni pako. 6Hao wajumbe waliporudi kwake Yakobo akamwambia: Tumefika kwa mkubwa wako Esau, naye anakuja na watu 400, mkutane njiani. 7Ndipo, Yakobo alipoogopa sana na kusongeka moyoni, akawagawanya watu, aliokuwa nao, hata mbuzi na kondoo, nao ng'ombe na ngamia kuwa vikosi viwili, 8akasema: Esau atakapojia kikosi kimoja na kukishinda, hicho kingine kitakachosalia kitapata kupona.
Yakobo anamwomba Mungu.
9Kisha Yakobo akaomba: Mungu wa baba yangu Aburahamu na Mungu wa baba yangu Isaka, wewe Bwana umeniambia: Rudi katika nchi yako kwenye ndugu zako! Mimi nitakufanyizia mema.#1 Mose 31:3,13. 10Hivyo, nilivyo mdogo, sipaswi na magawio yote wala na welekevu wote, uliomfanyizia mtumishi wako. Kwani hapo, nilipouvuka mto huu wa Yordani niliishika hii fimbo yangu tu, lakini sasa ni mwenye vikosi viwili.#2 Sam. 7:18. 11Niponye mkononi mwa mkubwa wangu Esau! Kwani namwogopa, asije, akanipiga mimi na wamama pamoja na wana. 12Wewe nawe umesema: Nitakufanyizia mema kweli, nao wa uzao wako nitawafanya kuwa wengi kama mchanga wa ufukoni usiohesabika kwa wingi.#1 Mose 28:13-14.
Yakobo anatafuta mapatano na Esau.
13Kisha akalala huko usiku huo, akatoa katika yale mapato yaliyokuwa mkononi mwake matunzo ya kumpa kaka yake Esau: 14mbuzi majike 200 na madume 20, kondoo majike 200 na madume 20, 15ngamia wanyonyeshao 30 pamoja na wana wao, ng'ombe majike 40 na madume 10, punda majike 20 na wana wa punda 10; 16akawatia mikononi mwa watumwa wake, kundi kwa kundi peke yake, akawaambia hawa watumwa wake: Nitangulieni, tena katikati ya kila makundi mawili acheni nafasi. 17Naye wa kwanza akamwagiza kwamba: Mkubwa wangu Esau atakapokutana na wewe na kukuuliza kwamba: Wewe mtu wa nani? Unakwenda wapi? Nao hao nyama, wanaowatanguliza, ni wa nani? 18Umwambie: Ni wa mtumishi wako Yakobo, ndio matunzo, anayomtumia bwana wangu Esau, naye mwenyewe anatufuata nyuma. 19Naye wa pili na wa tatu nao wote waliowafuata watumwa hawa akawaagiza kwamba: Mtakapomwona Esau mwambieni maneno yayo hayo! 20Kisha semeni nanyi: Naye mtumishi wako Yakobo anatufuata nyuma. Kwani alisema moyoni mwake: Nitaupoza uso wake kwa hayo matunzo yatakayonitangulia; nitakapoonana naye halafu, labda atanipokea vema. 21Kwa hiyo matunzo yakamtangulia, naye akalala usiku huo humo kambini.
Yakobo anashindana na malaika.
22Usiku huo alipoamka akawachukua wakeze wawili na wale vijakazi wawili na wanawe kumi na mmoja, akaenda kuvuka kivukoni kwa Yakobo; 23akawachukua, akawavusha hapo mtoni, akayavusha nayo yote, aliyokuwaa nayo. 24Naye Yakobo mwenyewe akasalia peke yake ng'ambo ya huko. Mara mtu akakamatana naye, mpaka jua lilipopambazuka.#Hos. 12:4-5. 25Alipoona, ya kuwa hamshindi Yakobo, akamgusa nyonga ya kiuno chake; ndipo, nyonga ya kiuno cha Yakobo ilipoteuka kwa kukamatana naye. 26Akamwambia Yakobo: Niache, niende zangu! Kwani jua limepambazuka. Lakini akasema: Sitakuacha, usiponibariki.#Mat. 15:22-28.
Yakobo anaitwa Isiraeli.
27Naye akamwuliza: Jina lako nani? Akasema: Yakobo.#1 Mose 35:10. 28Ndipo, aliposema: Hutaitwa tena jina lako Yakobo, ila Isiraeli (Mshinda Mungu), kwani umeshindana na Mungu, hata na watu, ukawashinda. 29Naye Yakobo akamwuliza kwamba: Niambie jina lako! Akamwambia: Jina langu unaliulizia nini? Kisha akambariki hapo.#Amu. 13:17-18. 30Yakobo akapaita mahali pale Penieli (Uso wa Mungu) kwamba: Nimeonana na Mungu uso kwa uso, nayo roho yangu ikapona.#2 Mose 33:20. 31Alipovuka hapo Penieli, usiku ukamchea, naye alikuwa akichechemea kwa ajili ya kiuno chake.
32Kwa sababu hii wana wa Isiraeli hawali mshipa ulio juu ya nyonga ya kiuno mpaka siku hii ya leo, kwani yule aliigusa nyonga ya kiuno cha Yakobo penye mshipa wa kiuno.
Kasalukuyang Napili:
1 Mose 32: SRB37
Haylayt
Ibahagi
Kopyahin

Gusto mo bang ma-save ang iyong mga hinaylayt sa lahat ng iyong device? Mag-sign up o mag-sign in
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.