Zaburi 7:6-11
Zaburi 7:6-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Inuka ee Mwenyezi-Mungu, kwa hasira yako, uikabili ghadhabu ya maadui zangu. Inuka, ee Mungu wangu, wewe umeamuru haki ifanyike. Uyakusanye mataifa kandokando yako, nawe uyatawale kutoka juu. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wayahukumu mataifa; unihukumu kadiri ya uadilifu wangu, kulingana na huo unyofu wangu. Uukomeshe uovu wa watu wabaya, uwaimarishe watu walio wema, ee Mungu uliye mwadilifu, uzijuaye siri za mioyo na fikira za watu. Mungu ndiye ngao yangu; yeye huwaokoa wanyofu wa moyo. Mungu ni hakimu wa haki; kila siku hulaumu maovu.
Zaburi 7:6-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA uondoke kwa hasira yako; Ujiinue Juu ya ujeuri wa watesi wangu; Uamke kwa ajili yangu; Umeamuru hukumu. Kusanyiko la mataifa na likuzunguke, Na juu yake uketi utawale. BWANA atawaamua mataifa, BWANA, unihukumu mimi, Kwa kadiri ya haki yangu, Kulingana na unyofu nilio nao. Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na fikira Ndiye Mungu aliye mwenye haki. Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu wa moyo. Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu akasirikiaye waovu kila siku.
Zaburi 7:6-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA uondoke kwa hasira yako; Ujiinue juu ya jeuri ya watesi wangu; Uamke kwa ajili yangu; Umeamuru hukumu. Kusanyiko la mataifa na likuzunguke, Na juu yake uketi utawale. BWANA atawaamua mataifa, BWANA, unihukumu mimi, Kwa kadiri ya haki yangu, Sawasawa na unyofu nilio nao. Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki. Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu wa moyo. Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.
Zaburi 7:6-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Amka kwa hasira yako, Ee BWANA, inuka dhidi ya ghadhabu ya adui zangu. Amka, Mungu wangu, uamue haki. Kusanyiko la watu na likuzunguke. Watawale kutoka juu. BWANA na awahukumu kabila za watu. Nihukumu Ee BWANA, kwa kadiri ya haki yangu, kwa kadiri ya uadilifu wangu, Ewe Uliye Juu Sana. Ee Mungu mwenye haki, uchunguzaye mawazo na mioyo, komesha ghasia za waovu na ufanye wenye haki waishi kwa amani. Ngao langu ni Mungu Aliye Juu Sana, awaokoaye wanyofu wa moyo. Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Mungu aghadhibikaye kila siku.