Waroma 7:1-3
Waroma 7:1-3 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu zangu, bila shaka mtaelewa yafuatayo, maana ninawazungumzia watu wanaojua sheria. Sheria humtawala mtu wakati akiwa hai. Mathalani: Mwanamke aliyeolewa anafungwa na sheria muda wote mumewe anapokuwa hai; lakini mumewe akifa, hiyo sheria haimtawali tena huyo mwanamke. Hivyo mwanamke huyo akiishi na mwanamume mwingine wakati mumewe yungali hai, ataitwa mzinzi; lakini mumewe akifa, mwanamke huyo yu huru kisheria, na akiolewa na mwanamume mwingine, yeye si mzinzi.
Waroma 7:1-3 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai? Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali yule mume akifa, amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati mumewe awapo hai, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine.
Waroma 7:1-3 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai? Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine.
Waroma 7:1-3 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ndugu zangu, sasa ninasema na wale wanaoijua Torati: Je, hamjui kwamba Torati ina mamlaka juu ya mtu wakati akiwa hai tu? Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa. Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.