Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 11:1-14

Ufunuo 11:1-14 BHN

Kisha nikapewa mwanzi uliokuwa kama kijiti cha kupimia, nikaambiwa, “Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, madhabahu ya kufukizia ubani na kawahesabu watu wanaoabudu ndani ya hekalu. Lakini uache ukumbi ulio nje ya hekalu; usiupime, maana huo umekabidhiwa watu wa mataifa mengine, ambao wataukanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arubaini na miwili. Nami nitawatuma mashahidi wangu wawili ili watoe unabii kwa muda huo wa siku 1,260, wakiwa wamevaa mavazi ya gunia.” Hao mashahidi wawili ni miti miwili ya mizeituni na taa mbili zinazosimama mbele ya Bwana wa dunia. Kama mtu akijaribu kuwadhuru, moto hutoka kinywani mwao na kuwaangamiza maadui zao; na kila mtu atakayejaribu kuwadhuru atakufa namna hiyo. Hao wanayo mamlaka ya kufunga anga, mvua isinyeshe wakati wanapotoa unabii. Tena wanayo mamlaka ya kuzigeuza chemchemi zote za maji ziwe damu, na ya kusababisha maafa ya kila namna duniani kila mara wanapopenda. Lakini wakisha maliza kutoa unabii huo, mnyama atokaye shimoni kuzimu atapigana nao, atawashinda na kuwaua. Maiti zao zitabaki katika barabara za mji mkuu ambapo Bwana wao alisulubiwa. Jina la kupanga la mji huo ni Sodoma au Misri. Watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti hizo kwa muda wa siku tatu na nusu, na hawataruhusu zizikwe. Watu waishio duniani watafurahia kifo cha hao wawili. Watafanya sherehe na kupelekeana zawadi, maana manabii hawa wawili walikuwa wamewasumbua mno watu wa dunia. Lakini baada ya zile siku tatu na nusu pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu. Kisha, hao manabii wawili wakasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njoni hapa juu!” Nao wakapanda juu mbinguni katika wingu, maadui zao wakiwa wanawatazama. Wakati huohuo, kukatokea tetemeko kubwa la ardhi, sehemu moja ya kumi ya ardhi ikaharibiwa. Watu 7,000 wakauawa kwa tetemeko hilo la ardhi. Watu waliosalia wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni. Maafa ya pili yamepita; lakini tazama! Maafa ya tatu yanafuata hima.