Zaburi 98:1-9
Zaburi 98:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu! Mkono wake hodari, mkono wake mtakatifu umempatia ushindi. Mwenyezi-Mungu ameonesha ushindi wake; ameyadhihirishia mataifa uwezo wake wa kuokoa. Amekumbuka fadhili na uaminifu wake kwa Waisraeli. Pande zote za dunia zimeuona ushindi wa Mungu wetu. Dunia yote imshangilie Mwenyezi-Mungu; imsifu kwa nyimbo na vigelegele. Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa shangwe, msifuni kwa sauti tamu za zeze. Mpigieni vigelegele Mwenyezi-Mungu mfalme wetu, mshangilieni kwa tarumbeta na sauti ya baragumu. Bahari na ivume na vyote vilivyomo; dunia na wote waishio ndani yake. Enyi mito pigeni makofi; enyi vilima imbeni pamoja kwa shangwe. Shangilieni mbele ya Mwenyezi-Mungu, maana anakuja kutawala dunia. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, atawatawala watu kwa uadilifu.
Zaburi 98:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwimbieni BWANA wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kulia, Na mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. BWANA ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake. Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu. Mshangilieni BWANA, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni sifa. Mwimbieni BWANA sifa kwa kinubi, Kwa kinubi na sauti tamu. Kwa panda na sauti ya baragumu. Shangilieni mbele za Mfalme, BWANA. Bahari na ivume na vyote viijazavyo, Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake. Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha. Mbele za BWANA; Kwa maana anakuja kuihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa uaminifu, Na mataifa kwa adili.
Zaburi 98:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwimbieni BWANA wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. BWANA ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake. Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu. Mshangilieni BWANA, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. Mwimbieni BWANA zaburi kwa kinubi, Kwa kinubi na sauti ya zaburi. Kwa panda na sauti ya baragumu. Shangilieni mbele za Mfalme, BWANA. Bahari na ivume na vyote viijazavyo, Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake. Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha. Mbele za BWANA; Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa adili.
Zaburi 98:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mwimbieni BWANA wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu umemfanyia wokovu. BWANA ameufanya wokovu wake ujulikane na amedhihirisha haki yake kwa mataifa. Ameukumbuka upendo wake na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli; miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu. Mpigieni BWANA kelele za shangwe, dunia yote, ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda; mwimbieni BWANA kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za kuimba, kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume: shangilieni kwa furaha mbele za BWANA, aliye Mfalme. Bahari na ivume na kila kiliomo ndani yake, dunia na wote wakaao ndani yake. Mito na ipige makofi, milima na iimbe pamoja kwa furaha, vyote na viimbe mbele za BWANA, kwa maana yuaja kuhukumu dunia. Atahukumu dunia kwa haki na mataifa kwa haki.