Soma Biblia Kila Siku Agosti 2021Mfano
Kwanza Mungu anaagiza juu ya utakaso wa hekalu kwa mujibu wa sheria za Musa: Bwana MUNGU asema hivi; Mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, utatwaa ng'ombe mchanga mume mkamilifu; nawe utapatakasa mahali patakatifu ... Tena, katika zile siku saba za sikukuu atamtengenezea Bwana sadaka ya kuteketezwa, ng'ombe saba na kondoo waume saba wakamilifu, kila siku kwa muda wa siku saba, na beberu mmoja kila siku kuwa sadaka ya dhambi (45:18 na 23; linganisha na neno kuhusu kuhani mkuu katika Law 16:16, Atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao). Lengo kuu ni watu kurudi kwenye ibada takatifu za kumwabudu Mungu. Neno hili linatukumbusha hata sisi wa agano jipya kuhusu haja ya kumwabudu Mungu kwenye msingi wa upatanisho. Hatuhitaji mlolongo wa mifugo ili ichinjwe na damu yake itumike kwa utakaso. Kitendo cha Yesu kufa msalabani ni msingi huo wa upatanisho. Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele (Ebr 9:11-12). Matokeo yake tunayasoma katika Ebr 10:19-25, Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi. Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu; tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.
Andiko
Kuhusu Mpango huu
Soma Biblia Kila Siku Agosti 2021 ni mpango mzuri wa kusoma Biblia kila siku sehemu kwa sehemu hasa katika kitabu cha Wakolosai, Marko na Ezekieli. Mpango huu una maelezo mafupi yatakayokusaidia kuelewa zaidi Neno la Mungu. Karibu kujiunga na mpango huu
More
Tungependa kuishukuru Soma Biblia kwa kutoa mpango huu. Kwa habari zaidi, tafadhali tembelea: http://www.somabiblia.or.tz