Waroma 14:1-23
Waroma 14:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye juu ya mawazo yake binafsi. Watu hutofautiana: Mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu; lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani. Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kila kitu; naye ambaye hula tu mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu, maana Mungu amemkubali. Wewe ni nani hata uthubutu kumhukumu mtumishi wa mwingine? Akisimama au akianguka ni shauri la Bwana wake; naam, atasimama imara, maana Bwana anaweza kumsimamisha. Mtu anaweza kufikiria siku fulani kuwa ya maana zaidi kuliko nyingine; mtu mwingine aweza kuzifikiria siku zote kuwa sawa. Kila mmoja na afuate msimamo wa akili yake. Anayeadhimisha siku fulani anaadhimisha siku hiyo kwa ajili ya kumtukuza Mungu; naye anayekula chakula fulani anafanya hivyo kwa kumtukuza Bwana maana anamshukuru Mungu. Kadhalika naye anayeacha kula chakula fulani anafanya hivyo kwa ajili ya kumtukuza Bwana, naye pia anamshukuru Mungu. Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana. Maana Kristo alikufa, akafufuka ili apate kuwa Bwana wa walio hai na wafu. Kwa nini basi, wewe wamhukumu ndugu yako? Nawe, kwa nini wamdharau ndugu yako? Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Maana Maandiko yanasema: “Kama niishivyo, asema Bwana, kila mtu atanipigia magoti, na kila mmoja atakiri kwamba mimi ni Mungu.” Kwa hiyo, kila mmoja wetu atatoa hoja juu yake mwenyewe mbele ya Mungu. Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe kikwazo kwa ndugu au kumsababisha aanguke katika dhambi. Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi. Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na upendo. Usikubali hata kidogo chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake! Basi, msikubali kitu mnachokiona kwenu kuwa chema kidharauliwe. Maana ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu. Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na kukubaliwa na watu. Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na yanayotusaidia kujengana. Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho kitamfanya mtu aanguke katika dhambi. Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke. Basi, shikilia unachoamini kati yako na Mungu wako. Heri mtu yule ambaye, katika kujiamulia la kufanya, haipingi dhamiri yake. Lakini mtu anayeona shaka juu ya chakula anachokula, anahukumiwa kama akila, kwa sababu msimamo wa kitendo chake haumo katika imani. Na, chochote kisicho na msingi wake katika imani ni dhambi.
Waroma 14:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, lakini msimhukumu mawazo yake. Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga. Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali. Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu. Basi tusiendelee kuhukumiana, bali amueni kuwa mtu asifanye kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha. Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi. Na ndugu yako akichukizwa kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Basi, huo wema wenu usitajwe kwa ubaya. Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Kwa kuwa yeye amtumikiaye Kristo katika mambo hayo humpendeza Mungu, tena hukubaliwa na wanadamu. Basi kama ni hivyo, na mfuate mambo ya amani na mambo yafaayo kwa kujengana. Kwa ajili ya chakula usiiharibu kazi ya Mungu. Kweli, vyote ni safi; bali ni vibaya kwa mtu alaye na kujikwaza. Ni vyema kutokula nyama wala kunywa divai wala kutenda neno lolote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa. Ile imani uliyo nayo uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiyejihukumu nafsi yake katika neno lile analolikubali. Lakini aliye na mashaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.
Waroma 14:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake. Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga. Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali. Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu. Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha. Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi. Na ndugu yako akiingia huzuni kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Basi, huo wema wenu usitajwe kwa ubaya. Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Kwa kuwa yeye amtumikiaye Kristo katika mambo hayo humpendeza Mungu, tena hukubaliwa na wanadamu. Basi kama ni hivyo, na mfuate mambo ya amani na mambo yafaayo kwa kujengana. Kwa ajili ya chakula usiiharibu kazi ya Mungu. Kweli, vyote ni safi; bali ni vibaya kwa mtu alaye na kujikwaza. Ni vyema kutokula nyama wala kunywa divai wala kutenda neno lo lote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa. Ile imani uliyo nayo uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiyejihukumu nafsi yake katika neno lile analolikubali. Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.
Waroma 14:1-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu. Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali. Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha. Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini. Yeye anayehesabu siku moja kuwa takatifu kuliko nyingine, hufanya hivyo kwa kumheshimu Bwana. Naye alaye nyama hula kwa Bwana, kwa maana humshukuru Mungu, naye akataaye kula nyama hufanya hivyo kwa Bwana na humshukuru Mungu. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe. Kama tunaishi, tunaishi kwa Bwana, nasi pia tukifa tunakufa kwa Bwana. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Bwana. Kwani kwa sababu hii hasa, Kristo alikufa na akawa hai tena kusudi apate kuwa Bwana wa wote, yaani, waliokufa na walio hai. Basi kwa nini wewe wamhukumu ndugu yako? Au kwa nini wewe unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sote tutasimama mbele ya kiti cha Mungu cha hukumu. Kwa kuwa imeandikwa: “ ‘Kama vile niishivyo,’ asema Bwana, ‘kila goti litapigwa mbele zangu, na kila ulimi utakiri kwa Mungu.’ ” Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu. Kwa hiyo tusiendelee kuhukumiana: Badala yake mtu asiweke kamwe kikwazo au kizuizi katika njia ya ndugu mwingine. Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Yesu kwamba hakuna kitu chochote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi. Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Usiruhusu kile ambacho unakiona kuwa chema kisemwe kuwa ni kiovu. Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Kwa sababu mtu yeyote anayemtumikia Kristo kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu. Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi. Usiiharibu kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula. Hakika vyakula vyote ni safi, lakini ni kosa kula kitu chochote kinachomsababisha ndugu yako ajikwae. Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lolote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae. Je, wewe unayo imani? Ile imani uliyo nayo, uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiye na sababu ya kujihukumu nafsi yake kwa ajili ya kile anachokifanya. Lakini kama mtu ana shaka kuhusu kile anachokula, amehukumiwa, kwa sababu hakula kwa imani. Kwa kuwa chochote kinachofanywa pasipo imani ni dhambi.