Zaburi 51:1-9
Zaburi 51:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Nihurumie, Ee Mungu, kadiri ya fadhili zako; ufutilie mbali makosa yangu, kadiri ya wingi wa huruma yako. Unioshe kabisa hatia yangu; unisafishe dhambi yangu. Nakiri kabisa makosa yangu, daima naiona waziwazi dhambi yangu. Nimekukosea wewe peke yako, nimetenda yaliyo mabaya mbele yako. Uamuzi wako ni wa haki hukumu yako haina lawama. Mimi ni mkosefu tangu kuzaliwa kwangu, mwenye dhambi tangu tumboni mwa mama yangu. Wewe wataka unyofu wa ndani; hivyo nifundishe hekima moyoni. Unitakase kwa husopo, nitakate; unioshe niwe mweupe pe. Nijaze furaha na shangwe, nifurahishe tena, mimi ambaye uliniponda. Ugeuke, usiziangalie dhambi zangu; uzifute hatia zangu zote.
Zaburi 51:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee Mungu, unirehemu, kulingana na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa uovu wangu, Unitakase dhambi zangu. Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu iko mbele yangu daima. Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu. Tazama, nikazaliwa nikiwa na hatia; Mama yangu akanichukua mimba nikiwa na dhambi. Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanifundisha hekima kwa siri, Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji. Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi. Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote.
Zaburi 51:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu. Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima. Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu. Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani. Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri, Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi. Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote.
Zaburi 51:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee Mungu, unihurumie, kwa kadiri ya upendo wako usiokoma, kwa kadiri ya huruma yako kuu, uyafute makosa yangu. Unioshe na uovu wangu wote na unitakase dhambi yangu. Kwa maana ninajua makosa yangu, na dhambi yangu iko mbele yangu daima. Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi na kufanya yaliyo mabaya machoni pako, ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo, na kuwa na haki utoapo hukumu. Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi, mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu. Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni, ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima. Nioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi, unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji. Unipe kusikia furaha na shangwe, mifupa uliyoiponda na ifurahi. Ufiche uso wako usizitazame dhambi zangu, na uufute uovu wangu wote.