Zaburi 95:1-11
Zaburi 95:1-11 NEN
Njooni, tumwimbie BWANA kwa furaha; tumfanyie kelele za shangwe Mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele zake kwa shukrani, tumtukuze kwa vinanda na nyimbo. Kwa kuwa BWANA ni Mungu mkuu, mfalme mkuu juu ya miungu yote. Mkononi mwake mna vilindi vya dunia, na vilele vya milima ni mali yake. Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya, na mikono yake iliumba nchi kavu. Njooni, tusujudu, tumwabudu, tupige magoti mbele za BWANA Muumba wetu, kwa maana yeye ndiye Mungu wetu, na sisi ni watu wa malisho yake, kondoo chini ya utunzaji wake. Kama mkiisikia sauti yake leo, msiifanye mioyo yenu migumu kama mlivyofanya kule Meriba, kama mlivyofanya siku ile kule Masa jangwani, ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu. Kwa miaka arobaini nilikasirikia kizazi kile, nikasema, “Hawa ni taifa ambalo mioyo yao imepotoka, nao hawajazijua njia zangu.” Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”