Luka 1
1
Luka Aandika Kuhusu Maisha ya Yesu
1Mheshimiwa Theofilo:#1:1 Theofilo Theofilo ndiye aliyemdhamini Luka katika mradi wa utafiti na uandishi wa kitabu hiki na kingine (Matendo ya Mitume). Ijapokuwa ni kama aliandikiwa yeye, makusudi ya mwandishi na Roho Mtakatifu ni kuwa watu wote wakisome. Theofilo maana yake ni “Mpendwa wa Mungu”.
Watu wengine wengi wamejaribu kuandika juu ya mambo yaliyotokea katikati yetu ili kuukamilisha mpango wa Mungu. 2Mambo hayo waliyoyaandika yanalingana na yale tuliyosikia kutoka kwa watu walioyaona tangu mwanzo. Na walimtumikia Mungu kwa kuwaambia wengine ujumbe wake. 3Nimechunguza kila kitu kwa makini tangu mwanzo. Na nimeona kuwa ni vyema nikuandikie kwa mpangilio mzuri. 4Nimefanya hivi ili uwe na uhakika kuwa yale uliyofundishwa ni ya kweli.
Malaika Amjulisha Zakaria Kuhusu Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
5Herode alipokuwa mfalme wa Uyahudi, alikuwepo kuhani mmoja aliyeitwa Zakaria, aliyekuwa mmoja wa makuhani wa kikundi#1:5 makuhani wa kikundi Makuhani wa Kiyahudi waligawanywa katika vikundi 24. Tazama 1 Mambo ya Nyakati sura ya 24. Vikundi hivi 24 vya Makuhani vilihudumu katika Hekalu mjini Yerusalemu kwa zamu (mzunguko). Kila kikundi kilikuwa na zamu kwa wiki nzima, aghalabu wiki mbili kwa mwaka. cha Abiya. Mkewe alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Haruni, na jina lake alikuwa Elizabeti. 6Wote wawili Zakaria na Elizabeti walikuwa wema waliompendeza Mungu na daima walifanya yote yaliyoamriwa na Bwana na kila mara walifuata maagizo yake kwa ukamilifu. 7Lakini hawakuwa na watoto kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, na wote wawili walikuwa wazee sana.
8Ilipofika zamu ya kundi la Zakaria kuhudumu Hekaluni, yeye mwenyewe alikuwepo ili kuhudumu kama kuhani mbele za Mungu kwa ajili kundi. 9Makuhani walikuwa wanapiga kura kumchagua mmoja wao atakayeingia katika Hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na Zakaria alichaguliwa wakati huu. 10Wakati wa kufukiza uvumba ulipofika watu wote walikusanyika nje ya Hekalu wakiomba.
11Zakaria akiwa ndani ya Hekalu alitokewa na malaika wa Bwana akiwa amesimama mbele yake upande wa kulia wa madhabahu ya uvumba. 12Zakaria alipomwona malaika aliogopa, na akaingiwa na hofu. 13Lakini Malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria. Mungu amelisikia ombi lako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14Utafurahi sana, na watu wengine wengi watamfurahia pamoja nawe. 15Atakuwa mkuu kwa ajili ya Bwana. Kamwe asinywe mvinyo wala kitu chochote kile kitakachomlewesha. Atajazwa Roho Mtakatifu tangu akiwa tumboni mwa mama yake.
16Naye atawafanya Waisraeli wengi wamrudie Bwana Mungu wao. 17Atamtangulia Bwana ili kuwaandaa watu kuupokea ujio wake. Atakuwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha wazazi na watoto wao na kuwafanya wale wasiomtii Mungu kubadilika na kuanza kumtii Mungu.”
18Zakaria akamwambia malaika, “Nitajuaje kuwa haya unayosema ni ya kweli? Maana mimi ni mzee na mke wangu ana umri mkubwa pia.”
19Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, ambaye daima husimama mbele za Mungu nikiwa tayari. Amenituma kuzungumza nawe na kukujulisha habari hizi njema. 20Sasa sikiliza! Hautaweza kuzungumza mpaka siku ambayo mambo haya yatatokea kwa sababu hukuyaamini yale niliyokwambia. Lakini nilichosema hakika kitatokea.”
21Watu waliokuwa nje ya Hekalu wakimngojea Zakaria walishangaa kwa sababu alikaa kwa muda mrefu ndani ya Hekalu. 22Zakaria alipotoka nje hakuweza kuzungumza nao. Aliwafanyia watu ishara kwa mikono yake. Hivyo watu walitambua kuwa alikuwa ameona maono alipokuwa Hekaluni. 23Zamu ya utumishi wake ilipokwisha alirudi nyumbani.
24Wakati fulani baadaye, Elizabeti, mke wa Zakaria akawa mjamzito. Alikaa katika nyumba yake na hakutoka nje kwa miezi mitano. Alisema, 25“Na sasa, hatimaye Bwana amenisaidia kwa kuniondolea aibu yangu.”
Malaika Atangaza Kuzaliwa kwa Yesu
26-27Mwezi wa sita wa ujauzito wa Elizabeti, Mungu alimtuma malaika Gabrieli kwa msichana mmoja bikira aliyeishi Nazareti, mji wa Galilaya. Msichana huyo alikuwa amechumbiwa na Yusufu mzaliwa katika ukoo wa Daudi. Jina la bikira huyo lilikuwa Mariamu. 28Malaika alimwendea na kusema “Salamu! Bwana yu pamoja nawe; Kwa kuwa neema yake iko juu yako.”
29Lakini, Mariamu alichanganyikiwa kutokana na yale aliyosema malaika. Akajiuliza, “Salamu hii ina maana gani?”
30Malaika akamwambia, “Usiogope Mariamu, kwa kuwa neema ya Mungu iko juu yako. 31Sikiliza! Utapata mimba na kuzaa mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yesu. 32Mtoto huyo atakuwa Mkuu na watu watamwita Mwana wa Mungu Aliye Mkuu Sana na Bwana Mungu atamfanya kuwa mfalme kama Daudi baba yake. 33Naye ataitawala nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
34Mariamu akamwambia malaika, “Jambo hili litatokeaje? Kwa maana mimi bado ni bikira.”
35Malaika akamwambia Mariamu, “Roho Mtakatifu atakujia, na nguvu zake Mungu Mkuu zitakufunika. Na hivyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu na ataitwa Mwana wa Mungu. 36Pia sikiliza hili: Jamaa yako Elizabeti ni mjamzito. Ijapokuwa ni mzee sana, atazaa mtoto wa kiume. Kila mtu alidhani hataweza kuzaa, lakini sasa huu ni mwezi wa sita wa ujauzito wake. 37Mungu anaweza kufanya jambo lolote!”
38Mariamu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, basi jambo hili litokee kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka.
Mariamu Amtembelea Elizabeti
39Mariamu akajiandaa na kwenda haraka katika mji mmoja ulio vilimani katika jimbo la Yuda. 40Alikwenda nyumbani kwa Zakaria, alipofika akamsalimu Elizabeti. 41Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akirukaruka, na Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu.
42Kisha akapaza sauti na kumwambia Mariamu, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43Lakini jambo hili kuu limetokeaje kwangu, hata mama wa Bwana wangu aje kwangu? 44Kwa maana sauti ya salamu yako ilipofika masikioni mwangu, mtoto aliye ndani yangu amerukaruka kwa furaha. 45Umebarikiwa wewe uliyeamini kuwa mambo aliyokuambia Bwana yatatokea.”
Mariamu Amsifu Mungu
46Mariamu akasema,
“Moyo wangu unamwadhimisha Bwana,
47kwa maana, Yeye, Mungu na Mwokozi
wangu amenipa furaha kuu!
48Kwa maana ameonesha kunijali,
mimi mtumishi wake, nisiye kitu.
Na kuanzia sasa watu wote
wataniita mbarikiwa.
49Kwa kuwa Mwenye Nguvu amenitendea mambo makuu.
Jina lake ni takatifu.
50Na huwapa rehema zake wale wamchao,
kutoka kizazi hadi kizazi.
51Ameonesha nguvu ya mkono wake;
Amewatawanya wanaojikweza.
52Amewaangusha watawala kutoka katika viti vyao vya enzi,
na kuwakweza wanyenyekevu.
53Amewashibisha wenye njaa kwa mambo mema,
na amewatawanya matajiri bila ya kuwapa kitu.
54Amemsaidia Israeli, watu aliowachagua ili wamtumikie.
Amekumbuka kuonesha rehema;
55Maana ndivyo alivyowaahidi baba zetu,
Abrahamu na wazaliwa wake.”
56Mariamu alikaa na Elizabeti kwa muda wa kama miezi mitatu, kisha alirudi nyumbani kwake.
Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
57Wakati ulipotimia kwa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. 58Majirani na jamaa zake waliposikia jinsi Bwana alivyokuwa mwema kwake, walifurahi pamoja naye.
59Mtoto alipofikisha umri wa siku nane, walikuja kumtahiri.#1:59 kumtahiri Yaani, kumfanyia tohara kama ilivyokuwa katika sheria ya Musa. Walipotaka kumwita mtoto Zakaria kutokana na jina la baba yake. 60Mama yake akasema, “Hapana, mtoto ataitwa Yohana.”
61Lakini wao wakamwambia, “Hakuna jamaa yako hata mmoja mwenye jina hilo.” 62Ndipo wakamfanyia ishara baba yake wakimwuliza jina alilotaka kumpa mtoto.
63Zakaria akataka ubao wa kuandikia,#1:63 ubao wa kuandikia Ni ubao uliokuwa umepakwa nta au mpira ili usiloe. Kisha akaandika, “Jina lake ni Yohana.” Wote wakashangaa. 64Mara hiyo hiyo mdomo wake ulifunguliwa na ulimi wake ukaachia, akaanza kuzungumza na kumsifu Mungu. 65Majirani zao wakajawa hofu na watu katika sehemu zote za vilima katika jimbo la Yuda wakawa wanazungumza kuhusu jambo hili. 66Watu wote waliosikia kuhusu mambo haya walijiuliza, wakisema, “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” Kwa kuwa nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
Zakaria Amsifu Mungu
67Kisha Zakaria, baba yake Yohana, akajaa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema:
68“Asifiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amekuja kuwasaidia
watu wake na kuwaweka huru.
69Na ametuletea sisi Mwokozi Mwenye Nguvu,
kutoka katika ukoo wa mtumishi wake Daudi.
70Hivi ndivyo alivyoahidi
kupitia manabii wake watakatifu tangu zamani.
71Aliahidi kwa Agano kuwa atatuokoa na adui zetu
na milki za wote wanaotuchukia.
72Ili kuonesha rehema kwa baba zetu,
na kulikumbuka agano lake takatifu aliloagana nao.
73Agano hili ni kiapo alichomwapia
baba yetu Abrahamu.
74Alipoahidi kutuokoa kutoka katika nguvu za adui zetu,
ili tuweze kumwabudu Yeye bila hofu.
75Katika namna iliyo takatifu na yenye haki
mbele zake siku zote za maisha yetu.
76Sasa wewe, mtoto mdogo,
utaitwa nabii wa Mungu Aliye Juu Sana,
kwa sababu utamtangulia Bwana
kuandaa njia yake.
77Utawaambia watu wake kwamba wataokolewa
kwa kusamehewa dhambi zao.
78Kwa rehema ya upendo wa Mungu wetu,
siku mpya#1:78 siku mpya Kwa maana ya kawaida, “Alfajiri”, imetumika hapa kama ishara ikimaanisha Masihi, Bwana. itachomoza juu yetu kutoka mbinguni.
79Kuwaangazia wale wanaoishi katika giza,
kwa hofu ya mauti,
na kuongoza hatua zetu
katika njia ya amani.”
80Na hivyo mtoto Yohana akakua na kuwa na nguvu katika roho. Kisha akaishi maeneo yasiyo na watu mpaka wakati alipotokea hadharani akihubiri ujumbe wa Mungu kwa watu wa Israeli.
ప్రస్తుతం ఎంపిక చేయబడింది:
Luka 1: TKU
హైలైట్
షేర్ చేయి
కాపీ

మీ పరికరాలన్నింటి వ్యాప్తంగా మీ హైలైట్స్ సేవ్ చేయబడాలనుకుంటున్నారా? సైన్ అప్ చేయండి లేదా సైన్ ఇన్ చేయండి
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International