Zekaria 8:1-8
Zekaria 8:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi likanijia mimi Zekaria: “Ninawaka upendo mkuu kwa ajili ya Siyoni, na ninawaka ghadhabu nyingi dhidi ya adui zake. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema hayo. Nitaurudia mji wa Siyoni na kufanya makao yangu mjini Yerusalemu. Mji wa Yerusalemu utaitwa ‘Mji Mwaminifu,’ na mlima wangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, utaitwa ‘Mlima Mtakatifu.’ Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Wazee, wanaume kwa wanawake, wataonekana tena wamekaa kwenye barabara za Yerusalemu, kila mmoja na mkongojo wake kwa sababu ya kuishi miaka mingi. Barabara za Yerusalemu zitajaa wavulana na wasichana, wakichezacheza humo. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Kwa watu hawa waliosalia, hali hii inaonekana kuwa kitu kisichowezekana; lakini mnadhani haiwezekani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi? Nitawaokoa watu wangu kutoka nchi ya mashariki na kutoka nchi ya magharibi na kuwafanya wakae katika mji wa Yerusalemu. Wao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; nitatawala juu yao kwa uaminifu na haki.”
Zekaria 8:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA wa majeshi likanijia, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu. BWANA asema hivi, Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji mwaminifu; na mlima wa BWANA wa majeshi utaitwa, mlima mtakatifu. BWANA wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu akiwa ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana. Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake. BWANA wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawa katika siku hizo, je, litakuwa neno gumu mbele ya macho yangu? Asema BWANA wa majeshi. BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi; nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.
Zekaria 8:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA wa majeshi likanijia, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu. BWANA asema hivi, Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji wa kweli; na Mlima wa BWANA wa majeshi utaitwa, Mlima mtakatifu. BWANA wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana. Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake. BWANA wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawa katika siku hizo, je! Liwe neno gumu mbele ya macho yangu? Asema BWANA wa majeshi. BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi; nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.
Zekaria 8:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Neno la BWANA Mwenye Nguvu Zote likanijia tena. Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Nina wivu sana kwa ajili ya Sayuni, ninawaka wivu kwa ajili yake.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Nitarudi Sayuni na kufanya makao Yerusalemu. Kisha Yerusalemu utaitwa mji wa kweli, mlima wa BWANA Mwenye Nguvu Zote utaitwa Mlima Mtakatifu.” Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Kwa mara nyingine tena wazee wanaume kwa wanawake walioshiba umri wataketi katika barabara za Yerusalemu, kila mmoja akiwa na mkongojo wake mkononi kwa sababu ya umri wake. Barabara za mji zitajaa wavulana na wasichana wanaocheza humo.” Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Mambo haya yanaweza kuonekana ya ajabu kwa mabaki ya watu wakati huo, lakini yaweza kuwa ya ajabu kwangu?” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Nitawaokoa watu wangu kutoka nchi za mashariki na magharibi. Nitawarudisha waje kuishi Yerusalemu, watakuwa watu wangu nami nitakuwa mwaminifu na wa haki kwao kama Mungu wao.”