Waroma 14:1-23
Waroma 14:1-23 BHN
Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye juu ya mawazo yake binafsi. Watu hutofautiana: Mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu; lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani. Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kila kitu; naye ambaye hula tu mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu, maana Mungu amemkubali. Wewe ni nani hata uthubutu kumhukumu mtumishi wa mwingine? Akisimama au akianguka ni shauri la Bwana wake; naam, atasimama imara, maana Bwana anaweza kumsimamisha. Mtu anaweza kufikiria siku fulani kuwa ya maana zaidi kuliko nyingine; mtu mwingine aweza kuzifikiria siku zote kuwa sawa. Kila mmoja na afuate msimamo wa akili yake. Anayeadhimisha siku fulani anaadhimisha siku hiyo kwa ajili ya kumtukuza Mungu; naye anayekula chakula fulani anafanya hivyo kwa kumtukuza Bwana maana anamshukuru Mungu. Kadhalika naye anayeacha kula chakula fulani anafanya hivyo kwa ajili ya kumtukuza Bwana, naye pia anamshukuru Mungu. Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana. Maana Kristo alikufa, akafufuka ili apate kuwa Bwana wa walio hai na wafu. Kwa nini basi, wewe wamhukumu ndugu yako? Nawe, kwa nini wamdharau ndugu yako? Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Maana Maandiko yanasema: “Kama niishivyo, asema Bwana, kila mtu atanipigia magoti, na kila mmoja atakiri kwamba mimi ni Mungu.” Kwa hiyo, kila mmoja wetu atatoa hoja juu yake mwenyewe mbele ya Mungu. Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe kikwazo kwa ndugu au kumsababisha aanguke katika dhambi. Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi. Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na upendo. Usikubali hata kidogo chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake! Basi, msikubali kitu mnachokiona kwenu kuwa chema kidharauliwe. Maana ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu. Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na kukubaliwa na watu. Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na yanayotusaidia kujengana. Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho kitamfanya mtu aanguke katika dhambi. Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke. Basi, shikilia unachoamini kati yako na Mungu wako. Heri mtu yule ambaye, katika kujiamulia la kufanya, haipingi dhamiri yake. Lakini mtu anayeona shaka juu ya chakula anachokula, anahukumiwa kama akila, kwa sababu msimamo wa kitendo chake haumo katika imani. Na, chochote kisicho na msingi wake katika imani ni dhambi.