Warumi 7
7
Kufunguliwa kutoka kwa Torati
1Ndugu zangu, sasa ninasema na wale wanaoijua Torati: Je, hamjui kwamba Torati ina mamlaka juu ya mtu wakati akiwa hai tu? 2Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa. 3Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.
4Vivyo hivyo, ndugu zangu, ninyi mmeifia Torati kupitia kwa mwili wa Al-Masihi, ili mweze kuwa mali ya mwingine, yeye ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu, ili tupate kuzaa matunda kwa Mungu. 5Kwa maana tulipokuwa tunatawaliwa na asili ya dhambi, tamaa za dhambi zilizochochewa na Torati zilikuwa zikitenda kazi katika miili yetu, hivyo tulizaa matunda ya mauti. 6Lakini sasa, kwa kufia kile kilichokuwa kimetufunga kwanza, tumewekwa huru kutokana na Torati ili tutumike katika njia mpya ya Roho wa Mungu, wala si katika njia ya zamani ya Torati iliyoandikwa.
Torati na dhambi
7Tuseme nini basi? Kwamba Torati ni dhambi? La, hasha! Lakini singejua dhambi isipokuwa kwa sababu ya Torati. Singejua kutamani ni nini kama Torati haikusema, “Usitamani.”#7:7 Kutoka 20:17; Kumbukumbu 5:21 8Lakini dhambi ilipata nafasi katika amri, nayo ikazaa kila aina ya tamaa ndani yangu. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa. 9Mwanzoni nilikuwa hai pasipo sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ikawa hai, nami nikafa. 10Nikaona kwamba ile amri iliyokusudiwa kuleta uzima, ilileta mauti. 11Kwa maana dhambi kwa kupata nafasi katika amri, ilinidanganya, na kupitia katika hiyo amri, ikaniua. 12Hivyo basi, Torati yenyewe ni takatifu, na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema.
13Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kupitia kwa amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi.
Mgongano wa ndani
14Kwa maana tunajua kwamba Torati ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi. 15Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia. 16Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa Torati ni njema. 17Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu. 18Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote linalokaa ndani yangu, yaani katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda. 19Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo. 20Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu.
21Hivyo naiona Torati ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo. 22Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia Torati ya Mungu. 23Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu. 24Ole wangu, mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
25Namshukuru Mungu anayeniokoa kupitia kwa Isa Al-Masihi Bwana wetu!
Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa Torati ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.
Iliyochaguliwa sasa
Warumi 7: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.