Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 11:1-14

Ufunuo 11:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, na madhabahu, na hao wanaosujudu humo. Na behewa lililo nje ya hekalu uliache nje wala usilipime, kwa maana Mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arubaini na miwili. Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, wakiwa wamevikwa magunia. Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi. Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa. Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo. Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua. Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulubiwa. Na watu wa hao jamaa na kabila na lugha na taifa waitazama mizoga yao siku tatu u nusu, wala hawaiachi mizoga yao kuwekwa kaburini. Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi. Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama kwa miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama. Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama. Na katika saa ile palikuwa na tetemeko kuu la nchi, na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka; wanadamu elfu saba wakauawa katika tetemeko lile. Na waliobakia wakaingiwa na hofu, wakamtukuza Mungu wa mbingu. Ole wao, pigo la pili limekwisha pita, tazama pigo la tatu linakuja punde.

Shirikisha
Soma Ufunuo 11

Ufunuo 11:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha nikapewa mwanzi uliokuwa kama kijiti cha kupimia, nikaambiwa, “Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, madhabahu ya kufukizia ubani na kawahesabu watu wanaoabudu ndani ya hekalu. Lakini uache ukumbi ulio nje ya hekalu; usiupime, maana huo umekabidhiwa watu wa mataifa mengine, ambao wataukanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arubaini na miwili. Nami nitawatuma mashahidi wangu wawili ili watoe unabii kwa muda huo wa siku 1,260, wakiwa wamevaa mavazi ya gunia.” Hao mashahidi wawili ni miti miwili ya mizeituni na taa mbili zinazosimama mbele ya Bwana wa dunia. Kama mtu akijaribu kuwadhuru, moto hutoka kinywani mwao na kuwaangamiza maadui zao; na kila mtu atakayejaribu kuwadhuru atakufa namna hiyo. Hao wanayo mamlaka ya kufunga anga, mvua isinyeshe wakati wanapotoa unabii. Tena wanayo mamlaka ya kuzigeuza chemchemi zote za maji ziwe damu, na ya kusababisha maafa ya kila namna duniani kila mara wanapopenda. Lakini wakisha maliza kutoa unabii huo, mnyama atokaye shimoni kuzimu atapigana nao, atawashinda na kuwaua. Maiti zao zitabaki katika barabara za mji mkuu ambapo Bwana wao alisulubiwa. Jina la kupanga la mji huo ni Sodoma au Misri. Watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti hizo kwa muda wa siku tatu na nusu, na hawataruhusu zizikwe. Watu waishio duniani watafurahia kifo cha hao wawili. Watafanya sherehe na kupelekeana zawadi, maana manabii hawa wawili walikuwa wamewasumbua mno watu wa dunia. Lakini baada ya zile siku tatu na nusu pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu. Kisha, hao manabii wawili wakasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njoni hapa juu!” Nao wakapanda juu mbinguni katika wingu, maadui zao wakiwa wanawatazama. Wakati huohuo, kukatokea tetemeko kubwa la ardhi, sehemu moja ya kumi ya ardhi ikaharibiwa. Watu 7,000 wakauawa kwa tetemeko hilo la ardhi. Watu waliosalia wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni. Maafa ya pili yamepita; lakini tazama! Maafa ya tatu yanafuata hima.

Shirikisha
Soma Ufunuo 11

Ufunuo 11:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, na madhabahu, na hao wasujuduo humo. Na behewa iliyo nje ya hekalu uiache nje wala usiipime, kwa maana Mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili. Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia. Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi. Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa. Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo. Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua. Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulibiwa. Na watu wa hao jamaa na kabila na lugha na taifa waitazama mizoga yao siku tatu u nusu, wala hawaiachi mizoga yao kuwekwa kaburini. Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi. Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama. Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama. Na katika saa ile palikuwa na tetemeko kuu la nchi, na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka; wanadamu elfu saba wakauawa katika tetemeko lile. Na waliosalia wakaingiwa na hofu, wakamtukuza Mungu wa mbingu. Ole wa pili umekwisha pita, tazama ole wa tatu unakuja upesi.

Shirikisha
Soma Ufunuo 11

Ufunuo 11:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo nikapewa mwanzi uliokuwa kama ufito wa kupimia, nikaambiwa, “Nenda ukapime hekalu la Mungu pamoja na madhabahu, nawe uwahesabu wale waabuduo humo. Lakini usiupime ua wa nje wa Hekalu, uache, kwa sababu ua huo wamepewa watu wa Mataifa. Hao wataukanyagakanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili. Nami nitawapa mashahidi wangu wawili uwezo, nao watoe unabii kwa muda wa siku 1,260, wakiwa wamevaa nguo za gunia.” Hawa ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili vya taa visimamavyo mbele za Bwana Mungu wa dunia yote. Kama mtu yeyote akitaka kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwateketeza adui zao. Hivi ndivyo impasavyo kufa mtu yeyote atakayetaka kuwadhuru. Watu hawa wanao uwezo wa kufunga anga ili mvua isinyeshe wakati wote watakapokuwa wanatoa unabii wao. Nao watakuwa na uwezo wa kuyabadili maji kuwa damu na kuipiga dunia kwa kila aina ya mapigo mara kwa mara kama watakavyo. Basi watakapokuwa wamemaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika lile Shimo atapigana nao vita, atawashinda na kuwaua. Maiti zao zitabaki katika barabara ya mji mkubwa, ambao kwa fumbo unaitwa Sodoma na Misri, ambapo pia Bwana wao alisulubiwa. Kwa muda wa siku tatu na nusu, watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa wataziangalia hizo maiti zao na hawataruhusu wazikwe. Watu waishio duniani watazitazama kwa furaha maiti za hao manabii wawili na kushangilia kwa kupeana zawadi kwa sababu hao manabii waliwatesa watu waishio duniani. Lakini baada ya zile siku tatu na nusu, pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu ikawaingia, nao wakasimama kwa miguu yao na wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu. Kisha wale manabii wawili wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njooni huku juu!” Nao wakapaa mbinguni katika wingu, wakati adui zao wakiwa wanawatazama. Saa iyo hiyo, kukatokea tetemeko kubwa la nchi na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka. Watu elfu saba wakauawa katika tetemeko hilo, nao walionusurika wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni. Ole ya pili imekwisha kupita, tazama ole ya tatu inakuja upesi.

Shirikisha
Soma Ufunuo 11