Waroma 14:1-9
Waroma 14:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye juu ya mawazo yake binafsi. Watu hutofautiana: Mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu; lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani. Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kila kitu; naye ambaye hula tu mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu, maana Mungu amemkubali. Wewe ni nani hata uthubutu kumhukumu mtumishi wa mwingine? Akisimama au akianguka ni shauri la Bwana wake; naam, atasimama imara, maana Bwana anaweza kumsimamisha. Mtu anaweza kufikiria siku fulani kuwa ya maana zaidi kuliko nyingine; mtu mwingine aweza kuzifikiria siku zote kuwa sawa. Kila mmoja na afuate msimamo wa akili yake. Anayeadhimisha siku fulani anaadhimisha siku hiyo kwa ajili ya kumtukuza Mungu; naye anayekula chakula fulani anafanya hivyo kwa kumtukuza Bwana maana anamshukuru Mungu. Kadhalika naye anayeacha kula chakula fulani anafanya hivyo kwa ajili ya kumtukuza Bwana, naye pia anamshukuru Mungu. Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana. Maana Kristo alikufa, akafufuka ili apate kuwa Bwana wa walio hai na wafu.
Waroma 14:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, lakini msimhukumu mawazo yake. Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga. Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali. Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia.
Waroma 14:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake. Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga. Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali. Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia.
Waroma 14:1-9 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu. Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali. Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha. Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini. Yeye anayehesabu siku moja kuwa takatifu kuliko nyingine, hufanya hivyo kwa kumheshimu Mwenyezi Mungu. Naye alaye nyama hula kwa Mwenyezi Mungu, kwa maana humshukuru Mungu, naye akataaye kula nyama hufanya hivyo kwa Mwenyezi Mungu na humshukuru Mungu. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe. Kama tunaishi, tunaishi kwa Mwenyezi Mungu, nasi pia tukifa tunakufa kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Mwenyezi Mungu. Kwani kwa sababu hii hasa, Al-Masihi alikufa na akawa hai tena kusudi apate kuwa Bwana wa wote, yaani waliokufa na walio hai.