Zaburi 95:1-11
Zaburi 95:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Njoni tumwimbie Mwenyezi-Mungu, tumshangilie mwamba wa wokovu wetu! Twende mbele zake na shukrani; tumshangilie kwa nyimbo za sifa. Maana Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mkuu; yeye ni Mfalme mkuu juu ya miungu yote. Vilindi vyote vya dunia vimo mikononi mwake, vilele vya milima ni vyake. Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya; kwa mikono yake aliiumba nchi kavu. Njoni tusujudu na kumwabudu; tumpigie magoti Mwenyezi-Mungu, Muumba wetu! Maana yeye ni Mungu wetu, nasi ni watu wa kundi lake, ni kondoo wake anaowachunga. Laiti leo mngesikiliza sauti yake: “Msiwe wakaidi kama kule Meriba, kama walivyokuwa kule Masa jangwani, wazee wenu waliponijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameona mambo niliyowatendea. Kwa miaka arubaini nilichukizwa nao, nikasema: ‘Kweli, hawa ni watu waliopotoka! Hawajali kabisa njia zangu!’ Basi, nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko!’”
Zaburi 95:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Njoni, tumwimbie BWANA, Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele zake kwa shukrani, Tumfanyie shangwe kwa zaburi. Kwa kuwa BWANA ni Mungu mkuu, Na Mfalme mkuu juu ya miungu yote. Mkononi mwake zimo bonde za dunia, Hata vilele vya milima ni vyake. Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya, Na mikono yake iliumba nchi kavu. Njoni, tuabudu, tusujudu, Tupige magoti mbele za BWANA aliyetuumba. Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu wa malisho yake, Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye mioyo yenu kuwa migumu; Kama ilivyokuwa huko Meriba Kama siku ile katika Masa jangwani. Hapo waliponijaribu baba zenu, Wakanipima, wakayaona matendo yangu. Miaka arubaini nilichukizwa na kizazi kile, Nikasema, Hawa ni watu wenye mioyo inayopotoka, Na wanaopuuza njia zangu. Ndipo Nikaapa kwa hasira yangu Hawataingia katika pumziko langu.
Zaburi 95:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Njoni, tumwimbie BWANA, Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele zake kwa shukrani, Tumfanyie shangwe kwa zaburi. Kwa kuwa BWANA ni Mungu mkuu, Na Mfalme mkuu juu ya miungu yote. Mkononi mwake zimo bonde za dunia, Hata vilele vya milima ni vyake. Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya, Na mikono yake iliumba nchi kavu. Njoni, tuabudu, tusujudu, Tupige magoti mbele za BWANA aliyetuumba. Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu wa malisho yake, Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu; Kama vile huko Meriba Kama siku ya Masa jangwani. Hapo waliponijaribu baba zenu, Wakanipima, wakayaona matendo yangu. Miaka arobaini nalihuzunika na kizazi kile, Nikasema, Hao ni watu waliopotoka mioyo, Hawakuzijua njia zangu. Nikaapa kwa hasira yangu Wasiingie rahani mwangu.
Zaburi 95:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Njooni, tumwimbie BWANA kwa furaha; tumfanyie kelele za shangwe Mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele zake kwa shukrani, tumtukuze kwa vinanda na nyimbo. Kwa kuwa BWANA ni Mungu mkuu, mfalme mkuu juu ya miungu yote. Mkononi mwake mna vilindi vya dunia, na vilele vya milima ni mali yake. Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya, na mikono yake iliumba nchi kavu. Njooni, tusujudu, tumwabudu, tupige magoti mbele za BWANA Muumba wetu, kwa maana yeye ndiye Mungu wetu, na sisi ni watu wa malisho yake, kondoo chini ya utunzaji wake. Kama mkiisikia sauti yake leo, msiifanye mioyo yenu migumu kama mlivyofanya kule Meriba, kama mlivyofanya siku ile kule Masa jangwani, ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu. Kwa miaka arobaini nilikasirikia kizazi kile, nikasema, “Hawa ni taifa ambalo mioyo yao imepotoka, nao hawajazijua njia zangu.” Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”